Habari za Punde

ZSTC Kuwapiga Jeki Wananchi Wanaoanzisha Vitalu vya Kuatikia Mikarafuu Zanzibar.


Mkulima wa vitalu vya karafuu wa Kitope Mzee Sheha Khamis akimuelezea Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la ZSTC changamoto anazokabiliana nazo katika kutekeleza kazi hiyo wakati Mkurugenzi huyo alipofanya ziara katika Mkoa Kaskazini Unguja na Wilaya Kati.
 Kitalu cha Mikarafuu cha Serikali cha Donge Mwanakombo kikionekana kikiwa na miche ya kutosha ikiwa tayari kupewa wakulima wa zao hilo wakati wa mvua za masika zitakapoanza mwezi ujao.
 Mfanyakazi wa kitalu cha Mikarafuu  cha Donge Bi Fatma akitayarisha udongo kwa ajili ya kuatika miche  katika shamba hilo linalomilikiwa na Wizara ya Kilimo na Mali Asili.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC Bibi Mwanahija Almasi akizungumza na waandishi wa habari katika kitalu cha S erikali cha Kivunge baada ya kumaliza ziara ya siku mbili kutembelea vitalu vya mikarafuu vya Mkoa Kaskazini AUnguja na Wilaya ya Kati

Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Mali Asili linakusudia kuongeza  mashirikiano   na  kuwasaidia wananchi wanaoanzisha vitalu vya mikarafuu Unguja na Pemba.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC  Bibi Mwanahija Almasi ametoa ahadi hiyo baada ya ziara yake ya siku mbili kutembelea vitalu vya mikarafuu vya Serikali na  vya watu binafsi katika vijiji vya Kitope, Kidimni, Machui Selem na Donge kuona matatizo yanayowakabili katika kutekeleza kazi zao.

Amesema vitalu vya watu binafsi vinamchango mkubwa katika  kuimarisha zao la karafu  Zanzibar kwa kuziba pengo linalojitokeza  wakati wa ugawaji wa miche ya mikarafuu kwa wakulima kutoka  vitalu vya Serikali

Amesisitiza kuwa  kutoakana umuhimu huo na kazi kubwa wanayochukua  wakulima hao huku wakikabiliwa na upungufu  wa nyenzo muhimu, Shirika litatoa pembejeo  zitakazosaidia  kufanikisha kazi zao  kwa ufanisi.
Wakati wa ziara hiyo wakulima  wanaomiliki  vitalu vya mikarafuu walimueleza 

Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC kwamba wanakabiliwa na tatizo la vifuko vya kuatikia miche (policing), mabero, pauro na maji hasa wakati wa kiangazi.
Mkurugenzi Mwendeshaji amewataka wakulima  hao kutovunjika moyo na changamoto wanazokabiliana nazo  na waendelee kushirikiana na maafisa wa Kilimo wakati Shirika linafanya juhudi za kupunguza changamoto zao.

Hata hivyo Bi Mwanahija amewashauri wenye vitalu vya mikarafuu baada ya kupata msaada kutoka  ZSTC   kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya  kuuzia miche ya  mikarafuu kwa wakulima ambapo hivi sasa wanauza shilingi 1000 kwa mche mmoja.


Amesema Serikali itaendelea kutoa miche ya mikarafuu bure kwa wakulima lakini vitalu vya Serikali viliopo hivi sasa haviwezi kukidhi mahitaji ya wakulima wote wa zao hilo, hivyo vitalu vya watu binafsi vitaendelea kuwa tegemeo kwa wakulima

“Wakulima  wa vitalu vya  Mikarafuu mumekuwa na mchango  mkubwa katika kuendeleza  na kuimarisha zao la karafuu Zanzibar lakini  wapunguzieni wakulima  bei ya miche ingawa gharama mnazotumia ni kubwa,” Bi Mwanahija aliwashauri.

Bibi Mwanahija amewaelekeza  maafisa Kilimo kuwapa wakulima miche  ya mikarafuu wanayoweza kuihudumia  kwani uzoefu unaonyesha wakulima huchukua miche mingi wasiyoweza   kuitunza na  hatimae inakufa  mara tu baada ya kumaliza mvua za masika.

Mkuu wa Vitalu kutoka Wizara ya Kilimo Rashid Nassor Rashid alimueleza Mkurugenzi Muendeshaji wa ZSTC kwamba vitalu  vya Serikali   vinakabiliwa na upungufu  mkubwa wa wafanyakazi  baada ya wengine kustaafu  na baadhi yao  kuzeeka hivyo wanampango wa kuajiri  wafanyakazi wa muda  kwa kazi za dharura kuziba pengo liliopo.

Amesema kazi  ya kutafuta mbegu  (matende) kwa ajili ya vitalu vya mikarafuu zinachukua muda mfupi kabla ya mvua za masika kuanza na  ikiwa  kazi hiyo haitofanywa kipindi cha sasa kazi hiyo itashindwa kutekelezwa.

Mkuu wa usimamizi wa zao la Karafuu kutoka Wizara ya Kilimo na Mali Asili Badru Kombo Mwemvura amemuhakikishia Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC kwamba iwapo wakulima watafuata maelekezo ya wataalamu wa kilimo lengo la Serikali la kuongeza uzalishaji wa Karafuu litafika muda mfupi ujao.

Amesema tatizo la wakulima wa zao la karafu ni kuchukua miche mingi bila ya kuwa na uwezo wa kuihudumia  na baadhi  yao huchelewa kuipanda  baada ya kuchukua hatimae hufa huku wengine wakikosa kabisa.

Ameongeza kuwa mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa yakiathiri sana nchi  za visiwa nayo imekuwa changamoto kubwa kwa kilimo cha zao la Karafuu na mazao  mengine Zanzibar.

Wizara ya Kilimo ilipanga kutoa miche ya Mikarafuu milioni moja kwa wakulima wa zao hilo Unguja na Pemba, kuanzia mwezi wa April, lakini kutokana na ukosefu wa mbegu ulijiotokeza mwaka jana  kiwango hicho huenda kikapungua . 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.