MATANGAZO MADOGO MADOGO

Thursday, February 25, 2016

ZEC Yaendelea na Matayarisho ya Uchaguzi wa Marudio Machi 20.

Na.Mwandishi Wetu.
Tume ya uchaguzi ya Zanzibar ZEC imesema maandalizi ya uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 marchi 2016 yamefikia hatua nzuri na  kazi ya uchapishaji wa daftari la wapiga kura itakuwa imekamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Mhe.Jecha Salim Jecha imesema kuwa madaftari ya wapiga kura yatakuwa nje ya vituo yatabandikwa wiki moja kabla ya uchaguzi  ili kuwapa nafasi wapiga kura kuelewa vituo walivyopangiwa.
Ameyataja matayarisho mengine yaliyokuwa katika hatua nzuri kuwa ni pamoja uteuzi wa wasimamizi wa Majimbo, upangaji wa vifaa na vituo, pamoja na mafunzo kwa watendaji.
Mhe.Jecha ameongeza pia  matayarisho ya awali ya uchapishaji wa karatasi za kura yamekamilika baada ya tume kumpitisha mchapishaji wa karatasi hizo na zinatarajiwa kuwasili nchini mwanzoni mwa mwezi wa Marchi.
Akizungumzia mawasiliano kwa vyama vya siasa na wagombea Mhe.Jecha amesema kuwa tume itaendelea kuwahesabu wagombea wote wa uchaguzi uliopita ni halali kutokana na kutofuata utaratibu wa kisheria za  kujitoa kwa wagombea.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi nambari 11 ya mwaka 1984 sura ya tatu kifungu cha 31 hadi 37a kinatoa sharti la kuwepo wadhamini wa wagombea na hakuna Chama kilichoiandikia tume kuwa kimefuta udhamini wa wagombea wake kushiriki katika uchaguzi huo.