STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24.9.2016
SERIKALI ya Mapinduzi ya
Zanzibar imeokoa kiasi cha Tsh. Bilioni 9.7 kutokana na upasuaji wa maradhi ya mishipa
ya fahamu, uti wa mgongo na vichwa maji uliofanywa katika hospitali kuu ya Mnazi
Mmoja tokea kuanzishwa kwa huduma hizo miaka miwili iliyopita.
Hayo
yalielezwa leo Ikulu mjini Zanzibar katika mazungumzo yaliofanywa kati ya Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein pamoja
na Rais wa Taasisi ya Maendeleo ya Elimu inayohusiana na upasuaji wa Mishipa ya
Fahamu, Uti wa mgongo na Vichwa maji (NED) Dk. Jose Picer akiwa na Makamo wa
Rais wa Taasisi hiyo Dk. Mahmood Quiresh.
Katika
mazungumzo hayo ambapo Madaktari hao bingwa walikuwa wameongozana na uongozi wa
Wizara ya Afya chini ya Waziri wa Wizara hiyo
Mahmoud Thabit Kombo, ambao walipongeza mashirikiano makubwa
wanayoyapata katika kutekeleza shughuli zao hapa nchini.
Pamoja
na hayo, madaktari hao walieleza kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa
yaliopatikana kutoka kwa Taasisi hiyo ni pamoja na kufanya upasuaji huo kwa
wananchi wa Zanzibar wapatao 500 wakiwemo watoto, wanawake na watu wazima.
Madaktari
hao walimueleza Dk. Shein kuwa gharama hizo ni kwa ajili ya taaluma na upasuaji
mbali na gharama nyengine ambazo Serikali ingeweza kutumia katika usafirishaji,
gharama za malazi na chakula kwa wagonjwa na wauguzi wao pale wanapowasafirisha
kwenda nje ya nchi.
Kwa
upande wake Dk. Jose Picer alitoa pongezi na shukurani kwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa juhudi zinazochukuliwa
katika kutoa huduma muhimu kwa wananchi wa Zanzibar zikiwemo huduma za afya.
Dk.
Picer alieleza kuwa juhudi hizo ni za kupongezwa kwani zimeweka kuokoa maisha
ya wananchi walio wengi sambamba na kuokoa fedha nyingi za umma ambazo
zingelitumika kuwapeleka wagonjwa hao nje ya nchi.
Nae
Dk. Mahmoud Qureshi alimueleza Dk. Shein kuwa mafanikio hayo yote yaliopatikana
katika sekta hiyo ya afya yanatokana na amani na utulivu mkubwa uliopo hapa
Zanzibar kwani bila ya mambo hayo muhimu mafanikio ya upasuaji huo yasengeweza
kufanyika.
Dk.
Quresh alieleza kuwa kutokana na umuhimu mkubwa wa maendeleo ya taasisi hiyo
kuna kila sababu ya kuendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu ambao watasaidia
kufanya upasuaji huo huku akiahidi kuwa Taasisi ya NED itaendelea kuunga mkono
juhudi hizo.
Nae
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
alitoa pongezi kwa madaktari hao pamoja na taasisi hiyo kwa juhudi zao za
kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha na kuiendeleza sekta ya afya
hapa nchini .
Dk.
Shein alipongeza juhudi zilizofanywa na viongozi hao wa NED katika kuhakikisha
jengo la Taasisi ya mishipa ya fahamu, uti wa mgongo na vichwa maji linajengwa
katika hospitali ya Mnazi Mmoja na kukiri kuwa kabla ya kuwepo kwa huduma hizo
hapa nchini fedha nyingi zilikuwa zikitumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.
Aidha,
Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kuhakikisha Hospitali ya Mnazi Mmoja inarejesha hadhi yake
iliokuwepo hapo siku za nyuma kutokana na huduma mbali mbali muhimu zilizokuwa
zikitolewa pamoja na kuwa na madaktari bingwa waliobobea katika fani mbali
mbali.
Alisema
kuwa Zanzibar ina historia kubwa katika kutoa huduma za afya historia ambayo
ilikuwa kabla ya Mapinduzi na kuimarishwa zaidi baada ya Mapinduzi matukufu ya
Januari 12, 1964.
Dk.
Shein alieleza kuwa licha ya kuwepo changamoto mbali mbali zikiwemo ongezeko la
idadi ya watu hapa Zanzibar ikilinganishwa na idadi iliyopo kabda ya Mapinduzi
ya Januari 12, 1964 bado Serikali imekuwa ikichukua juhudi kubwa katika
kuimarisha sekta ya afya.
Sambamba
na hayo Dk. Shein alieleza haja ya kuimarishwa mafunzo kwa madaktari wazalendo hasa
katika kada hiyo huku akieleza kuwa nchi nyingi wahisani na mashirika yasio ya
kiserikali yamekuwa yakivutiwa kuisaidia Zanzibar kutokana na amani, utulivu na
upendo uliopo hapa nchini.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment