Habari za Punde

Waziri wa Afya Zanzibar Atembelea Kambi ya Kipindupindu Chumbuni Zanzibar.

Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo akisalimiana na Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania Dk. Rufaro Chatora alipofika kuangalia kambi ya wagonjwa wa kipindupindu iliyopo  Chumbuni Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dk. Fadhil Suleiman Mohd akitoa taarifa ya kambi ya kipindupindu ya Chumbuni kwa wawakilishi wa WHO Tanzania walipofika katika kambi hiyo.
Muonekano wa kambi ya kipindupindu ya Chumbuni iliyokuwa ikipokea wagonjwa kwa karibu mwaka mmoja sasa ikiwa haina mgonjwa hata mmoja hivi sasa.(Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.)

Na Faki Mjaka. Maelezo Zanzibar.
Shirika la Afya Duniani WHO limeipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na watu wake kwa juhudi mbalimbali walizochukua katika kukabiliana na Ugonjwa wa Kipindupindu nchini.

Aidha Shirika hilo limetaka juhudi zaidi kuendelezwa licha ya kutokuwepo kwa Mgonjwa yeyote wa Kipindupindu katika Kambi za kulaza wagonjwa wa Ugonjwa huo nchini Unguja na Pemba.

Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa WHO nchini Dkt. Rufaro Chatora alipotembelea Kambi kuu ya matubabu ya Kipindupindu huko Chumbuni Zanzibar.

Amesema hatua hiyo inatokana na kiwango kikubwa cha utashi wa kisiasa na kiungozi kilichooneshwa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kukabiana na Janga hilo.

Dkt. Rufaro ametaka juhudi ziendelee kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha jamii inaendelea kuzingatia kanuni za Afya hasa utumiaji wa maji yaliyochemshwa kwa matumizi.

Ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha wanasaidia upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na usimamizi wa kanuni za Afya ili kukabiliana na Kipindupindu.

Aidha Dkt. Rufaro Amemuhakikishia Waziri wa Afya kuwa Shirika lake litaendelea kushirikiana na Serikali katika kupambana na magonjwa mbalimbali ambayo yamekuwa yakichochewa na Mabadiliko ya Tabia nchi na ukuwaji wa Miji.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo amelishukuru Shirika la Afya na Wadau wengine kwa juhudi zao ambazo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na Ugonjwa wa Kipindupindu nchini.

Amesema licha ya hali kuimarika lakini njia pekee ya kulimaliza tatilo la kipindupindu kwa ujumla wake ni kuhakikisha mazingira ya Zanzibar yanakuwa safi muda wote.

Amesema Serikali inaendelea kuruhusu Wafanyabiashara waliotimiza masharti ya Afya kuendeleza biashara zao na kwamba Wafanyabiashara wengine wanatakiwa kufuata utaratibu huo.

Jumla ya Watu 68 Zanzibar wamepoteza maisha yao kutokana na Ugonjwa wa kipindupindu na Wagonjwa zaidi ya 4,320 walilazwa katika kambi mbalimbali za ugonjwa huo Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.