WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema Serikali inahitaji ushirikiano mkubwa na wafanyabiashara,
hivyo haitakubaliana na mtumishi yeyote wa umma atakayefanya urasimu kwa lengo
la kukwamisha uboreshaji wa sekta binafsi.
Amesema miongoni mwa
maboresho yanayofanywa na Serikali katika sekta binafsi ni pamoja na kuimarisha
utendaji wa watumishi na kuondoa urasimu katika utendajikazi wa kila siku baada
ya eneo hilo limelalamikiwa sana.
Waziri Mkuu ametoa
kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Desemba 2, 2016) wakati akizungumza na
wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda mkoani Arusha kwenye Ukumbi wa Mikutano wa
Kimataifa wa Arusha (AICC) akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi
mkoani Arusha.
Ziara hiyo inalenga
kuangalia utelelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM,Utendaji wa Serikali,
kusikiliza na kujionea kero zinazowakabili wananchi wa Mkoa huo na
kushirikiana na viongozi wa Mkoa ili kuweza kuzipatia suluhisho.
“Serikali inafanya
jitihada kubwa katika kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili
kukuza uchumi wa nchi yetu. Pia mapambano dhidi ya rushwa yanayofanyika ndani
ya Serikali na nje yanalenga kuleta maboresho makubwa katika sekta binafsi ,”
alisema.
Alisema Serikali
inawataka watendaji wake wote watumie lugha nzuri na rafiki katika kutoa huduma
kwa wafanyabiashara na wananchi kwa jumla na haitamvumilia mtumishi yeyote
atakayefanya urasimu ili mfanyabiashara atoe rushwa.
“Hatuwezi kuzungumzia
maendeleo katika sekta za maji, madini na viwanda bila ya kutaja
wafanyabiashara kwa sababu hata viwanda wao ndiyo wamiliki. Wafanyabiashara
wameondoa vijana wengi waliokuwa wanakaa vijiweni na kujadili mambo yasiyokuwa
na tija na kuwaajiri kwenye viwanda vyao,” alisema.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema Serikali itaimarisha
mipaka yake na kuzuia uingizwaji holela wa bidhaa kutoka nje ambazo
nyingi zinazalishwa hapa nchini huku lengo likiwa ni kulinda viwanda vya ndani.
“Hatuwezi kuwalinda
wazalishaji wetu wa ndani bila ya kuweka doria ya nguvu kwenye
mipaka yetu ili kudhibiti uingizwaji wa bidhaa, hususan zinazozalishwa nchini.
Lazima Serikali isaidie kulinda masoko ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda
vyetu,” alisema.
Aliongeza kuwa “Mfano
Jiji la Arusha linajenga mradi wa maji na kisha mzabuni anaagiza mabomba kutoka
nje wakati viwanda vya ndani vinatengeza kwa viwango sawa au bora zaidi ya
yanayoagizwa nje, huko si kutaka kuongeza gharama ya mradi”? Alihoji.
Alisema Serikali
haitakubali kuruhusu viwanda vya ndani vife kwa kukosa soko baada ya uingizwaji
wa bidhaa za nje. “Ni lazima mitaji ya wafanyabiashara iheshimiwe na ilindwe
ili iweze kuleta tija inayokusudiwa,”.
Waziri Mkuu alisema
Serikali na sekta binafsi zimefanya jitihada kubwa
katika kuhakikisha kunakuwa na uwekezaji kwenye sekta ya viwanda
nchini. Na sekta hiyo ndiyo inategemewa katika kulifikisha Taifa kwenye uchumi
wa kati.
Kwa upande wao
wafanyabiasha wengi walilalamikia kuwepo kwa wingi wa kodi ambapo wameiomba
Serikali kuangalia uwezekano wa kuzipunguza ili kuwaondolea usumbufu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, DESEMBA 3,
2016.
No comments:
Post a Comment