Habari za Punde

CCM Z'bar yasisitiza utekelezaji wa agizo la Dk Magufuli

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewasisitiza watendaji wa  Chama na Jumuiya zake  kuharakisha zoezi la kuhorodhesha Mali za taasisi hizo ili kutekeleza kwa vitendo agizo la chama hicho.

Akizungumza na watendaji wa chama, jumuiya na watumishi wa  chama hicho wa ngazi mbali mbali , Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai huko afisi kuu ya CCM Kisiwanduzi Unguja.

Alifafanua kwamba hatua hiyo inatokana na agizo la Mwenyekiti mpya wa CCM Dkt. John Pombe Magufuli aliyetaka mali za chama hicho kuhorodheshwa haraka kwa lengo la kuimarisha chama hicho.

Alisema kwamba CCM Zanzibar ilianza utaratibu wa kukagua mali zake kabla ya Mwenyekiti huyo kutoa agizo hivyo anatarajia kwamba watendaji hao watatekeleza kazi hiyo haraka na kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima.

Alieleza kwamba licha ya Chama kupata ruzuku kutoka serikali bado kina wajibu wa kutumia rasilimali zake vizuri kuongeza vyanzo vya mapato ili kuongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya chama hicho.

Alisema hatua ya kuhorodhesha mali za chama hicho iambatane na kumaliza kasoro na mapungufu yaliyopo katika miradi ya chama na jumuiya hasa kupitia upya mikataba ya ukodishwa ili kuhakikisha inakidhi na kufuata utaratibu wa kisheria.

“ Nawakumbusha watendaji wenzangu wa CCM kwamba tujiandae vizuri kifikra kwa kuhakikisha tunafanya kazi kwa bidii kubwa na kuacha tabia za kufanya kazi kwa mazoea kwani huu ni wakati wa mabadiliko kwa kila sekta ndani ya chama chetu.

Pia mnajua kwamba chama chetu hivi karibuni kumefanyika Mkutano Mkuu Maalum na kumpata Mwenyekiti Mpya Dkt. Jonh Pombe Magufuli atakayesaidiana na Makamo Mwenyekiti wake Dkt. Shein kuhakikisha wanaendeleza kuimarisha na kukuza ustawi wa CCM, hivyo nasi ni lazima twende sambamba na kasi ya utendaji wao.”., alisema Vuai.

Vuai aliwataka watendaji hao kuzidisha ari na juhudi za kiutendaji kwa lengo la kwenda sambamba na kasi ya matakwa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Akizungumzia maagizo mbali mbali yaliyotolewa na CCM katika vikao mbali mbali vya Mkutano Mkuu huo, alisema kila mtendaji ama kiongozi wa chama hicho Zanzibar aliyeguswa na maelekezo hayo anatakiwa kuyafanyia kazi bila ya kusubiri kuwajibishwa.

Alisema miongoni mwa vipaumbele vya Mwenyekiti wa Chama hicho, Dkt. Magufuli ni kuimarisha maslahi ya watumishi wa CCM ili yaeeze kwenda sambamba na wakati uliopo kiuchumi.

Alisema Dkt. Magufuli alikiri kuwepo kwa mazingira magumu ya kiundaji ndani ya CCM na kuahidi kutatua changamoto hizo ili kuhakikisha wafuasi wa chama na wananchi kwa ujumla wananufaika na sera bora zilizowekwa na chama hicho.

Aliwasihi watendaji hao kuongeza ushirikiano na umoja katika utekelezaji wa majukumu yao na kuepuka majungu na fitna miongozi mwao na pakijitokeza kasoro za kiutendaji waziwasilishe katika vikao vinavyotambulika kikatiba ili ziweze kufanyiwa kazi.

Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo aliwapongeza wanachama, viongozi na watendaji wa chama hicho kwa kuendelea kuiunga mkono CCM kwa kila hatua licha ya kukabiliwa na changamoto za kisiasa.

Pamoja na hayo alisema ushindi wa CCM wa mwaka 2020 unatakiwa kuanza kuandaliwa hivi sasa kwa kuendeleza mazingira rafiki na yanayovutia ya kiutendaji, uwajibikaji na uwazi katika shughuli mbali mbali za chama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.