Habari za Punde

Waliokosa Mikopo Sasa HESLB Ruksa Kukata Rufaa

Na Mwandishi Wetu
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza siku 90 kuanzia leo (Jumatatu, Oktoba 31, 2016) kwa waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2016/2017 kukata rufaa kwa njia ya mtandao ikiwa hawajaridhsihwa na matokeo ya upangaji uliotangazwa hivi karibuni.

Serikali imetenga Tshs 483 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo kwa jumla wanafunzi 119,012 – kati yao, wanafunzi 93,295 ni wanaondelea na masomo na wanafunzi 25,717 ni wa mwaka wa kwanza. Hadi sasa, jumla ya wanafunzi 20,183 wa mwaka wa kwanza wameshapata mikopo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Jumatatu, Oktoba 31, 2016) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru, Bodi imeanza kupokea rufaa hizo kwa njia ya mtandao (Online Loan Application and Management System) kuanzia leo (Oktoba 31, 2016) hadi Januari 31, 2017.

“Wanachotakiwa kufanya wanafunzi ni kulipa Tshs 10,000.00 kwa njia ya M-Pesa na kuingia katika mtandao wetu wa http://olas.heslb.go.tz na kujaza fomu, kuichapa na kuiwasilisha kwa Afisa Mikopo wa chuo chake ambaye atawasilisha kwetu fomu zote za chuo chake kwa barua kwa ajili ya sisi kuzifanyia kazi,” amesema Bw. Badru.

Bw. Badru, katika taarifa yake inayopatikana pia katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz) ameongeza kuwa Bodi haitapokea wala kuzifanyia kazi fomu za rufaa ambazo zitawasilishwa Bodi na wanafunzi bila kupitia kwa maaifsa mikopo wa vyuo vyao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.