Habari za Punde

CCM Zanzibar kuwatumbua viongozi wanaokiuka maadili

 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai   mada ya Muelekeo wa Uchaguzi Mkuu wa CCM mwaka 2017/2022 katika mafunzo maalum ya siku Moja ya viongozi na watendaji wa chama hicho ngazi za matawi, wadi na majimbo ya Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja kichama.   
  Washiriki wa Mafunzo hayo ambao ni Viongozi na watendaji wa chama hicho ngazi za matawi, wadi na majimbo ya Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja kichama. 

 Washiriki wa Mafunzo hayo ambao ni Viongozi na watendaji wa chama hicho ngazi za matawi, wadi na majimbo ya Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja kichama. 
******************************************
Na Is-haka Omar , Zanzibar.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewaonya baadhi ya viongozi na wanachama wanaowashutumu na kuwadhalilisha viongozi wenzao katika vyombo vya habari na hadharani kinyume na utaratibu wa taasisi hiyo.

Onyo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati akitoa mada ya Muelekeo wa Uchaguzi Mkuu wa CCM mwaka 2017/2022 katika mafunzo maalum ya siku Moja ya viongozi na watendaji wa chama hicho ngazi za matawi, wadi na majimbo ya Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja kichama.

Alisema viongozi na wanachama wenye tabia hiyo ndani ya CCM hawawezi kuvumiliwa na watachukuliwa hatua za kinidhamu kupitia vikao vya maadili vya chama hicho endapo watathibitika kukutwa na hatia ya kuwajibika.

Alifafanua kwamba Chama hicho kikiwa ndio kinara wa Demokrasia katika mfumo wa vyama vingi Tanzania, utamaduni wa kukosoana, kuelekezana , wajibishana na kufanya maamuzi mazito kwa baadhi ya mambo yasiyokwenda sawa kimaadili na kiuongozi upo lakini kwa kufuata utaratibu wa vikao rasmi vya kikanuni ndani ya chama na sio hadharani.

“ Kuna tabia imezuka kwa baadhi ya viongozi na wanachama ndani ya CCM Zanzibar wamekuwa wababe kiasi cha kuwashutumu viongozi wenzao shutuma nzito, tena hadharani na kupitia vyombo vya Habari, wakati kuna fursa pana ya vikao vya chama ambayo ndio sehemu pekee ya kuelekezana kwa lengo la kupata ufumbuzi wa tatizo.

Tabia hiyo hatuwezi kuivumilia lazima tukate mizizi mapema kabla haijakomaa na kukiangamiza chama chetu, na wote wanaohusika na tuhuma hizo kwa sasa tunawachunguza na kuwafuatilia kwa kina ili kujiridhisha na yeyote atakayekutwa na hatia vikao vya Maadili vya chama vitachukua hatua stahiki bila ya kumuonea mtu yeyote.” Alieleza Vuai huku akiwataka wanaofanya vitendo hivyo kuacha mara moja.

 Vuai alisisitiza kauli yake na kuahidi kuwa  Chama hicho  Zanzibar hakitomvumilia kiongozi yeyote anayevunja maadili ya uongozi kwa makusudi badala yake kitamshughulikia  bila kujali cheo na umaarufu wake kisiasa.

Aliziagiza Kamati za Maadili kwa ngazi mbali mbali katika maeneo yaliyozuka migogoro hiyo kuanza mara moja kutekeleza wajibu wao wa kuwaita viongozi hao  katika vikao vya kikanuni ili kusuluhisha na ikishindikana wafuate utaratibu na kuwapeleka katika ngazi zingine za maamuzi.  

Alitoa wito kwa viongozi na watendaji wa Chama na jumuiya zake pamoja na wanachama kwa ujumla kusoma Ibara ya 18 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2012 inayoelekeza kuwa ni Mwiko kwa kiongozi  “ Kutumia madaraka aliyopewa ama kwa ajili ya manufaa yake binafsi au kwa upendeleo , au kwa namna yoyote ambayo ni kinyume cha lengo lililokusudiwa madaraka hayo”., alinukuu kifungu hicho Vuai.

Naibu Katibu Mkuu huyo akizungumzia mulekeo wa CCM aliwataka  viongozi, watendaji na wafuasi wa Chama hicho kujiandaa kikamilifu kukabiliana na mabadiliko ya muundo mpya wa Chama na Jumuiya zake.

Alisema mabadiliko hayo yanatokana na kikao Cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichokaa Disemba 13 mwaka 2016, kufikia maamuzi ya kupitisha mapendekezo ya Kamati Kuu ya kufanya mabadiliko ya muundo wa Chama hicho.

Vuai alieleza kuwa  lengo la kufanyika kwa mabadiliko ya muundo wa chama ni kuimarisha uhai wa taasisi hiyo kiutendaji na kiuongozi ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi  kulingana na wakati uliopo sasa katika ushindani wa kisiasa.

