Habari za Punde

Balozi Seif: Kwa kuwa ZEC imeshatangaza tarehe ya marudio, mwenye malalamiko anaweza kwenda mahakamani

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Waandishi wa Habari hawapo pichani hapo uwanja wa ndege wa Pemba kabla ya kurejea Unguja baada ya kumaliza ziara ya Siku Tatu Kisiwani Pemba.

Kulia ya Balozi Seif ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Nd. Vuai Ali Vuai na Kushoto ya Balozi Seif ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Panadu Ameir Kificho.
Balozi Seif akijibubaadhi ya maswali ya Waandishi wa Habari alipokutana nao  uwanja wa ndege wa Pemba baada ya kukamilisha ziara yake ya siku Tatu Kisiwani humo.

Kushoto ya Balozi Seif ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Mh. Pandu Ameir Kificho, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Mwanajuma Majid na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Dr. Maua  Daftari.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwa vile Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeshatangaza Tarehe ya Kurejewa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar  yeye binafsi haoni umuhimu wa kurejewa kwa mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein .

Alisema mazungumzo hayo kwa sasa hayana tija yoyote kwa vile Wananchi katika kipindi hichi wameanza kujiweka tayari wakijiandaa kupiga kura kufuatia  Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC} kufuta matokeo ya uchaguzi Tarehe 28 Oktoba mwaka 2015.

Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye Uwanja wa ndege wa Pemba akijiandaa kurejea Kisiwani Unguja baada ya kumaliza ziara yake ya siku Tatu Kisiwani Pemba kukagua shughuli mbali mbali za Maendeleo akiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali Balozi Seif Ali Iddi alisema iwapo yapo malalamiko yoyote muhusika wake ana wajibu wa kwenda Mahakamani kwa hivi sasa.


Balozi Seif alisema mazungumzo ya pamoja kati ya Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi {CUF } Maalim Seif Sharif Hamad  kuhusu kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu yalifanyika kwa maombi ya Maalim Seif ambae yeye binafsi ndie aliyeamua kujiondoa kwenye maendeleo ya vikao vya mazungumzo hayo.

Alisema kinacholikabili Taifa kwa wakati huu ni suala la marejeo ya uchaguzi na kuwaomba watu walioamua kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio ni vyema wakabakia nyumbani ili kutoa fursa kwa wenzao waliokubali kushiriki watumie haki yao ya Kidemokrasia kuwachaguwa Viongozi wanaowataka.

Balozi Seif alifahamisha kwamba hata yeye anaheshimu maamuzi ya Tume ya Uchaguzi  ya Z anzibar ambayo haiwezi kuingiliwa na chombo chochote licha ya kwamba tayari alikuwa ameshashinda na kupewa cheti kinachothibitisha kuwa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda.

“Tupo tuliokwishashinda kwenye chaguzi zetu za Majimbo na kupewa vyeti vinavyothibisha ushindi huo lakini baadhi yetu kwa nini tuendelee kushutumu maamuzi ya tume ambayo kutokana na sababu za msingi ilizoeleza  za kujitokeza kwa dosari kadhaa kwenye zoezi zima ikalazimika kufuta matokeo na uchaguzi wote ? ”. Aliuliza Balozi Seif.

Akizungumzia uvumi uliojitokeza  wa kuwepo kikundi cha Vijana wanaopiga watu katika badhi ya maeneo maarufu Mazombi Balozi Seif alisema hana taarifa yoyote iliyomfikia akiwa kama Kiongozi wa Juu wa Serikali kuhusu shutma hizo.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa agizo kwa vyombo 
vya Ulinzi kufanya uchunguzi dhidi ya shutuma hizo na pale itakapobainika kuwepo kwa shutma hizo vifanye juhudi ya kuwakamata wahusika hao na kuwafikisha mbele ya Dola ili sheria ichukuwe mkondo wake.

Balozi Seif alieleza kwamba nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Ile ya Jamuhuri ya Mauungano wa Tanzania ni kuiona nchi inaendelea  kubakia katika hali ya amani na utulivu wakati wote kabla na baada ya uchaguzi.

Aliwaasa na kuwaomba Wananchi wa maeneo mbali mbali Kisiwani Pemba kuendelea kuishi kwa amani na upendo na kushirikiana katika mambo yao bila ya kuendekeza zaidi itikadi zao za Kisiasa ambazo tayari zimeshaonyesha muelekeo mbaya.

Alieleza kwamba matokeo ya sasa yaliyojichomoza katika hujuma za moto sambamba na baadhi ya watu kuanza kuashiria vitisho dhidi ya wananchi wenzao walioamua kushiriki uchaguzi wa marejeo kwa kuwatilia X nyumba zao yanaonyesha safari ya hatari katika maisha miongoni mwa jamii.

1 comment:

  1. Allah swt anajua nia zenu zaidi kuliko madhahir tunayoyaona bora zaidi kuitawala nchi kwa nia safi badili ya kukomoana na matusi kama mambo yanavyo endelea katika huko na nchi za kiarabu kwa sasa hasa nchi za kiislam ingawa mifano mingi imeonekana na viongozi bado hawataki kuachia madaraka hata kama roho za watu na mali za watu zinapotea na mifano ya hii senario za nchi zisizo za kiislamu imeonekana na mifano yake nchi za Somalia, Sudan, Syria, Iraq, Egypt, Afghanistan, Kashmiri Pakistan, Bosnia na nyingi nyenginezo kaeni mfikirie sana kwani kubomoa ni dakika 10 kujenga ni miaka kumi nchi zenu za kiafrika haziwezi kuhimili hasara hizo ni masikini kwa hivyo acheni ubinafsi na sikilizeni watu wanataka nini katika nchi yao la sivyo yatawapeleka pabaya. huo ni ushauri oneni syria leo kumebakia magofu ya majumba na watu wengi kuuwawa na wengi ni wakimbizi kisa ubishi kufanya kosa sio kosa bali kurudia kosa ni kosa Allah swt wanusuru waja wako zanzibar na kila pahala amin.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.