Habari za Punde

Mchezo wa kuogelea waweza kuitoa Zanzibar kimataifa ikiwa….……..


Na Haji Nassor, PEMBA--
KWA miaka kaka na dahari Zanzibar, kama zilivyo nchi nyengine, imekuwa ikijishughulisha na mchezo wa soka bila ya mafakio yanayotarajiwa na wengi.
Mipango, mikakati, kurekebisha katiba, kuajiri makocha kutoka nje na hata kuwa na timu mbili za taifa, tumekua tukifanya ili kuona walau siku moja Zanzibar, inasemwa vyema kwenye ramani ya Afrika kisoka.
Kwa serikali kuu, imefikia pahala hata kuwa na wizara maalumu inayoshughulikia michezo, ukiwemo mpira wa miguu, lakini mambo bado yamekuwa yakituwawiya vigumu kila mwaka.
Na hata kwa ligi yetu hapa visiwani, kuwa na mfadhili wa ligi kuu, naamini lengo likiwa ni kuona tunasonga mbele kwenye medani ya soka, lakini bado tunaposhuka kwenye michezo ya kimataifa, huambulia kapu la visingizio.
Kama kwenye soka, maji yamezidi unga kwanini hatuelekezi nguvu kwenye mchezo wa kuogelea, ambao naamini waweza kututoa kimataifa siku moja kama mipango ikiwekwa.
Maeneo ya kufanyia mazoezi na hata waalimu wazalendo wa mchezo huo, wamejaa pomoni kila pembe ya Zanzibar, na wapo wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu.
Sasa iweje vyombo kama BTMZ wasielekeze nguvu, mipango na sera imara kwenye mchezo wa kuogelea, ambao naamini kama tukijikita nao ndani ya miaka kumi, Zanzibar itatajwa kwenye sekta hivyo kimataifa.
Nahisi serikali na hata ZFA yenyewe, imeshapoteza nguvu na fedha nyingi kwa kushughulikia soka, na hadi sasa kufika mahala kunyoosheana vidole wenyewe, maana matunda hayapatikani.
Mbona kama nguvu hizi laiti kama zingeekezwa kwenye mchezo wa kuogelea, leo hii tungeshakirejeshea hesima kisiwa chetu mbele ya dunia na kuwapa ajira vijana wetu.
Wapo vijana kama wa kisiwa cha Kojani, Tumbatu, Nungwi, Uvinje na maeneo kadhaa ya ukanda wa bahari, wanavipaji na uhodari mkubwa wa kuogelea, sasa je hatujashituka kwamba tunabeba zigo la soka tusiloliweza?
Inaweza chombo kama BTMZ, hawajapewa ushauri kama huu, sasa ndio huu, maana kwenye soka bado kwa Zanzibar kuna giza nene ambalo kila uchao linazidi na wenzetu nchi kama Uganda, Kenya na Algeria kwao kweupe.
Tena cha kushangaaza zipo nchi ambazo tunalingana au kuzipita kwa umaskini, lakini mbona wao wako juu kisoka, kwani soka limetajwa kwenye katiba yetu kama hatukuuendekesha ndio tumevunja sheria?
Kama jawabu hapana, basi mchezo wa kuogelea ndio chaguo la wazanzibari na naamini kama sio leo basi kesho, tunaweza kukusanya rundo la tuzo za dhahabu huko ulimwenguni kwenye michuano ya kimataifa.
Kama kuna jini limeturoga, basi mmiliki wake ameshafariki, maana tumeganda kwenye mchezo ambao hutupotezea gharama kubwa pasi na matunda ya kimataifa kutoonekana, sasa tunahitaji mganga atufumbue macho kwenye mchezo wa kuogolea.
Kama hivyo ndivyo, wizara yetu sikivu ya Habari na Michezo, wakati ndio huu wa kuumarisha mchezo huo ambapo zile nguvu, maarifa, sera na mikakati kuelekezwa huko.
Lakini hata nanyi vijana wenye vipaji vya kuyachana maji, ikalieni kooni serikali kuona sasa mchezo huo unapangiwa mikakati na kuingia kwenye michuano ya kimataifa.
Lakini kama wapo wenye fedha za kutosha, makampuni ya ndani na nje, wakati ndio huu kufadhili mchezo wa kuogelea ambao naamini unaweza kukitoa kimataifa kisiwa chetu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.