Na Haji Nassor, Pemba
“Haki mbele ya sheria, haki na uhuru wa mtu binfasi, uhuru wa maoni’’, zote ni haki mama ambazo zinatokana na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Haki ya kupiga kura, usawa mbele ya sheria, uhuru wa maoni, ambazo nazo ni haki za kikakatiba, utazikuta ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kuanzia Ibara yake ya 5 hadi 18 zikiwa zimetuliwa.
Na walishasema wanaozifahamu sheria kuwa, hata ukiikuta haki imetajwa ndani ya katiba moja kwa moja, basi huwa ni vigumu haki hiyo kumpokonywa muhusika.
Naamini haki hizi zimewekwa na wanaadamu sisi, lakini kwa hapa basi nisema walikwenda ndipo, maana kwa mfano kama hakuna haki ya maoni, kusingekuwa na usawa.
Wapo walioiita Katiba kuwa ni sheria mama, wangine wakaitaja kama ndio uti wa mgongo wa taifa lolote lile, lakini pia wapo walioitaja kuwa ndio dira ya leo na kesho.
Katiba inapotaja kitu kuwa ni haki ya muhusika, huwa hakuna mwengine mwenye nguvu ‘mandate’ ya kuichukua haki hiyo na wala kumshawishi kutoitekeleza.
Kwa mfano kwa Ibara ya 5 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imetaka uwepo wa haki ya kupiga kura kwa kila mtanzania alietimiza masharti moja likiwa ni umri wa miaka 18.
Kuwepo ndani ya katiba kwa jambo hilo, hakukutosha tu, maana kisha bunge likatunga sheria mwaka 1985, juu ya kukazia haki hii ya kupiga kura na ndani yake kuwepo ya kuchagua na kuchaguliwa.
Na hata Baraza la wawakilishi Zanzibar mwaka 1984, nayo ilichukua nafasi kutunga sheria ya uchaguzi no 11 ya mwaka huo, ili kulitia nguvu hili la kupiga kura.
Kumbe suala la kupiga kura halipo kiutashi wala halikuwekwa kwa bahati mbaya, lengo ni kuwapa nafasi wanawake na wanaume wenye sifa kuchagua viongozi wawatakao.
Mwaka huu 2015, Oktoba 25 taifa la Tanzania, liliingia kwenye ngwe ya kidemokrasia ya uchaguzi mkuu wa vyama vingi, ambao wengi walishiriki na wapo waliotimiza ndoto zao za kikatiba kwa kuwapigia kura wawatakao.
Maana Mratibu wa Kituo wa Kituo cha Huduma za Sheria ZLSC tawi la Pemba Fatma Khamis Hemed, akinukuu sheria, alishasema kuwa ‘haki ya kupiga kura ni ya mtu binafsi’.
“Haki ya kupiga kura sio ya mke kwa muumewe, wala mtoto kwa baba yake, bali ni mtu mmoja mmoja maana ni haki asili aliopewa na katiba’’,alisema.
Kwa Zanzibar haki ya kupiga kura hasa kwa walio kwenye ndoa wapo walioitumia ipasavyo, na wengine kuwekewa vikwazo na waume zao.
Wapo wanawake ambao kwa utashi wa waume zao, eti pia suala la kikatiba la kupiga kura na kuchagua kiongozi amtakae wa chama apendacho, kimo ndani ya mamlaka ya muume.
Wapo wanawake wenye uwelewa wa haki ya kupiga kura, kuwa ni mtu na wala sio ya mamlaka ya ndoa na sasa wametelekezwa na wenzao kwenye ndoa.
Zanzibar imekuwa ikitajwa kwenye ramani ya ulimwengu kuwa, lipo kundi lenye kuamini dini ya kiislamu kwa asilimia 99, sasa suali kwako msomaji ndo kwa ‘staili’ hii?
Wanawake waliojaribu kufuatilia mikutano kadhaa ya kampeni kama walivyo wanaume, lengo apate kumchagua kiongozi na chama atakacho.
Sasa baada ya kupingana na amri za waume zao, ndio leo baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 Zanzibar, wapo wanawake 47 wameshapewa talaka na kutengana na familia zao kwa sababu hizo.
Wanawake hao walitalikiwa na kwa madai yaa kutotii amri za waume zao, ambao waliwataka kutokwenda kupiga kura, kutokana na kutofautiana kwa itikadi za vyama.
“Mimi wangu aliniambia kama naenda kupiga kura lazima tufuatane ili akanisaidie kunipigia, nilipokataa ikawa ndio sababu ya kuachwa’’,alisema mama (30) wa Mkoani.
