Habari za Punde

Balozi Seif Akutana na Ujumbe wa Benki ya Exim ya China

Balozi wa China Bwana Lu Youqing kupokea Ripoti aliyoiomba  kutoka kwa Balozi Seif Ali Iddi inayofafanua kwa kina mikataba ya miradi ya upanuzi wa sehemu ya Maegesho ya Ndege kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar ili kusaidia ukamilishaji wa miradi hiyo.

Makabidhiano ya Ripoti hiyo yamefanyika Nyumbani kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Bara bara ya Haile Sellasie Jijini Dar es salaam.
Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Lu Youqing aliyepo kati kati akimueleza Balozi  Seif ujio wa Ujumbe wa ngazi ya Juu ya Benki ya Kimataifa ya China ya Exim kwa lengo la kukagua miradi inaqyofadhiliwa na Taasisi hiyo ya Kifedha.

Makamu wa Pili w Rais wa Zanzibar Balozi Seif Kushoto akibadilishana mawazo na Balozi wa China Nchini Tanzania Bwana Lu Youqing aliyepo kati kati baada ya kukamilisha mazungumzo yao Jijini Dar es salaam.

(Picha na – OMPR)

Na. Othman Khamis. OMPR. 
Ujumbe wa Benki ya Kimataifa ya Jamuhuri ya Watu wa China  ya Exim Bank ukiongozwa na Mkuu wa Benki hiyo unatarajiwa kuwasili Zanzibar mnamo Tarehe 21 Mwezi huu wa Saba kwa ziara rasmi ya kutembelea miradi inayofadhiliwa na Taasisi hiyo ya Kifedha ya Nchini China.Balozi wa Jamuhuri ya Watu wa China Nchini Tanzania Bwana Lu Youqing alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo yake Nyumbani kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Bara Bara ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam kufuatia muendelezo wa  mazungumzo yao kuhusu miradi inayofadhiliwa na Serikali ya China kupitia Benki ya
Exim.


Mazungumzo hayo yamekwenda sambamba na Balozi wa China Bwana Lu Youqing kupokea Ripoti aliyoiomba  kutoka kwa Balozi Seif Ali Iddi inayofafanua kwa kina mikataba ya miradi ya upanuzi wa sehemu ya Maegesho ya Ndege kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar ili kusaidia ukamilishaji wa miradi hiyo.

Balozi Lu Youqing alisema ujumbe huo wa Benki ya Exim utatembelea na kuona maendeleo ya ukamilishaji wa ujenzi wa sehemju ya Maegesho ya Ndege katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amaani Abeid Karume Kisauni pamoja na kukagua eneo la Mpiga duri linalotarajiwa  kujengwa Bandari ya Kimataifa ya upakizi na ushushaji wa Mizigo.

Balozi Lu alifahamisha kwamba pamoja na ziara hiyo ujumbe huo pia utafanya mazungumzo ya pamoja na Mawaziri wanaosimamia Wizara za Fedha na Mipango na Ujenzi, Miundombinu na Mawasiliano na watendani waandamizi katika jitihada za kuongeza nguvu za kukamilisha miradi
hiyo.

Alisema ripoti aliyoipokea kutoka kwa Balozi Seif itamrahisishia kazi yake ya ufuatiliaji  wa muendelezo wa miradi hiyo na kuelezea faraja yake kwamba uhusiano kati ya Jamuhuri ya Watu wa China na Zanzibar utaendelea kuimarika zaidi kwa karne nyingi ijayo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar inaendelea kuthamini hatua zinazochukuliwa na Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Benki yake katika kufadhili miradi mbali mbali ya Maendeleo na Uchumi Visiwani Zanzibar.

Balozi Seif alisema Jamuhuri  ya Watu wa China imeonyesha wazi kuguswa kwake na harakati za kimaendeleo zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajengea miundo mbinu imara  Wananchi wake kwenye sekta tofauti zitakazosaidia kuwakwamua kutokana na ukali
wa maisha.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Balozi zake za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika kuunga mkono miradi ya Maendeleo ya Wananchi wa
Zanzibar.

Balozi Seif Ali Iddi yupo nyumbani kwa Dar es salaam kwa mapumziko mafupi akiwa njiani kujiandaa kuelekea Mjini Dodoma kuhudhuria vikao vya juu vya Chama cha Mapinduzi ukiwemo Mkutano Mkuu Maalum wa CCM wa kumkabidhi Uwenyekiti Rais wa sasa Dr. John Pombe Magufuli.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.