Habari za Punde

Kamati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Yatembelea Hospitali ya Mnazi Mmoja.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Mwinyihaji Makame akizungumza  na viongozi wa Wizaraya Afya ya Zanzibar wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya kikazi kuangalia utendaji kazi katika Wizara hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik Akili akisoma taarifa ya Wizara kwa wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi wakati wajumbe wa Kamati hiyo walipofanya ziara ya kuangali utendaji wa kazi ndani ya Wizara hiyo (kushoto) Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bi. Halima Maulid Salum.
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt. Jamala Adam Taib akizungumza na Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi walipotembelea Hospitali Kuu ya Mnazimmoja.
Mhadisi wa Vifaa Tiba vya Hospitali Dkt. Mathna Kassim Marine akiwaeleza wajumbe wa Kamati ya Ustawi wa Jamii  kuhusu vifaa  vya kisasa vitakavyo fungwa  katika  jengo jipya la mama wajawazito na watoto linalojengwa pembezoni mwa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja.
Muonekano wa Jengo jipya litakalotumika kwa ajili ya mapokezi ya wagonjwa wa kawaida (OPD) watakaofika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja kwa ajili ya kupatiwa matibabu.(Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.)

Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar.

Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi inayoshughulikia Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu imeipongeza Wizara ya Afya kwa kudhibiti maradhi ya kipindupindu baada ya kudumu kwa miezi kumi.

Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti Mwinyihaji Makame imeeleza hayo wakati ilipotembelea Hospitali Kuu ya Mnazimmoja na kufanya mazungumzo na uongozi wa Wizara  ikiwa katika shughuli zake za kazi za kawaida.

Mwenyekiti Mwinyihaji Makame amesema Wizara ilitekeleza wajibu wake kwa ufanisi mkubwa katika kupambana maradhi hayo, na hatua iliyochukuliwa na Wizara  kuanzisha utaratibu maamul wa biashara hasa za chakula ulisaidia sana kudhibiti maradhi hayo.

Hata hivyo Kamati hiyo imeishauri Wizara ya Afya kuzipa uwezo Hospitali za Wilaya ziweze kuhudumia wananchi wanaoishi huko ili azma ya kuifanya Hospitali Kuu ya Mnazimmoja kuwa ya rufaa liweze kutimia.

Wamesema baadhi ya Hospitali  walizotembelea katika maeneo mbali mbali huduma zake sio nzuri jambo ambalo linawakatisha tama wananchi wa vijijini.
Aidha wameitaka Wizara kuishauri Serikali kutoa ajira kwa  vijana waliomaliza masomo chuo cha Afya Mbweni ili kupunguza tatizo la  wafanyakazi hasa katika Idara  ya kinga.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Juma Malik Akili ameihakikishia Kamati hiyo kwamba Wizara katika robo  ya kwanza ya mwaka ipo vizuri kwa upande wa dawa baada ya kutiliwa fedha zote zilizoombwa kwa kazi hiyo.

Hata hivyo amesema tatizo linaloikabili Wizara ni njia bora za kudhibiti matumizi ya dawa hizo na ameitaka Kamati ya Ustawi wa Jamii kuisaidia Wizara kuhakikisha dawa zinawafikia  wananchi wanaofika vituoni kutafuta huduma.

Amesema Wizara inafanya juhudi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya dawa katika vituo vya Serikali lakini tatizo ni  watendaji baadhi yao hawana uaminifu mzuri.

Wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kutembelea jenge jipya la mapokezi ya wagonjwa (OPD) wanaofika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja na jengo la mama wajawazito na watoto yanayojengwa pembezoni mwa Hospitali hiyo.

1 comment:

  1. Kaka Mapara kuwa makini na typos, angalia umeandika nini kichwa cha habari,Baeaza.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.