Habari za Punde

Usafi wa mazingira kuadhimisha sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi waitikiwa vyema

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akishiriki na Wananchi, Vikundi ya vya usafi wa mazingira pamoja na Vikosi vya Ulinzi kwenye usafi wa mazingira hapo Kwahani Uwanja wa Farasi ikiwa ni kuanza rasmi kwa maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

 Baadhi ya wapiganaji wa Vikosi vya ulinzi wakishiriki zoezi la usafi wa mazingira katika Mtaa wa Kwahani Uwanja wa Farasi kuanza kwa shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 52.


Watendaji wa Baraza la Manispaa Zanzibar wakijumuika pamoja na Wananchi na Vikosi vya Ulinzi kwenye usafishaji wa mazingira hapo Mtaa wa Kwahani Uwanja wa Farasi Mjini Zanzibar.

Balozi Seif akimkabidhi vifaa vya usafi wa mazingira Mwenyekiti wa Kikundi cha Usafi wa Mazingira cha Kilimani { Kilimani City } Nd. Khamis Shaali Chum  { mwenye T. Shirt Nyeupe  }vilivyotolewa zawadi na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Idara ya Mazingira.

Kushoto ya Mwenyekiti huyo wa Kilimani City ni Mkurugenzi Maingira Nd. Juma Bakari Alawi na wa kwanza kutoka Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mazingira Zanzibar Nd. Juma Mjaja.

Picha na – OMPR – ZNZ.

NA Othman Khamis Ame, OMPR

Kazi za usafi wa mazingira  kwenye maeneo tofauti Nchini katika kuanza rasmi kwa maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeonekana kuitikiwa vyema na Wananchi walio wengi pamoja na vikosi vya ulinzi hapa Nchini.

Hali ya mazingira salama katika mtaa wa Kwahani Uwanja wa Farasi imeonekana kubadilika kidogo kutokana na juhudi kubwa iliyofanywa na washiriki wa zoezi hilo la usafi wa mazingira iliyoanza mapema asubuhi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alijumuika na Wananchi hao kwa kazi za usafishaji wa Mtaro wa maji machafu unaokusanya maji kutokea mitaa ya Muembe Njugu, Kwahani, Kariakoo, Kilimani na Kumalizikia Pwani ya Kilimani.

Wapiganaji wa Vikosi vya Mafunzo, Jeshi la Kujenga Uchumi, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo, Zimamoto na Uokozi, Valantia, vikundi vya usafi wa mazingira vilivyomo  ndani ya Wilaya ya Mjini, watendaji wa Baraza la Manispaa na Wananchi walionekana kuhamasika katika harakati hizo.


Akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhandisi wa Baraza la Manispaa Zanzibar Nd. Mzee  Khamis alisema Baraza la Manispaa limeanzisha mradi maalum wa usafi wa mazingira katika Manispaa ya Zanzibar kwa kuwashirikisha moja kwa Wananchi kwenye Mitaa yao.

Mhandisi Mzee alisema hatua hiyo itatoa fursa pana kwa kila mwananchi  kuona kwamba suala la usafi  wa mazingira ambalo linapaswa kuwa la kudumu linaigusa Jamii moja kwa moja badala ya kufikiria kuwa jukumu hilo ni la Baraza la Manispaa pekee.

Akitoa ufafanuzi wa kina Afisa Uhusiano wa Baraza la Manispaa  Zanzibar Moh’d Nassor Ali alieleza kwamba Baraza la Manispaa tayari limeanzisha mradi maalum wa kuimarisha Miundombinu katika uchimbaji wa mitaro { ZUSP } ndani ya Manispaa ya Mji wa Zanzibar wa lengo la kuujengea mazingira mazuri Mji wa Zanzibar katika miendendo ya maji machafu.

Moh’d Nassor alisema hatua hiyo kwa hivi sasa inaendelea katika eneo la Mtaa wa Mpendae { Maarufu kwa Binti Hamrani } kwa ujenzi wa Mtaro mkubwa kazi ambayo inakwenda sambamba na ujenzi wa mtaro kama huo katika Uwanja wa Michezo wa Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.

Akizungumza na washiriki wa zoezi hilo la usafi wa mazingira kwa ajili ya kuanza kwa shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 52 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza Wananchi pamoja na Vikosi vya ulinzi kwa ushiriki wao wa usafi wa mazingira.

Balozi Seif alisema  kwa vile Zanzibar imefanikiwa vyema katika kuangamiza Maradhi ya Malaria kwa asilimia 99% hakuna sababu  nguvu na hamasa kama hiyo  Wananchi wakachukuwa  juhudi ya kuielekeza katika usafi wa mazingira kwenye maeneo wanayoishi.

Alisisitiza kwamba kutokana na mabadiliko ya tabia Nchi  Ulimwenguni yaliyoathiri  Mataifa mbali mbali Duniani haitakuwa vibaya kwa Zanzibar kutenga siku maalum ya usafishaji wa mazingira mpango ambao tayari umekuwa ukifanywa na baadhi ya Nchi Duniani zikiwemo pia za Bara la Afrika.

Katika kazi hiyo ya usafi wa mazingira kuanza rasmi kwa maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi zawadi ya vifaa tofauti vya usafi wa mazingira  kwa Kikundi cha usafi wa Mazingira cha Kilimani  { Kilimani City }.

Vifaa hivyo vyenye Thamani ya Shilingi Laki Saba vimetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Idara yake ya  Mazingira ikiwa ni muendelezo wa utaratibu iliyojipangia wa kutoa zawadi za vifaa kila mwaka kwa Vikundi vilivyoonyesha juhudi katika kushiriki  kwenye usafi wa mazingira maeneo mbali mbali Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.