Habari za Punde

ZRB Yakusanya Bilioni 16 Mwezi wa Juni.2016

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Wakuu wa Taasisi za Umma za Fedha Zanzibar Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohammed 
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohammed akimueleza Balozi Mikakati inayochukuliwa na Wizara yake katika suala zima la ukusanyaji wa Mapato ya Serikali.
(Picha na –OMPR – ZNZ.)

Na.Othman Khamis OMPR. 
Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar { ZRB } Ndugu Amour Mohammed alisema kwamba makusanyo ya Mapato kwa mwezi wa Juni mwaka huu yamefikia shilingi Bilioni Kumi na Sita ikikadiriwa kufikia lengo la makusanyo ya shilingi Bilioni Ishirini mwezi Julai mwaka huu.

Hata hivyo alisema yapo baadhi ya makusanyo yanayofikia shilingi Bilioni Mbili ambayo hupatikana kutokana na mapato ya Wizara na Taasisi mbali mbali za Umma.

Kamishna Amour Mohammed alitoa takwimu hizo katika kikao cha pamoja kati ya Watendaji Wakuu wa Taasisi za Fedha wakiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d walipokutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif ameitisha Kikao hicho ikiwa ni muendelezo wa Mikutano yake ya kukutana na watendaji wapya wa Taasisi hizo kwa kutambuana kufuatia mabadiliko ya muundo mpya wa Serikali sambamba na kuangalia fursa za kukabiliana na changamoto zinazozikabili Taasisi hizo.

Kamishna huyo wa Bodi ya Mapato Zanzibar { ZRB } Ndugu Hamil Bakari alieleza kwamba mwaka 2015 Taasisi hiyo ilisimamia kukusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 83%.

Alisema kutokana na kasi ya ukusanyaji inayotekelezwa na watendaji wake yapo matarajio makubwa ya kufikia asilimia 100% ya makusanyo ya mapato ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa fedha wa 2016.

Akitoa taarifa fupi katika Kikao hicho Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d alieleza kwamba Bodi ya Mapato Zanzibar ilipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni Mia 272 kwa mwaka kati ya hizo shilingi Bilioni 35.2 zinatokana na mapato ya Wizara.

Dr. Khalid alisema Miezi ya Aprili, Mei na Juni Mwaka huu makusanyo ya mapato yalikadiriwa  kufikia shilingi Bilioni 117 ambapo mwezi juni pekee  makusanyo ya mapato yalifikia  shilingi Bilini 49 ikilinganishwa na mapato ya shilingi Bilioni 37 ya nyuma yake.

Waziri Khalid alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ukusanyaji wa mapato kwa sasa unakwenda  vizuri na kutoa fursa njema ya kupatikana kwa wakati mishahara ya wafanyakazi wa Taasisi za Umma pamoja na viinua Mgongo vya watumishi waliostaafu.

Dr. Khalid alifafanua kwamba watumishi wa umma waliostaafu kazi tokea mwaka 2015 kwa mujibu wa sheria na kanuni za Utumishi  Serikalini tayari wameshapata viinua mgongo vyao.

Alisema watumishi wastaafu wanaoendelea kusubiri haki yao kwa sasa ni wale waliostaafu katika kipindi cha miezi sita ndani ya mwaka huu wa 2016.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar { PBZ } Ndugu Juma Ameir Hafidh alisema utendaji wa Taasisi hiyo uko katika kiwango   kinachokubalika kibiashara kutokana na ushirikiano mzuri na Mabenki mengine hapa Nchini.

Hata hivyo ndugu Juma alisema zipo changamoto zinazoikabili Benki hiyo ikiwa ni pamoja na usumbufu wa kuchelewa kwa kesi zake dhidi ya Wateja wanaochukuwa Mikopo kwa ajili ya uwekezaji wa miradi tofauti nchini.

Alisema Mwekezaji asiye na mtaji mara nyingi husababisha mitihani katika kuanzisha miradi ambayo baadaye hukumbwa na ukosefu wa fedha za kurejesha deni alilokopeshwa.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Benki ya Watu wa Zanzibar aliiomba Serikali Kuu kupitia Taasisi na vitengo vinavyohusika na masuala ya uwekezaji kuhakikisha kwamba vinaratibu kwa kina viwango vya fedha za mitaji  vinavyomlazimisha Mwekezaji kuanzisha mradi utakaompa uwezo wa kuchukuwa mkopo.

Alisema utaratibu huo mbali ya kuinusuru Benki hiyo kukumbwa na hila za wawekezaji wajanja lakini pia utasaidia pande zote husika kudhibiti matatizo yanayoweza kuepukwa mapema katika suala la mikopo.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alizipongeza Taasisi hizo za Kifedha za ZRB na PBZ kwa jitihada zinazochukuwa katika uratibu wa ukusanyaji wa fedha hapa Nchini.

Balozi Seif aliuomba Uongozi na watendaji wa Taasisi hizo kutovunjika moyo katika utekelezaji wa majukumu yao na badala yake kuendelea kufanya kazi kizalengo bila ya kujali changamoto wanazopambana nazo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.