Yeye anasema Oktoba 24 alielezwa na mumewake ambae anaamini wako vyama tofauti, kwamba aidha asiende kupiga kura au aongozane nae hadi kituoni ili amsaidie.
Alipodahili juu ya hilo na hasa kwa vile uchaguzi wa mwaka 2010 pamoja na ujauzito aliokuwa nao alipiga mwenyewe, alielezwa na mumewake kuwa uchaguzi wa mara hii ni wa aina yake.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA, Zanzibar Mzuri Issa, anasema katika uchaguzi huo wanawake wengi walikumbwa na udhalilishaji wa kulazimishwa kupigia kura chama fulani kinyume na ridhaa yao.
Lakini wapo wanawake wengine 24 waliotishiwa kupewa talaka, ikiwa watahudhuria mikutano ya kampeni ama watapiga kura na matokeo yake hawakwenda kupiga kura.
“Wanawake wanne (4) waliambiwa wasipige kura na walipiga kura, lakini hawakuachwa, ambapo mmoja kati ya hao katelekezwa baada ya kukataa amri ya kuhudhuria mkutano wa kampeni,” alisema Mzuri.
TAMWA imelaani baadhi ya wanaume wanaoendesha udhalilishaji hata wa kikatiba, na kwamba jambo la lazima kwa serikali kuu ichukue hatua.
Ali Mussa Kombo (55) wa Chake chake, anasema wapo wanaume wameingia kwenye ndoa pasi na kupata misingi ya jambo hilo, na matokeo yake ni kuhusisha mamlaka walionayo na kupiga kura.
Hassan Rajab Juma (32) wa Mkoani, yeye anafafanua kuwa inawezekana hayo yamejiri kutokana na uchaguzi wa mwaka huu, kuwa na hisia za pekee.
“Na pengine sasa wanaume hao kuwaacha wake zao wanajuta, illa jua kuwa mwandishi uchaguzi wa mwaka huu ulikua wa mfano, ndio maana wengine wamepoteza ndoa zao”,alisema.
A…aaa…. mimi mke wangu yuko chama tofauti na mimi tokea uchaguzi uliopita na wala hakuna mtikisiko wa ndoa, alinijibu nilipotaka kujua, juu ya msimamo wa ndoa yake na siasa.
Wakati tayari Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC, ikiwa imeshatangaaza tarehe 20 Machi mwaka huu ndio uchaguzi wa marejeo chonde chonde wanaume waliokwenye ndoa hao wanawake wasisulubiwe.
Iweje wanawake wanapofanya uamuzi wa kuchagua viongozi wawatakao kisha wasulubiwe na waume kwa sababu ya kutofautiana kichama.
Ndio tumeshashuhudia kwa uchgauzi wa awali, wanawake wakipindwa kwa kutimiza ndoto zao za kikatiba, sasa huu unaitwa udhalilishaji kwenye siasa.
Shifaa Said kutoka TAMWA juzi akizungumza na waandishi kwenye mafunzo ya usuluhishi wa migogoro, alisema sasa udhalilishaji umeshahamia hata kwenye haki ya kikatiba.
“Jamani lazima waandishi muielezea jamii kuwa, mwanamke ana haki ya kuachagua na kuchaguliwa kama alivyo mwanamme, sasa na huu uchagauzi wa marejeo haya yasijitokeze’’,alisema.
Sharifa Ali Haji wa Mtemani Wete, anasema wapo wanaume wasoiofahamu wajibu wao, na ndio maana huwataka kuwadhibiti wake zao hata kwenye haki za kisisasa.
Mohamed Haji Kassim (50), wa Mtambile anasema ukosefu wa elimu ya ndoa ndio chanzo cha yote waliofanyiwa baadhi ya wanawake kwa uchaguzi uliopita.
Mwanaharakati na mtetezi wa haki za wanawake ambae ni mwandishi wa zamani Valarie Msoka, anasema lazima wanaume waelewa kuwa mamlaka kwa wake zao yanamipaka na sio kila jambo.
“Mimi siamini kwamba hata suala la haki ya kuchagua liwe mikononi mwa mwanamme, sasa lazima waelewa hilo maana hii ni haki ya kikatiba na hakuna mtu wala mamlaka yenye uwezo wa kuwapokonya’’,alisema.
Chonde chonde, wanaume ni vyema kuhakikisha suala la haki ya kuchagua haliwasulubu wanawake kwenye uchaguzi wa marejeo mwezi Machi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment