Na Haji Nassor, Pemba
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesikitishwa na
kulaani vikali, matukio zaidi ya manane ya uchomaji nyumba za wananchi, matawi
ya vyama pamoja na majengo ya serikali yaliojitokeza kisiwani Pemba, usiku wa
kuamkia Machi 12 mwaka huu.
Akitoa taarifa ya
Serikali waziri wa nchi afisi ya Makamu wa pili Zanzibar Mhe: Mohamed Aboud
Mohamed mjini Chakechake, alisema serikalili hairidhishwi hata kidogo na
matendo hayo.
Alisema serikali
kila siku imekuwa ikipiga kelele kwa wananchi kuendelea kuishi kwa amani na
utulivu, ikiamini kuwa ndio msingi wa kufikia maendeleo ya kweli.
Waziri Aboud
alisema suala la siasa kuitia moyoni hadi kupelekea kutiliana moto, sio jambo
jema na wala sio malengo ya kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi nchini.
Alieleza kuwa,
suala la uchomaji moto, haliashirii mwisho mwema miongoni mwa wananchi, na ndio
maana amewataka wananchi waliokumbwa na matukio hayo, kuwa wastahamilivu na
serikali inaendelea kuwatafuta wahusika, ili wafikishwe mbele ya vyombo vya
sheria.
“Serikali kwa kupitia
Jeshi la Polis, linaendelea na uchunguzi wa hali ya juu, ili kuwapa wahusika na
kisha sheria ichukuwe nafasi yake, maana matendo haya sio ya kuyavumilia’’, alifafanua.
Alibainisha kuwa
kuanzia kipindi cha mwezi Febuari mwaka huu, kumeanza kujitokeza tena matukio
mbali mbali ya kuashiria uvunjifu wa amani yakiowemo hayo ya utiwaji wa moto.
Alisema tayari
jumla ya nyumba nane za wananchi zimeshateketezwa kwa moto, ikiwa ni pomoja na
shehia ya Kangagani nyumba mbili, Mihogoni, Tondooni moja moja.
Nyumba nyengine
ambazo zimeshateketezwa kwa moto na watu wasiofahamika ni shehia ya Msuka,
Makangale na Tumbe kukiwa na nyumba moja moja, Maskani ya CCM Junguni, tawi la
CCM Tibirinzi, na kituo cha afya Kiuyu.
Kuhusu hasara
ambayo imepatikana kutokana na matukio hayo manane ambayo yaliripotiwa juzi,
kutoka Idara ya maafa, alisema, ni wastani wa shilingi milioni 200 (shilingi
milioni mia mbili), ambapo serikali baadae itawafidia wananchi hao.
Katika hatua
nyengine waziri huyo wa afisi ya makamu wa pili wa rais Zanzibar, Mohamed Aboud
Mohamed, aliwataka wananchi wenye sifa za kupiga kura kwenye uchaguzi wa
marudio, kujitokeza kwa wingi bila ya woga.
“Keshokutwa
tunakabiliwa na uchaguzi, wala wananchi wasiwe na hofu waende kwenye vituo
walivyopangiwa na serikali itaimarisha ulinzi kama kawaida’’,alifafanua.
Hata hivyo waziri
Aboud amerejea kauli yake, kuwa serikali haitosita kuwanyang’anya leseni
wafanyabiashara yoyote atakaebainika kuendesha mgomo wa utoaji huduma.
“Serikali inarudia
kila siku tamko lake, kwamba itawanyng’anywa lesini wafanyabiasha hata akiwa
chama gani, kama atatoa huduma kwa njia ya ubaguzi’’,alisisitiza.
Usiku wa kuamkia
juzi Machi 12 hasa mkoa wa kaskazini Pemba kuliripotiwa matukio ya uchomaji
moto nyumba za wananchi, matawi ya CCM, na kituo cha Afya cha Kiuyu na watu
wasiofahamika.
No comments:
Post a Comment