Habari za Punde

Watetezi wa Haki za Binadamu, bado Pemba kuna tatizo


Na Salmin Juma -Pemba

Mataifa mbalimbali duniania yamekubali  kutia saini mitakaba ya “haki za binaadamu”kupitia umoja wa mataifa UN  ambazo kwa namna moja ama nyengineyo zitapelekea kua na maisha bora kwa kila raia wake, moja miongoni mwa mataifa hayo  ni Tanzania, kupitia mikataba hiyo imeridhia na kukubali kulinda na kuhifadhi haki za binaadamu ikiwemo ya kuishi,elimu na nyenginezo na haki hizo pia zinapatikana katika katiba yake ya 1977 na ile ya 1984 ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ).

Katika kulinda haki hizo michakatombalimbali tumekua tukishuhudia nchini mwetu  ikitekelezwa ili kuhakikisha kila raia anajua haki zake kama binaadamu,miongoni mwa hatua hizo ni utoaji wa elimu kwa wananchi unaoendelea kutolewa na taasisi mbalimbali za kiserikali na za kibinafsi.

Ingawa zipo nyingi sana lakini hapa inafaa kukipongeza kituo cha huduma za sharia Zanzibar (ZLSC) tawi la Pemba, wamekua  wakishuhudiwa kupita kila kona ya visiwa vya Pemba, shehia baada  ya shehia kutoa elimu kwa wananchi pamoja na uwendeshaji mafunzo maalum juu ya uwelewa wa haki hizo wanazotakiwa kuzipata, kanakwamba haitoshi pia kituo hicho kinashuhudiwa wakiendesha vipindi tofauti katika luninga (radio) wakizungumzia haki za kibaadamu, kuzilinda na kuzihifadhi.

Licha ya kua juhudi ya usambazaji elimu juu ya dhana hii ni kubwa  lakini bado inaonekana kuna baadhi ya raia hawajanufaika kabisa na elimu hiyo ukizingatia haki kubwa mojawapo  ni “haki ya kuishi tena katika mazingira yaliyobora” lakini bado kuna raia wa kitanzania wanakosa na wanaendelea kukosa haki hiyo, bado wanaishi katika maisha ya dhiki, dhihaka na ya kudhalilika, yaliyosababishwa na ukosefu wa elimu baina ya wanajamii wenyewe. 

Jicho la  mwandishi wa makala hii lilihuzinika na kupigwa na butwaa baada ya  kushuhudia hali mbaya ya maisha yanayomkabili  Mwadhanije Hamadi kutoka  kijiji cha Tondooni Makangale Wilaya ya Micheweni Mkoa wa kaskazini Pemba.


Mwadhanije ni kijana mdogo wa miaka 19, mpaka naandika makala hii bado hajui nini maisha bora, na hii imesababishwa na aliyekua mumewe mara tu baada ya kuingia katika ndoa. Kijana huyu aliishi katika maisha ya umasikini tangia alipozaliwa kijijini kwao hapo, familia yake haikua yenye kujipata kimaisha  kama zilivyo baadhi ya familia nyengine nchini, ingawa hali haikua hali lakini alistahamili kuishi mpaka pale wazee walipoamua kumpa mume. Aliingia katika ndoa kwa furaha na amani akiamini maisha yatakua mazuri na alizidi kupata matumaini pale  alipokua akipokea ahadi kemkem kutoka kwa mtarajiwa wa ndoa yake.

Mwezi wa 09/2015 rasmi aliolewa na bw: Ali Jabir na kuishi huko huko Tondooni Makangale Pemba, maisha yalikua mazuri ya kusikizana katika miezi mitatu ya mwanzo, kila mmoja alimuona mwenzake ndie wake katika kila jambo maishani.

Misukosuko na mikasa ilijitokea punde tu baada ya kupata ujauzito, wataalamu wa afya ya mwanaadau wanatueleza kua, mara nyingi mwanamke anapokua katika hali ya ujauzito hubadilika katika halitofauti (kama vile kumchukia mume,kuchagua vyakula,kukerwa na baadhi ya harufu n.k) hapa ndipo mambo yalipoanzia.

Nilibahatika kunzungumza na mama wa Mwadhanije Bi Mbikau Kombo Hamadi alionesha hali ya masikitiko makubwa  kutokana na misukosuko ya ndoa ya binti yake, alisema ndoa hiyo haikua na amani hata kidogo kwa sababu hata uyo mume walikua hawamtaki isipokua baba mzazi ndio alieifanya harusi hiyo.

Wakati namzungumza na mama wa kijana huyo ilikua ni mwezi wa 05/2016 ambapo tayari Mwadhanije alishaachika, ndoa yao takriban ilidumu kwa muda wa miezi 9.

Msomaji wa makala hii napenda kukwambia bayana kua hutoona mazungumzo baina yangu na Mwadhanije mwenyewe ni kwasababu ya kua ni mgonjwa wa akili (pungufu) pia hawezi kuzungumza hata kidogo (Bubu)
Bi Mbikau alizidi kueleza kua, hali ya mototo wao waliijua mapema na waliamua kumueleza (muowaji) hali halisi ilivyo  baada ya baba mzazi kutaka kumuozesha na walizidi kupata matumaini kwa sababu bw:Jabir alikua(aliyekua mumewe) ni mkaazi wa hapo hapo kijijini alimfahamu fika Mwadhanije na hali yake ilivyokua, aliahidi kuishi nae hivyohivyo na kweli alitimiza ahadi yake ingawa haikua dumu daima uzalendo ulianza kumshinda pale alipoona hali yake kubadilika baada ya ujauzito,kama maneno ya daktari yalivyofahamisha ndivyo hali ilivyokua kwa Mwadhanije Hamadi dhidi ya mumewe Jabir ilifikia hatua mpaka  unyumba alinyimwa, nguo za kazini kuchwanwa, chakula kutoekea tena kama ilivyo kawaida.