Hata hivyo aliyataja baadhi ya mapendekezo yaliyofikiwa katika Kikao hicho kuwa ni pamoja na kupunguza idadi ya wajumbe na vikao ambayo kwa sasa ni kubwa na inafanya  chama hicho kishindwe kutekeleza vizuri baadhi ya majukumu yake.

“ Wajumbe tulitafakari kwa kina muelekezo wa CCM, mienendo ya kiutendaji ya watumishi na viongozi  pamoja na mahitaji halisi ya wanachama wetu tukaona kuna haja ya kufanyika mabadiliko ili  tutabane matumizi kwa kupunguza baadhi ya gharama zisizokuwa za msingi ndani ya chama.

Ili chama chetu kiendelee kuwa mwalimu wa Demokrasia ndani na nje ya Tanzania lazima wanachama wote tuwe wamoja na wenye mshikamano katika kuunga mkono juhudi za kuleta mabadiliko yenye ufanisi  kiutendaji ndani ya chama hicho.”, alielza Vuai.

Naibu Katibu Mkuu huyo alifafanua baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na kikao hicho kuwa yaliamua kupunguza Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kutoka 388 na kupendekezwa wawe 158 kutoka Tanzania bara na Zanzibar.

Kwa upande wa ngazi ya Kamati Kuu walipendekezwa wawe wajumbe 24 badala 34 ambapo kati ya hao wajumbe watatu watachaguliwa na Halmashauri Kuu kutoka Tanzania bara na watatu wengine watachaguliwa na Halmashauri kuu ya Zanzibar.

 Alisema maandalizi ya kufanyika kwa muundo huo   ndani ya Chama yalianza  zamani kwani yalikuwa yafanyike mwaka 2012, na kuhairishwa kutokana na sababu zisizoweza kuepukika.

Alisema baada ya kuhairishwa kufanyika kwa muundo  huo  chama kiliendelea kujipanga  kwa kuwashirikisha wataalamu wa masuala ya kisiasa, kutoka Vyuo   ili watathimini   na kutoa ushauri wa kitaalamu utakaozaa muundo unaokidhi mahitaji ya wanachama.

Alibainisha kuwa Mapendekezo hayo yatapelekea kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba ya Chama na kanuzi za jumuiya na chama, na kuongeza kuwa vyeo ambavyo havitokuwemo katika Katiba hiyo havitoruhusiwa ndani ya Chama jumuiya.

Vuai aliwataka  viongozi wanaohusika na vikao vya kuchuja waombaji wa nafasi za uongozi kufuata maadili ya kikanuni kwa kuhakikisha, muombaji ametimiza masharti ya uanachama kwa mujibu wa ibara ya 8 ya Katiba ya CCM.

Alitoa angalizo kwa wanachama wa chama hicho kuhakikisha wanachagua viongozi wenye uwezo, waadilifu  na waumini wa kweli wa CCM watakaoweza kusimamia maslahi ya Chama kwa vitendo.

“ Tutumie vizuri fursa hii ya uchaguzi kwani ndio sehemu pekee ya kupata timu imara ya kuongoza jahazi la CCM kwa ufanisi na mafanikio makubwa kwa miaka mitano ijayo.

Pia ngazi husika hasa Kamati za siasa kwa ngazi mbali mbali lazima mtoe taarifa na matangazo  mapema kwa wanachama ili waweze kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi kwani ni haki ya kikatiba kwa kila mwanachama kuchagua na kuchaguliwa  ’’ Alisisitiza kiongozi huyo.

Aidha aliwataka wabunge, wawakilishi na madiwani kutengeneza mazingira rafiki ya upatikanaji kwa urahisi fursa za Mikopo na mafunzo ya Ujasiriamali kutoka katika taasisi zinazozihusika na masuala ili ziweze kuwasaidia vijana ambao hawapo katika mfumo rasmi wa ajira na waweze kujiajiri wenyewe.

Nao Washiriki wa Mafunzo hayo waliwashauri viongozi na Watumishi wa CCM na Jumuiya zake wa ngazi za Juu kuonyesha mfano wa kiutendaji ili viongozi na wanachama wa ngazi za chini waweze kufuata nyayo hizo kwa vitendo.

Walisema licha ya Mkoa huo kuwa na fursa ya Hoteli nyingi za Kitalii na rasilimali ya bahari bado kundi la  vijana wanakabiliwa na tatizo la upungufu wa ajira, jambo linalotakiwa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu na serikali kwa kushirikiana na Chama.

Mafunzo hayo ya siku moja yamewashirikisha jumla ya  viongozi na watendaji 487 wa chama na jumuiya wa ngazi za matawi, wadi na majimbo ya Wilaya ya Kaskazini “B” kichama.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.