Habari za Punde

Chuo cha Uongozi wa Fedha kuwapeleka wanafunzi Taasisi za kijamii kufanya mazoezi ya vitendo (Field)

 Baadhi ya wanafunzi  wa Chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar wakifuatilia ufungaji wa mafunzo elekezi  yaliyofanyika katika Chuo chao Chwaka Mkoa Kusini Unguja.
 Mratibu wa mafunzo elekezi ya wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar Said Mohd Khamis akieleza lengo la Chuo kuanzisha mpango wa wanafunzi kufanya mazoezi ya vitendo katika taasisi za kijamii.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Mauwa Makame Rajab akifunga mafunzo elekezi ya wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar watakaoshiriki mazoezi ya vitendo katika vikundi vya kijamii (kushoto) Mkurugenzi wa Vyama vya Ushirika Zanzibar Khamis Simba na (kulia) Kaimu Mkuu wa Chuo Dkt. Iddi.

PICHA NA RAMADHANI ALI/HABARI MAELEZO ZANZIBAR

Na Ramadhani Ali/Maelezo 

CHUO cha Uongozi wa Fedha Zanzibar (ZIFA) kimeanzisha mpango wa kuwapeleka wanafunzi wa Chuo hicho  kufanya mazoezi ya vitendo katika vikundi vya   Kijamii (SACCOS) kuanzia mwaka huu.

Uamuzi huo unafuatia muongozo uliotolewa na Baraza la Chuo baada ya kubaini kuwa wanafunzi wengi wanapokuwa katika mazoezi ya vitendo  katika Mawizara, Maidara na Taasisi za  Umma wanakaa maofisini bila ya kufanya kazi yoyote na kutofaidika  na mazoezi yao.

Jumla ya wanafunzi 130 wa mwaka wa pili shahada ya kwanza wanaosoma fani ya Uhasibu, Manunuzi na Tehama wataanza mazoezi ya vitendo katika SACCOS za Unguja na Pemba baada ya kupatiwa mafunzo elekezi ya siku tatu yaliyotolewa na Idara ya Vyama vya Ushirika kwa kushirikiana na ZIFA.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, 

Mhadhiri wa Chuo cha Uongozi wa Fedha Maalim Said Mohd Khamis alisema lengo la mpango huo ni kuwawezesha wanafunzi kutoa  elimu kwa jamii baada ya masomo yao.

Amesema vyama vingi  vya ushirika vinakabiliwa na matatizo hasa katika masuala ya uhasibu, manunuzi na matumizi ya Tehama hivyo wanafunzi wao watakwenda kusaidia katika kutoa elimu kwa wanachama wa vikundi hivyo.

‘’Wanafunzi wetu watakwenda kufundisha  matumizi ya Teknolojia ya kisasa, utaratibu mzuri wa manunuzi na masuala ya uhasibu”, alisisitiza Maalim Said.

Ameongeza kuwa mtazamo  wa Chuo ni kutoa huduma na fursa zinazopatikana chuoni hapo kwa jamii ili kuisaidia Serikali katika juhudi zake za kuwapunguzia wananchi hali ngumu ya maisha.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Mauwa Makame Rajab amewaeleza wanafunzi hao kuwa baadhi ya SACCOS  wanachama wake hawana taaluma kubwa katika masuala ya ushirika hivyo mchango wao utasaidia sana katika kuviimarisha vikundi hivyo.

Amewataka vijana hao kuitumia elimu waliyonayo  na fursa waliyopata ya kufanyakazi katika  vikundi vya kijamii vijijini  kujiajiri kwa kuanzisha SACCOS ama kuongoza ziliopo katika kukabiliana na tatizo kubwa la ajira liliopo.

Amewashauri wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri katika sehemu watakazokwenda kupinga vitendo vya udhalilishaji  wa kijinsia vinavyozidi kuongozeka katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

Aidha amevishauri vyuo vyengine viliopo Zanzibar na Tanzania kwa jumla kuiga mfano ulioonyeshwa na ZIFA kuwapeleka wanafunzi wao kufanya mazoezi ya vitendo katika vikundi vya kijamii kusaidia masuala mbali mbali ikiwemo sheria, uongozi demokrasia ndani ya vikundi vyao.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Fedha Zanzibar    amesema wameupokea mpango wa Chuo kwenda kusaidia vikundi vya ushirika vijijini  kwa moyo safi na ameahidi watatoa mchango mkubwa.

Amesema wanauchukulia mpango huo kama ni majaribio kwao na watajitahidi kuweka mazingira mazuri na kuwa  mfano  wa kuigwa  na wanafunzi wenzao watakaofuata hapo baadae.        



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.