Sikutaka kuishia hapo nilijaribu kudadisi kwa undania kutaka kujua kwanini aliamua kuchukua uwamuzi wa kumuacha mkewe huyo ambae hata kuongea hawezi na akili zake zimempungua pia ukizingatia ni mjamzito, alisema amechoshwa na vitendo vyake hasa kwakua kila apelekapo malalamiko wa wazee wake haoni lolote linalotendeka kama msaada kwake.

Katika hali ya kuhuzunisha Ali Jabir anaamini Mwadhanije ndie aliemkataa wala sio yeye “hata kulala aliondoka hapa akawa analala kwa mamaake, kamba zangu za kupandia minazi amezikata zote, kila kitu changu amekiharibu hata tandiko tulilokua tunalalamia amelichanachana lakini kila nikishitaki kwa wazee wake hakuna wanalonifanyia hapo mimi ndio nikaamua kumuacha kwasababu kanikataa mwenyewe”alisema Jabir.

Hali bado ni ya kuumiza kwa wazazi wa Mwadhanije wamesema wanaumia sana kuachwa kwa mototo wao na mengi sana waliyaeleza mbele ya mwandishi, baba mzazi ambae ni bw:Hamad wa Hamad alisema hakuridhika hata kidogo na tuko hilo kwani mtoto wao haachiki kwakua ni mpungufu wa akili “akili za mtoto kama unavyoziona haachiki yule”alisema Hamad

Madai mengine wanayoyadaiwa na wanafamilia hao ni kua, kuna haki zake bado hajarudishiwa kama ikiwamo  kitanda na godoro kwakua ndivyo vilivyokua mahari yake wakati alipoolewa sambamba na kutohudumiwa huduma yoyote na alieyekua mumewe. Katika kulifatilia hili uchunguzi uligundua ni kweli hakuna chochote katika mahari yake alichorudishiwa na bwana Ali Jabir.

Wakati nazungumza na wazazi wa kijana huyu nilishuhudia hali ya afya ya Mwadhanije  ikiwa dhoofulhali baada ya kuuliza nilijibiwa kua ujauzito wa miezi mitano (5) na siku kadhaa aliyokua nao ndio unaomsumbua na kumuhilikisha namna hiyo.

Bi Zuwena Swaleh Ali ni mratibu wa  wanawake na watoto na mwanamtandao wa wanawake wilaya ya Micheweni mkoa wa kaskazini Pemba  amethibitisha kutokea mkasa huo shehiani mwake huku akisema kua  aliwahi kumtafuta  aliyekua mumewe na kumtaka kurudisha mahari ya kijana Mwadhanije lakini Jabir alikataa katakata kurudisha chochote katika mahari.

Wakati tuyanzungumza haya Mwadhanije alikua pembeni yetu hali yake si ya kuridhisha hata kidogo, amewiva kwa ujanjano ngozi yake, miguu ilimvimba pamoja na uso wake, la kusikitisha ni kua alikua peke yake lakini sasa ana mwenzake tumboni na hali kama inavyojieleza unafikiri nini kinakuja mbele yake katika mazingira kama haya.

Aidha tulipata bahati ya kuzungumza na Bi Mize wa Bimize afisa wa wanawake na watoto Wilaya ya Micheweni kutoka Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wazee Vijana Wanawake na Watoto  alifahamisha kua,kesi hiyo ipo ingawa juhudi za kunusuru ndoa hiyo zinaendelea lakini bado inaonekana kua na ugumu ndani yake ni kutokana na kutokuwepo kwa mashirikiano ya kutosha kwa wahusika wa tukio hilo.

Kupitia tukio la  kijana huyu, inabainika wazi kua  ni elimu inayotolewa inaonekana bado haijatosheleza kwa baadhi ya wananchi juu ya haki za binaadamu, ni kwamba yote yaliyombele ya kijana huyu yalisababishwa na kuvunjiaka kwa ndoa, hata ukitazama sababu zenyewe utagundua kua ni kutokua na elimu tu ya jinsi gani utaishi na mtu kama Mwadhanije, jinsi gani utanishi na mwenye ujauzito.

Kutokana na kutokua na elimu ya kutosha imepelekea mpaka muda huu Mwadhanije kukosa haki ya msingi ya kibinaadamu “haki ya kuishi katika maisha bora” hali yake ni dhaifu ya kutazamaiwa.

Kila mmoja ni shuhuda nambari moja wa matukio yaliyotanda nchini mwetu ya kuhilikishwa na kunyanya kingono wasichana wasiokua na hatia mfano mzuri wale wenye akili timamu,jee kwa Mwadhanije tunamtazama vipi katika mazingira kama haya.

Hujudi bado inahitajika kwa upande wa serikali ,wadau na watetezi wa haki za raia tulitazame hili kwa jicho la huruma,ndoa imeshatenguka ingawa kuna michakato ya kuirudisha tena kama ilivyokua lakini bado inaonekana kuna ugumu wa kufikia lengo hilo.

Kubwa zaidi hapa ninalopenda kulifikisha kwa wadau tujali afya ya Mwadhanije lakini hasa kile kiumbe kilichopo tumboni ambacho kina siku chache tu  kuja duniani maandalizi yake yanahitajika tokea leo nini kinafanyika kwa kunusura hali ya maumivu kuzidi kumuandama msichana huyu?

0772997018
No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.