Na Khadija Khamis – Maelezo
Mtaalamu wa kitengo cha lishe kutoka Wizara ya Afya Zanzibar Maryam Amir amesema kunyonyesha mtoto maziwa ya mama mara tu anapozaliwa hadi kufikia miaka miwili humjenga kukuwa mwili na kiakili pamoja na kumuepushia utapiamlo na maradhi nyemelezi.
Aliyasema hayo leo katika Shehia ya Muungano wakati akitoa elimu kwa wananchi wa shehia hiyo katika siku ya kwanza ya wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa watoto wenye umri wa siku ziro hadi miaka miwili .
Alisema kinga bora kwa watoto ni maziwa ya mama katika kuwaepusha na maradhi mbali mbali iwapo wazazi watawanyonyesha watoto wao kwa mujibu inavyotakiwa .
“Kunyonyesha maziwa ya mama ni njia inayomsaidia mtoto kukua vizuri na kumuepushia mzazi kupata ujauzito katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo,”alisema mtaalamu huyo .
Alifahamisha kuwa maziwa ya kifua hupatikana muda wote na pahala popote na ni safi na salama pia yanavirutubisho vya kutosha na joto linalohitajika kwa kumjenga mtoto.
Aliongeza kuwa maziwa ya mama hupunguza vifo vya watoto kwa asilimia kubwa iwapo mtoto atanyonyeshwa maziwa pekee kwa miezi sita ya mwanzo
Wiki ya unyonyeshaji huanzia wiki ya kwanza ya mwezi wa nane kila mwaka na tarehe nane huwa ni kilele cha siku hiyo na kaulimbiu ya mwaka huu ni UNYONYESHAJI NA KAZI HAKIKISHA INAWEZEKANA .
Akizungumzia unyonyeshaji kwa akinamama wanaofanyakazi ofisini, amewashauri kukamua maziwa katika chombo safi na kuyahifadhi katika jokofu na kupewa mtoto mara kwa mara kwani yana uwezo kukaa hadi masaa manane bila kuharibika.
No comments:
Post a Comment