Habari za Punde

Balozi Seif Atembelea Eneo la Jumba la Treni Darajani leo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali  Iddi akikagua harakati za uwekwaji wa uzio katika Jumba la Treni Darajani kwa ajili ya matengenezo makubwa ya Jumba hilo yanayofanywa na Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF }Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohammed Mahmoud.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mh. Haji Omar Kheir aliyevaa suti ya Bahari akimpatia maelezo Balozi Seif  wa kwanza kutoka kulia juu ya hatua zinazochukululiwa za mwanzo wa matengenezo mkubwa ya Jumba la Treni liliopo Darajani Mjini Zanzibar.
Kula ya Balozi Seif ni Meneja Mipango, Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Khalif Muumin Hilal, Meya wa Manispaa ya Zanzibar Mstahiki Khatib Abdulrahman Khatib na nyuma ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Joseph Abdulla Meza.
Wa kwanza kulia ni Meneja Utawala na Rasilmali Watu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Makame Mwadini Silima na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimwa Ayoub Mohammed Mhmoud.
Meneja Mipango, Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Khalif Muumin Hilal akimuonyesha Balozi Seif Ramani ya Matengenezo makubwa ya Jumba la Treni Darajani.Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimwa Ayoub Mohammed Mhmoud.(Picha na –OMPR – ZNZ.)

Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameonya kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitakuwa tayari kulipa fidia kwa hasara ya mali au vitu vya mtu yeyote atakayeendelea kukaidi agizo la Serikali la kuhama ndani ya Jengo la Treni liliopo Drajani Mjini Zanzibar kupisha ujenzi wake.

Onyo hilo alilitoa wakati alipofanya ziara fupi mapema asubuhi kuangalia maandalizi ya utiaji uzio kuzuunguusha eneo hilo kwa lengo la kuanza kazi ya Matengenezo makubwa ya jengo hilo yaliyoanza rasmi Tarehe 4 Mwezi huu wa sita 2016.

Balozi Seif Ali Iddi alisema msimamo unaotolewa na Serikali katika kutekeleza majukumu yake ya kuendesha Nchi katika miradi ya Kiuchumi na Maendeleo lazima uheshimiwe na kila Mwananchi awe Mtu wa kawaida na hata Kiongozi wa ngazi ya juu.

Alisema kazi za matengenezo makubwa ya Jumba la Treni Darajani itaendelea kama ilivyopangwa chini ya Mradi utakaosimamiwa na mfuko wa Hifadhi Zanzibar { ZSSF } na hakutakuwa na mjadala wowote utakaosababisha kuzoroteshwa kwa kazi za ujenzi huo.

“ Kazi hii haina msalie Mtume kwa sasa na Viongozi na watendaji wa kazi hiyo wamechoka kusikia sifa za baadhi ya watu kusifu miji mengine mizuri Duniani wakati miongoni mwao ndio wanaohusika kuzorotesha miradi inayoanzishwa hapa Nchini ”. Alisema Balozi Seif.




Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba zoezi la kupisha ujenzi huo halitakuwa na ajizi tena kwa wakati huu kwa vile muda waliopewa watumiaji wa Jumba hilo umeshapindukia mpaka.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ  Mh. Haji Omar Kheir  alisema Serikal iliunda Kamati Maalum  kuangalia hali halisi ya mazingira ya  Jumba hilo chini ya Mwenyekiti wake Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira.

Waziri Haji alisema ripoti ya Kamati hiyo iliyowasilishwa Serikali ilishauri   kufanyiwa matengenezo makubwa Jumba hilo kutokana na ubovu wake ambao ungeweza kusababisha maafa kwa wakaazi waliomo ndani yake pamoja na wanaopita karibu na eneo hilo.  

Alisema watumiaji wa Jumba hilo ambao asilimia 70% tayari wameshahama walipewa barua za kupisha ujenzi huo na kutakiwa kuhama ifikapo Tarehe 4 mwezi huu bila ya kuwa na mjadala  wa vikao au mikutano mengine yoyote  ile kati yao na Serikali Kuu.

Waziri Haji alimfahamisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hatua hiyo imekuja kufuatia watumiaji hao kuomba kupishwa kuendelea na shughuli zao za Kibiashara katika mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani wa mwaka uliopita na kuendelea na pirika zao hadi kutolewa kwa uamuzi huo wa kuhama kwa mara ya Pili.

Akitoa ufafanuzi wa mazingira ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uendelezaji na Uhifadhi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani alisema Jumba la Treni limejengwa mnamo mwaka 1880.

Nd. Sarboko alimueleza Balozi Seif kwamba Jumba la Treni ni kati ya Majumba Elfu 2,632 yaliyomno ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar ambapo Jumba hilo ni miongoni mwa Majumba 26 ya Daraja la kwanza yasiyotakiwa kubadilishwa maumbile yake kwa kujibu wa uhifadhi wa majengo la asili.

Alisema Wataalamu wa Mamlaka ya Uendelezaji na Uhifadhi  wa Mji Mkongwe  wa Zanzibar wataendelea kufuatilia Matengenezo ya Jumba hilo kwa lengo la kulinda na kuhifadhi urithi wa Kimataifa uliomo ndani ya Mji Mkongwe za Zanzibar  chini ya Usimamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,Sayansi na Utamaduni{ Unesco}.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohammed  Mahmoud  alisema Operesheni ya Pili ya Uimarishaji wa Mji wa Zanzibar  katika eneo linaloanzia Malindi hadi Darajani itaanza rasmi Mwezi Sita wa Kiislamu mara baada ya kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Mh. Ayoub alisema opereshni hiyo itahusisha uondoshwaji wa makontena ya Biashara mchanganyiko yaliyopo mbele ya Skuli ya Darajani ili kupisha ujenzi wa bustani pamoja na maegesho ya Gari.

Mapema akitoa maelezo ya ujenzi Meneja Mipango, Uwekezaji na Utafiti wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Nd. Khalif Muumin Hilal alisema Jumba la Treni litakalokuwa na hadhi ya Kisasa kama majengo mengine Duniani litazingatia huduma zote muhimu za lazima anazostahiki kuzipata mwanaadamu.

Nd. Muumin alisema ghorofa ya juu ya jengo hilo litakapomalizika likiwa na lifti Tatu kati ya hizo mbili zikihudumia sehemu ya maduka, litakuwa na sehemu ya makaazi ya watu katika eneo la juu, wakati sehemu ya chini itaendelea kutoka huduma za maduka kama lilivyokuwa uasili wake.

Alieleza kwamba ujenzi huo pia utazingatia uwepo wa sehemu za mazoezi , huduma za mitandao ya Habari na Mawasilano { internet , bustani pamoja na eneo maalum la mbele kwa ajili ya maegesho ya gari za watu watakaofika kupata huduma kwenye jengo hilo.

Kamati Maalum  ya kuangalia hali halisi ya mazingira ya  Jumba la Treni chini ya Mwenyekiti wake Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira ilijumuisha wajumbe Watano ambao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Bishara, Viwanda na Masoko pamoja na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar.

Wengine Waliokuwa wakialikwa katika vikao vya Kamati hiyo ni pamoja na  Mkuu wa Mkoa Mjini Mgharibi, Mkurugenzi wa Idara ya Mipango Miji, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uendelezaji na Uhifadhi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar pamoja na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.