Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Atuma Salamu za Rambirambi kwa Kifo cha Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki Kamanda wa Brigedia ya Nyuki Zanzibar.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                          15.12.2016
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambi rambi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Davis Adolf Mwamunyange kufutia kifo cha Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki, Kamanda wa Brigedia ya Nyuki Zanzibar.

Katika salamu hizo za rambi rambi, Dk. Shein alieleza kuwa amepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Brigedia Jenerali Cyril Ivor Mhaiki, Kamanda wa Brigedia ya Nyuki Zanzibar, kilichotokea jana katika Hospitali ya Jeshi la Wananachi wa Tanzania, Lugagalo, Dar-es-Salaam.

Dk. Shein kwa niaba yake binafsi pamoja na wananchi wote wa Zanzibar, alieleza kuwa wamepokea kwa mshtuko, taarifa ya kifo cha Kamanda huyo hodari aliyetoa mchango mkubwa katika shughuli za ulinzi na usalama na maendeleo ya nchi.

“Siku zote, Kamanda Mhaiki alikuwa mtu mwenye mashirikiano na wenziwe, muadilifu, msikivu na mahiri katika kazi zake”ilisema sehemu ya salamu hizo za rambi rambi.

Aidha, salamu hizo za rambirambi zilieleza kuwa hakika Marehemu Mhaiki ameacha pengo kubwa kwa familia yake, Brigedi ya Nyuki, Jeshi la Wananachi wa Tanzania pamoja na nchi nzima kwa jumla huku akisisitiza kuwa mchango wake hautosahaulika.

Dk. Shein alimuomba Jenerali Mwamunyange kuzifikisha salamu hizo za rambirambi kwa Wanafamilia, Maofisa na Wapiganaji wa vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama.

Pamoja na hayo, salamu hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa subira ndugu, jamaa na marafiki wa Marehemu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huku akimuomba Mwenyezi Mungu kumlaza mahala pema Kamanda huyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.