Habari za Punde

Dk Shein: WanaCCM Msichokozeke.


                                STATE HOUSE ZANZIBAR                                                         

 OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
                                           PRESS RELEASE                                              
                                                                                                                                                                          05 Machi, 2016  
                                           TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wanachama na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa na subira na wasikubali kuchokozeka kufuatia vitendo vya uchokozi vinavyofanywa na baadhi wa watu dhidi yao na mali za chama hicho.

Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amesema hayo jana mara baada ya kutembelea maskani ya Mwembekisonge iliyopo Michenzani mjini Unguja kufuatia maskani hiyo kuharibiwa kutokana na mripuko uliotokea Alhamisi usiku.

Kwa mujibu wa Katibu wa Maskani hiyo Mzee Yunus mlipuko huo ulitokea kati ya saa 6 na 6 na nusu usiku wa siku hiyo na kusababisha hasara kwa kuharibu ofisi hiyo na baadhi ya vifaa vilivyokuwemo.

“CCM tunatii sheria za nchi lakini Jeshi la Polisi lazima litimize wajibu wake kwa kuwatafuta waliofanya kitendo hiki na kuwapeleka katika vyombo vya sheria” Dk. Shein aliwaeleza wananchi na viongozi waliokuwepo katika eneo hilo.

Katika mnasaba huo amelitaka Jeshi la Polisi Zanzibar kufanya uchunguzi wa haraka na kuwabaini waliohusika na kitendo hicho na kuhakikisha kuwa wanafikishwa katika vyombo vya sheria mara moja.

Aliahidi kusaidia maskani hiyo kufanya ukarabati wa sehemu iliyoharibika ili shughuli za maskani ziweze kuendelea.
Wakati huo huo akijibu maswali ya waandishi wa habari waliokuwepo katika eneo hilo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alisema uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika tehere 20 Machi, 2016 utakuwa huru na wa haki.

Kuhusu suala la usalama Dk.Shein aliwahakikishia wananchi kuwa amani na utulivu itaendelea kuwepo Unguja na Pemba na kuongeza kuwa ulinzi na usalama wakati wote utaimarishwa ili kuhakikisha wananchi wote wenye haki ya kupiga kura wanafanya hivyo kwa mujibu wa Katiba na Sheria.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax:024 2231822 

1 comment:

  1. huwo mripuko unaonekana umetokea kwa ndani halafu munasema nini? munajifanya muna akili sana lakini mungu hayupo pamoja na nyinyi ndo mana munaadhirika.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.