Habari za Punde

Dk Shein ahutubia Baraza la Eid na kusisitiza wajibu wa viongozi wa siasa kuhimiza utiifu wa sheria, amani, utulivu na upendo

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                      06 Julai, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Viongozi wa vyama vya siasa wamekumbushwa kuwa ni wajibu wao kuhimiza utiifu wa sheria, amani, utulivu na usalama wa nchi pamoja na kuhamasisha upendo miongoni mwa jamii.

Akizungumza katika Baraza la Eid leo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein alieleza kuwa viongozi hawapaswi kuhamasisha wafuasi wa vyama vyao kufanya vitendo vya hujuma na kuleta sintofahamu katika jamii na kuvuruga amani na utulivu uliopo.

Alisema kuwa viongozi hao kuwachochea wafuasi wao kufanya vitendo kama hivyo ni “kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu” na kutolea mfano vitendo ambavyo vimekuwa vikifanyika kisiwani Pemba tangu baada ya kufanyika uchaguzi mkuu.

Alifafanua kuwa vitendo vya kibaguzi, kuharibu mazao, miti na mimea ya chakula pamoja na biashara ni kuzikufuru neema za Mwenyezi Mungu ambazo kila mwanadamu anapaswa kuzienzi na kumshukuru Mola kwa ukarimu wake huo.

“Ni wajibu wetu kuzishukuru neema tulizobarikiwa na Mwenyezi Mungu kwa kuziheshimu, kuzitunza vizuri, badala ya kuonesha kiburi, kuzidharau na kutozijali” Dk. Shein alieleza.Alisema ni bahati mbaya kuwa baadhi ya vitendo hivyo vimefanyika ndani ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambao una mafunzo makubwa kwa kila muumini.

“Mafunzo tunayopata katika saumu hayatufundishi ubaguzi, dharau, kejeli na kiburi miongoni mwetu.Tunapaswa kurudi kwa Mola wetu kwa kuyazingatia maamrisho yake” Dk. Shein aliwaasa wanaotenda vitendo hivyo.

Katika mnasaba huo, alitoa wito kwa kila mwananchi kuwa makini na watu ambao wanavuka mipaka na kudharau mafunzo ya dini, mila na tamaduni.

Sambamba na kauli hiyo Dk. Shein alitoa wito kwa viongozi hao wa siasa kufanya siasa kwa mujibu wa sheria, Katiba na maadili ya vyama vya siasa na kusisitiza umuhimu wa kushindana bila ya kugombana na kudharauliana.

Dk. Shein alibainisha kuwa utekelezaji wa shughuli za serikali unategemea sana sio tu ushirikiano kati ya serikali na wananchi bali pia kuwepo kwa amani na utulivu nchini hivyo alito wito kwa kila kiongozi na mwananchi kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu.

Alionya dhidi ya vitendo vya kujaribu kuzorotesha utekelezaji wa mipango ya serikali na kutoa tahadhari kuwa hatomvumilia mtu yeyote au kikundi chochote “kitakachojaribu kutuchelewesha kwa mbinu yoyote ile utekelezaji wa majukumu ya serikali”.

Alisisitiza kuwa malengo ya mipango ya maendeleo inaweza kufikiwa ikiwa wananchi wataongeza ushirikiano wao kwa serikali na kuwataka wananchi kuzipuuza habari za kuwepo uchaguzi mwingine au kuundwa serikali ya mpito.

“Hayo yanayosemwa mitaani ni sadiki ukipenda na upotoshwaji wa makusudi, uchaguzi umekwisha hakuna uchaguzi mwingine hadi  hapo mwaka 2020” 

Dk. Shein aliwaeleza viongozi na wananchi kupitia hotuba yake hiyo ambayo ilikuwa ikitangazwa moja kwa moja katika vituo vya redio na televisheni ikiwemo kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC).

Katika hotuba hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliwapongeza waumini wa dini ya Kiislamu nchini na ulimwenguni kote kwa kutimiza nguzo hiyo ya dini yao na kueleza matumaini yake kuwa mafunzo makubwa waliyoyapata katika mwezi wa Ramadhani watayatumia katika miezi mingine ijayo.

“…mambo mema yote tuliyotendeana bado yanahitajika kuelezwa na kutekelezwa wakati wote hata baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani. Tuuendeleze mwendo huu mwema huku tukizingatia kuwa sote ni wamoja na tunamtegemea Mwenyezi Mungu” alieleza Dk. Shein.

Mapema asubuhi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekitki wa Baraza la Mapinduzi alihudhuria sala ya Eid iliyofanyika kwenye viwanja vya Maisara na kuongozwa na Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Soraga.

Kabla ya kuhutubia Baraza la Eid, Dk. Shein alikutana na kusalimiana na masheikh mbalimbali huko Ikulu wakiongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabbi ambapo walitakiana kheri na fanaka ya sikukuu.

Aidha kama kawaida ya siku za Eid el Fitri , alijibu maswali ya kipindi cha watoto cha kituo cha televisheni cha ZBC na alisalimiana pia na wananchi mbalimbali waliofika Ikulu na kuwapa mkono wa Eid.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
  E-mail: saidameir@ikuluzanzibar.go.tz

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.