Habari za Punde

Shamrashamra za sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi zaanza kwa shughuli za usafi

  Baadhi ya Wananchi wakishiriki usafi wa mazingira  hapo Mtoni Kidatu pamoja na meneo mengine Nchini ikiwa ni kuanza rasmi kwa maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar  ya Mwaka 1964 kutimia Miaka 53.
  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwaongoza Viongozi pamoja  na Wananchi katika usafi wa Mazingira hapo Mtoni Kidatu ikiwa ni uzinduzi wa Sherehe za Mapinduzi kutimia Miaka 53.

Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud.
 Balozi Seif akijumuika pamoja na Wananchi katika usafishaji wa Bara bara ya Mkapa hapo Mtoni Kidatu ili ziwe katika mazingira mazuri kwa wanaozitumia wakiwemo wageni wanaotembelea Zanzibar.

Sambamba na  Balozi Seif  kulia yake ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud.
Balozi Seif akionyesha mfano wa umuhimu wa kutunza mazingira kwa kufanya usafi katika zoezi la uzinduzi wa sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 kutimia miaka 53 hapo Mtoni Kidatu.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Shamra shamra za Maadhimisho ya kusherehekea kutimia Miaka 53 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar  ya kwaka 1964  yaliyowakomboa Wakwezi na Wakulima kutokana na madhila ya Wakoloni yameanza rasmi  hapa Nchini kwa shughuli za usafi wa mazingira katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba.

Usafi huo uuliowajumuisha wananchi wa rika zote  wakiongozwa na Viongozi wao wa Wadi,  Majimbo, Wilaya pamoja na Mikoa umefanyika mapema asubuhi kwa kuweka mazingira safi katika baadhi ya sehemu zikiwemo Bara  bara Kuu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar  alijumuika pamoja na Wananchi hao katika usafi huo hapo Mtoni Kidatu  Wilaya ya Magharibi “A”.

Eneo hilo limechaguliwa maalum na Uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kufanya usafi wa mazingira kutokana na Historia yake ya kuwa chimbuko  Kuu la kuibika kwa mripuko wa maradhi ya kuharisha na kuambukiza ya Kipindu  pindu.

Akizungumza na Viongozi pamoja na Wananchi walioshiriki kwenye zoezi hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema usafi wa mazingira ni suala la msingi linalopaswa kuendelezwa  miongoni mwa Wananchi wenyewe katika mazingira yao ya kila siku.

Balozi Seif aliendelea kusisitiza kila mara  anaposhiriki kwenye masula ya usafi wa mazingira kwamba  bado utaratibu wa kufikiria kufanya usafi siku moja ya kila Mwezi una manitiki yake katika dhana nzima ya kuweka mazingira safi yanayochangia uwepo wa uhakika afya za Wananchi Mitaani.

Alisema yapo Mataifa mengi  Duniani yaliyofanikiwa kujiwekea utaratibu mzuri wa kutekeleza mpango wa usafi wa mazingira yakiwemo pia yale ya Bara la Afrika akiitolea mfano Rwanda ambayo Wananchi wanastahiki kuuiga mfano huo muhimu kwa faida ya Taifa.

Akigusia uvamizi holela wa maeneo mbali mbali ya ardhi nay ale ya wazi  hapa Nchini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema tabia hiyo mbaya inaathiri utaratibu mzuriunaowekwa  na Serikali katika  suala la Mipango Miji.

Balozi Seif alitahadharisha kwamba ujenzi holela unafanywa na baadhi ya watu kwa tamaa zisizo na msingi kwa Taifa na Wananchi wake  hazitovumiliwa na Serikali kupitia Taasisi zake kama Baraza la Manispaa pamoja na Hamlashauri za Wilaya.

Aliupongeza Uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa hatua kubwa unaoendelea kuchukuwa katika kuimarisha Mipango Miji itakayosaidia  kurejesha haiba ya Mji wa Zanzibar katika Nyanja ya Kihistoria.

Alisema juhudi hizo ni vyema zikaungwa mkono  kwa dhati na Wananchi kwa kutoa taarifa pale wanapogundua uvunjaji wa sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali pamoja nja Halmashauri zake kwenye Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Mapema  Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed  Mahmoud  alisema Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Baraza la Manispaa na Halmashauri zake zimetenga maeneo Matatu ndani ya Mkoa huo kwa ajili ya usafi wa mazingira ndani ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 53.

Mh. Ayoub aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Bara bara na Mkapa, Bara  bara ya Amani hadi Biziredi , Jang’ombe pamoja na Amani hadi Mwanakwerekwe ambayo alisema hayamo katika utaratibu wa kufanyiwa usafi wa mazingira.

Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa kugawa Mabaraza ya Mji kitendo ambacho kimeonyesha mwanzo mzuri wa kubadilika hali ya mazingira na usafi wa Halmashauri mpya zilizoundwa.

Akigusia eneo la Mtoni Kidatu liloteuliwa maalum kwa ajili ya usafi wa mazingira katika maadhimisho ya kuanza kwa sherehe za Mapinduzi  ya Zanzibar kutimia Miaka 53, Mh. Ayoub  lengo ni kuwashajiisha wananchi wa eneo hilo kupenda kufanya usafi wa mazingira kila mara.

Alisema Mtoni Kidatu na Mto Pepo  ni maeneo hatarishi ya kuwa chanzo kikuu cha  mripuko wa maradhi ya kuambukiza ya Kipindu pindu  yanayosababishwa na mazingira mabovu ya uchafu.

Maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kutimia miaka 53 yanatarajiwa kufikia kilele chake Tarehe 12 Januari 2017 katika Uwanja wa michezo wa Amani Mjini Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.