Habari za Punde

Ni sahihi ‘School bus’ kujaza wanafunzi pomoni?


Na Haji Nassor, PEMBA
KATIKA miaka ya hivi karibuni, skuli mbali mbali hasa za watu binafsi, zimekuwa na utaratibu mzuri wa kuwawekea wanafunzi wao usafiri wa kudumu wa kuwapekeka na kuwarejesha skuli.
Hili ni jambo zuri sana, maana kwa njia moja ama nyengine, huwapa faraja wazazi na walezi kwamba, watoto wao wanakuwa salama zaidi wakati wanapokwenda na kurudi.
Naamini wazazi hujipunguzia fikira na dhana ya mtoto wake kwamba anayumba yumba barabarani na kupepesuliwa na gari na vyombo vyengine hasa wanapokatisha barabara.
Suala la usafiri wa uhakika kwa wanafunzi, naamini hata kwa skuli za serikali ni zuri mno, maana wanafunzi wamekuwa wakisumbuliwa na kusukumwa na makonda, wakati wakihangaika kutafuta usafiri.
Lakini je suala la gari za skuli ‘school bus’ kujaza wanafunzi wapendavyo na kisha kupita mbele ya jeshi la Polisi ambao ndio wasimamizi wa sheria hili ni sahihi?
Mbona zipo gari ambazo kisheria zilipaswa zibebe abiria 30, lakini he..hujazwa wanafunzi hadi 50 na kukaliana kaliana, kama makumbi yaliokosa mtunzaji.
Au sheria za usalama barabarani, zimetamkwa kwamba ni sahihi kwa wanafunzi wanapokwenda skuli kujazwa hadi kupindukia, kama ndio hivyo hapa hapatoshi.
Wala siamini hata kidogo kwamba, kuwajaza wanafunzi kwenye gari ambazo wazazi wao wamelipa ada na kisha wao kuumizana na kushindwa hata kuvuta pumzi, kama ndio jambo jema.
Mbona imekuwa kama sheria, kwa gari zinazobeba wanafunzi kuwajaza wanafunzi pomoni, na tena wakati mwengine hupita hata mbele ya vituo vya Polisi, bila ya kuulizwa chochote.
Au tusemeje hapa, kwamba kwa vile wanafunzi ni watoto na hawawezi kujitetea, ndio maana madereva na makondakta wamekuwa wakithubutu kuwajaza wanafunzi wapendavyo kwenye gari?
Iweje Polisi barabarani wawe wakali kwa gari za abiria, pale wanapokiuka sheria na kuzidisha abira mmoja tu, sasa je kwa hizi gari zinazobeba wanafunzi kuzidisha mara mbili ya kiwango chake na kisha kuachiwa, ndio uungwana?
Au kwa sababu tu kwenye gari zile hakuna ramba ramba kama zilivyo gari za abiria, kama ndio hivyo nadhani sio sahihi maana moja ya kazi zenu ni kuwalinda raia wote bila ya ubaguzi.
Hebu tusimamieni sheria zetu, maana sasa tumeshajitawala weyewe tokea mwaka 1964, sasa kama tunashindwa kujisimamia wenyewe, ni nani atakuwa muokozi wa watoto na ndugu zetu.
Allah ndie pekee anaeweza kuepusha ajali, sasa ikitokezea bahati mbaya ya ajali na wale mule wamejazana pomoni,roho ngapi zitateketea, kisha tusema ajali haina kinga,  mengine tuone haya.
Kama hivyo ndivyo, wakati umefika sasa kwa wazazi na walezi kuwa na sauti moja ili kuona kwamba watoto wao hawatelekezwi kwenye usafiri wanapokwenda na kurudi skuli kwa kupachikwa kama ndizi kwenye mkungu.
Lakini nanyi jeshi la Polisi, hebu kazeni buti kuona kwamba watoto wetu ambao ndio polisi na viongozi wa kesho, wanalindwa na kuenziwa kwa kuanzia kwenye usafiri wao wa skuli.
Hata nyinyi wamiliki wa gari, oneni kwamba sio sahihi kuwapachika watoto wetu 50 kwenye gari ambayo inauwezo wa kubeba abiria 25, sio sahihi maana kinachojitokeza ni maumivu na mkanyagano.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.