Habari za Punde

Waziri wa Elimu: Barua za uhamisho sasa ziwasilisheni kwangu


Na Haji Nassor, Pemba
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe: Riziki Pemba Juma, amesema kuanzia sasa barua zote za waalimu wanaotaka kuhama, kutoka kisiwa kimoja kwenda chengine, lazima ziwasilishwe mezani kwake kwa ajili ya kuzifanyia udahili wa kina.
Amesema wapo waalimu hasa wanawake, muda mfupi tu baada ya kuajiriwa kwa lengo la kukabiliana na uhaba waalimu, huomba ruhusa ya uhamisho kuwafuata waume zao kisiwani Unguja au Pemba.
Waziri huyo alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akizungumza na waalimu wa skuli za sekondari na msingi za wilaya ya Wete Pemba, kwenye ukumbi wa baraza la Wawikilishi wilaya humo.
Alisema, wapo waalimu wakuu wanapoombwa ruhusa ya uhamisho na waalimu ya kuhamia Unguja, hutoa ruhusa hizo pasi na kudahili na kisha nae Afisa Mdhamini kutoa ruhusa, hivyo sasa barua hizo ameagiza ziwasilishwe mezani kwake.
Waziri huyo alifafanua kuwa hakuna mwalimu atakaepewa ruhusa pasi na barua hiyo, kwanza kuiona yeye na ili aangalie sababu za mwalimu huyo, kutaka kuhama pale aneo aliloajiriwa awali.
“Wapo waalimu hasa wanawake wenzangu, huajiriwa kisiwani Pemba muda mfupi kisha huomba ruhusa ya kumfuata mume wake Unguja au Pemba na kuacha pengo la uhaba wa waalimu’’,alifafanua.
Waziri huyo wa Elimu na Mfunzo ya Amali Zanzibar, alisema zipo sababu kama za kufiwa na mke au mume, kuachika au kuwa na mgonjwa anaepaswa kushughuliwa, lakini sio sababu nyengine nyepesi nyepesi.
Hata hivyo ameuagiza uongozi wa wizara hiyo Pemba, kuwarejesha maeneo yao ya kazi, waalimu wote walioomba uhamisho wa muda, wa miezi sita ili kuziba pengo la uhaba wa waalimu.
Wilaya ya Wete Pemba ina jumla ya waalimu 815, wanawake 426 na wanaume 389, na madarasa 448 yanayohitaji waalimu 598, ingawa waliopo madarasani ni waalimu 521  na 77 ndio wanaohitajika ili kuziba pengo hilo.  
Katika hatua nyengine amewataka waalimu kutosubiri vikao vikubwa kama hivyo, ndio waeleze matatizo yao, bali wavitumie vikao vya skuli, wilaya kwa ajili kusaka mwarubaini wa matatizo yao.
“Jamani kama mnachangamoto kwenye utendaji wenu, hebu kaeni vikao vyenu, maana leo kusikia kwa mfano skuli haina huduma ya maji ni maajabu’’,alifafanua.
Hata hivyo amewataka waalimu hao kuendelea kujitolea na kusomesha kwa moyo safi, wakijua kuwa kazi wanayoifanya ni ya wito wala hakuna malipo watakayopewa yanayofanana na kazi yao.
Mapema Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo Pemba Salum Kitwana Sururu, amesema wizara hiyo imekuwa ikihakikisha kutatu changamoto zinazowakabili waalimu na wafanyakazia wengine kila hali ya kifedha inaporuhusu.
Alisema tayari agizo la Mhe: Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi dk: Ali Mohamed Shein la kulipa malimbilizo ya madeni, litaazna kufanyiwa kazi pale watakapoonza kuingizwa fedha shilingi milioni 300 kila mwezi.
Alisema wizara hiyo kwa Unguja na Pemba ina deni la shilingi billion 3, kama malimbikizo, na ndio maana rais wa Zanzibar akaamuru kupatiwa fedha taratibu kila mwezi, ili kupunguza deni hilo.
Baadhi ya waalimu waliopata nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo, walimuomba waziri huyo kufanya kila juhudi ili kuhakikisha anayapatia ufumbuzi malimbikizo ya madeni yao.

Ziara ya waziri huyo wa elimu inatarajiwa kuendelea tena kwa wilaya za Chakechake na Mkoani kwa ajili ya kuonana na kuzungumza na waalimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.