Habari za Punde

Balozi Seif aagiza kuharakizwa matengenezo ya mashine ya uchunguzi wa ndani ( Ultra Sound)

Makamu wa Pili wa Rais wa  Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimjuilia Hali aliyekuwa Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba Tanzania Bwana Makame Launi aliyelazwa Wadi ya Mapinduzi Kongwe katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja akipatiwa matibabu.
(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais  wa  Zanzibar Balozi  Seif Ali  Iddi  ameuagiza Uongozi wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kuharakisha matengenezo ya Mashine ya uchunguzi wa Maradhi ya Matumbo {Ultra sound} ili kupunguza msongamano wa Wagonjwa wanaohitaji huduma hizo.

Alisema Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ndio kimbilio pekee la Wananchi wote wa Zanzibar  wanalolitegemea  kukidhi  mahitaji  yao ya  dharura wakati  wanapokumbwa na matatizo mbali mbali ya kiafya.

Balozi Seif Ali Iddi  alitoa agizo hilo wakati alipofanya  ziara fupi ya kukagua chumba cha uchunguzi wa maradhi ya Matumbo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambapo Mashine moja kati ya Mbili zilizomo ndani ya chumba hico imeharibika kwa zaidi ya miezi miwili sasa.

Alisema mabadiliko ya kimaisha katika  mazingira ya matumizi yasiyo sahihi ya vyakula mchanganyiko wanavyotumiwa Wanaadamu yamechangia ongezeko la mardhi tofauti yakiwemo yale yanayowasumbua akina Mama ya Matumbo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Ali Salum Ali alisema juhudi za matengenezo za Mashine hiyo tayari zimeshachukuliwa  na Uongozi huo ili kuurejesha mpangilio wa huduma hizo uwe wa kawaida.

Hata hivyo Dr. Ali alisema kilichochelewesha kukamilika kwa matengenezo hayo ni mtaalamu wa kuifanyia marekebisho Mashine hiyo ambaye analazimika kutoka nje ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.