Habari za Punde

SMZ kuanza kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa kutumia Kompyuta

Na Mwashungi Tahir -Maryam Kidiko. Maelezo

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mageuzi ya vyeti vya kuzaliwa kutoka mfumo uliozoeleka wa kutumia karatasi pekee (PAPER BASED) kwenda katika mfumo wa kisasa unaotumia komputa.

Hayo   yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa  na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir  wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Habari Utalii na Michezo huko kikwajuni mjini Zanzibar.

Amesema jitihada hizi zinalenga kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma kwa haraka na utunzaji mzuri wa kumbukumbu za usajili na kufanikisha upatikanaji wa takwimu za uhakika ambazo ni muhimu katika kuiwezesha Serikali kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.

Aidha amefahamisha kuwa Serikali hiyo imeamua kuhamisha Ofisi ya Mrajis wa Vizazi , Vifo na Kadi za Utambulisho ambayo ndio yenye mamlaka kisheria kusajili matukio ya kijamii (vizazi , vifo ndoa na talaka)  katika ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa  na Idara Maalum za SMZ kwa madhumuni ya  kuunganishwa usajili wa mtoto tangu kuzaliwa mpaka kufariki kwake.

Hata hivyo ameeleza kuwa vyeti hivyo vinavyotolewa katika mfumo huo mpya vinamuonekano mzuri na ukubwa  ukilinganisha na vile vilivyozoeleka ambavyo huchapwa kwa kutumia typewriter.
Vile vile alisema  kupitia mfumo huo muombaji wa cheti cha kuzaliwa hutakiwa kuwasilisha uthibitisho wa taarifa ya kizazi kutoka Hospitalini au kwa Sheha pamoja na taarifa nyengine ili kuingizwa katika komputa na kuweza kupatikanwa cheti kwa haraka.


“Napenda kusisitiza kwamba utaratibu huu unafanyika kwa vizazi ambavyo taarifa zake zitakuwa zimeingizwa katika komputa na kwa vizazi ambavyo taarifa zake hazijaingizwa katika komputa utaratibu utakaoendelea kutumika ni uleule wa asili hadi ofisi itakapoweza kuingiza taarifa zote za vizazi katika mfumo mpya wa usajili .”Alisema waziri huyo.

Sambamba na hayo aliwataka wananchi wote wa mkoa wa Mjini Maghribi Unguja watakapojaaliwa kupata watoto kufika katka ofisi husika iliopo Mazizini wakiwa na taarifa zote zinazohitajika na kusajili vizazi vyao katika mfumo mpya ulioanzishwa .

Haji omar Kheir amesisitiza kuwa kila mtu ni haki yake kusajili vyeti hivyo kwa kufuata utaratibu maalum uliowekwa na ofisi hizo.
Jumla ya Vyeti 480 vitaanza kutolewa rasmin hivi karibuni katika Mkoa mjini Magharibi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.