Habari za Punde

Jalada la Hija na wenzake tisa latua kwa DPP .Njemba aliebaka mlemavu wa akili nae ahemea Polisi

Na Mwandishi wetu, Pemba
AFISI ya Mkurugenzi wa Mashitaka Pemba, imekiri kuwa jalada  la watuhumiwa 10, akiwemo aliekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani Hija Hassan Hija, wameshalipokea kutoka Polisi na wanaendelea kulipitia mstari kwa mstari, ili wajiridhishe kabla ya kuliombea kibali ili lipelekwe mahakamani.

Afisi hiyo imesema, jalada hilo limetua afisini mwao, tokea Julai 11, mwaka huu, na baada ya kazi wanayoendelea nayo watalisafirisha hadi kwa Mkurugenzi wa Afisi hiyo Kisiwani Unguja, ili kuliombea kibali kabla ya kulipandisha mahakamani.

Mwanasheria Dhamana wa afisi hiyo kisiwani Pemba Al-baghiri Yakut Juma, alisema wao wanapokea majalada kadhaa ya kesi, huwa hawakurupuki kuyapandisha mahakamani, kwani sheria zainawaruhusu kwanza kuyapitia, ili waone kama kuna uhusiano wa kesi na kilichomo ndani ya jalada husika.

Alieleza kuwa, majalada ya tuhuma kama za uchochezi na fumanizi baada ya wao kuyapatia kwa pamoja, huyapeleka Unguja kwa mkuu wao wa kazi, ili kuyaombea kibali maalum na kisha ndio wapande nayo mahakamani.


“Kwanza ni kweli jalada lenye watuhumiwa kadhaa akiwemo Hija Hassan Haji, Seif Khamis Mohamed, Hamad Mussa Rashid, Simai Mcha Khamis, Khatib Haji Dadi, Abdalla Ali, Mussa Seif Massoud tumelipokea tokea tarehe 11 mwezi huu na tunaendelea nalo kulipitia kwa umakini’’,aliweka wazi.

Aidha mwanasheria huyo dhamana wa afisi ya Mkurugenzi wa mashitaka Pemba, aliwataka wengine waliomo kwenye jalada hilo kuwa ni Rashid Ali Hamad, Juma Abdalla Khatib, Mohamed Ame Ussi na Maulid Issa Salim ambapo alisema baada ya taratib kukamilika hatua nyengine zitafuata.

Hata hivyo alisema afisi yake wala Jeshi la Polisi, halipo kwa ajili ya kuwaonea wananchi na wamekuwa wakifanyakazi kwa kushirikiana ili haki itendeke katika kuwahudumia wananchi.

“Wananchi wasiwe na hofu wala wasisi, kwamba eti sisi na Jeshi la Polisi tutamuonea mtu hapana, tunafanyaka kazi kwa mujibu taratibu na sheria na ndio maana, jalada lipo kwetu ili kuangalia zaidi kisheria’’,alieleza.

Awali Kamanda wa Polisi mkoa wa kusini Pemba, Shehan Mohamed Shehan alisema kuwa, tayari jalada la watuhumiwa kadhaa akiwemo Hija Hassan Hija wameshalifikisha kwa DPP, kwa ajili ya kwenda mahakamani.

Nilisikia kuwa wenzetu wa DPP wanaendelea kulipitia jalada hilo, na naamini wanafanya kazi zao kwa sheria na taratibu, na wananchi wawe watulivu, sheria zinafanyakazi ili hali itendeke.

 Wakati huo huo Kamanda wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba Hassan Nassir, alisema Jeshi lake halijamshikilia wala kumuhoji aliekuwa mwakilishi wa Jimbo la Gando Said Ali Mbarouk kama taarifa zilivyozagaa mitaani.

Alisema kwa sasa mkoa wake ni shuwari na wanaendelea na doria na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana ili kulinda hali ya amani na utulivu mkoani humo.

Katika hatua nyengine, taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo, limefanikiwa kuwatia mikononi, watuhumiwa watatu wakidaiwa kuwabakaji watoto wanne akiwemo pia mlemavu mmoja wa akili.

Matukio hayo ambayo yanamuhusisha mtuhumiwa Khamis Sief Khamis (35) mkaazi wa Limbani aliwabaka watoto wawili baina ya Julai 1 na 10 mwaka huu.

Tukio la kwanza linamlomkabilia mtuhumiwa huyo lilitokea Julai 1 mwaka huu, majira ya saa 6: 30 mchana ndani ya mwezi mtukufu wa ambapo ilidaiwa alimbaka mtoto (8).

Aidha Jeshi hilo pia linamshikilia kijana huyo huyo kwa kosa kama hilo, ambalo alidaiwa kulitenda Juali 10 kwa kumbaka mtoto mwengine (6).   

Mtuhumiwa mwengine aliekamatwa na jeshi hilo kwa tuhuma kumuingilia kwa nguvu mwanamke (35) mwenye ulemavu wa akili mkaazi wa Wete, tukio lililotokea Julai 7 majira ya saa 2:00 asubuhi.

Mmwengine aliemikononi mwa Jeshi la Polisi  akikabiliwa na matukio mawili ni Nassor Issa Nassor (26) kwa tuhuma za kumbaka watoto wawili mmoja (3) na mwengine (8).


Juzi Julai 12, mahakama ya wilaya ya Chakechake, iliwapa dhamana watuhumiwa 26 wa makosa mbali mbali yakiwemo ya ukataji na ung’oaji wa mikarafuu 174, mihogo, migomba na wanatarajia kurudi tena mahakamani hapo Julai 26, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.