STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba 8.1.2017

RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Mapinduzi Matukufu ya Januari 12,
1964 ndiyo yaliowapa uhuru wanyonge na kuwaondoshea maisha ya matabaka na
kuwawezesha watoto wa wanyonge kupata elimu bure ikiwa ni miongoni mwa malengo
ya Mapinduzi hao.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo mara baada ya kuifungua skuli
mpya ya Sekondari Mkanyagani, Mkoa wa Kusini Pemba aliyoipa jina la Mohammed Juma Pindua kwa
heshima kubwa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na historia yake na
mchango mkubwa wa mzee huyo katika kuifanyia
kazi kubwa Serikali, hafla hiyo ni miongoni mwa shamra shamra za sherehe za
Mapinduzi matukukufu ya Zanzibar.
Katika maelezo yake
Dk. Shein alisema kuwa ipo haja ya kuyatunza na kuyaenzi Mapinduzi ya Januari
12, 1964 kutokana na kuondosha madhila mbali mbali yaliokuwepo hasa
ikizingatiwa kuwa Zanzibar hapo mwanzo haikutawaliwa na wananchi wake walikuwa
wakijitawala wenyewe na ndipo baada ya kuja wakoloni wakaanza ukoloni sambamba
na utumwa.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa historia ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 huku akiwasisitiza
wazazi kuwafundisha historia vijana wao ili waijue nchi yao na wayajue
Mapinduzi sambamba na kujijuwa walikotoka, walipo na wanapokwenda.
Hivyo, alisema kuwa
iwapo wataijua vyema historia ya nchi yao pamoja na Mapinduzi yao ya Januari
12, 1964 hawatodanganyika wala kusikiliza kasumba za watu wachache waliokuwa
hawajitambui na wanaojitoa ufahamu na kusisitiza kuwa wale wote wanaoyabeza
mafanikio ya Mapinduzi basi watambue kuwa wanabeza maneno ya Mwenyezi Mungu.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kueleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuwaletea maendeleo wananchi
wake wote huku akieleza namna alivyochukua juhudi katika kuhakikisha eneo hilo
linapata maendeleo katika uongozi wake kabla, baada na wakati alipokuwa
Mwakilishi jimbo hilo la Mkanyageni na hadi hivi leo akiwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Alisema kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua juhudi kubwa za kupeleka maendeleo katika
eneo hilo lote ambalo kabla ya hapo huduma muhimu zilikuwa hazipo zikiwemo maji
safi na salama, miundombinu ya barabara, umeme, vituo vya afya vya uhakika na
huduma nyenginezo muhimu.
Alisema leo hii
Mkanyageni imebadilika na kila mmoja anaiona na kueleza kuwa mafanikio yote
hayo ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya CCM na kuwataka
wananchi kuwapuza na waliofilisika kisiasa na kuyabeza maendeleo hayo wakiwemo
wanaopita wakisema nchi yao imechukuliwa huku akiuliza ni nani aliyeichukua
nchi hiyo.
Dk. Shein akitoa
historia fupi ya elimu hapa nchini alisema kuwa Wakoloni waliacha skuli mbili
tu za maandalizi, skuli za msingi zilikuwa 62 tu na skuli za Sekondari zilikuwa
4 nchi nzima ambapo hivi sasa idadi ya skuli katika ngazi ya elimu ya lazima
zimefikia 843 katika mwaka 2016.
Kwa upande wa Pemba
Dk. Shein alisema kuwa hadi kufikia mwaka
1963, kulikuwa na skuli 21 ikiwa ni pamoja na skuli moja tu ya Sekondari
ya Fidel Castro ambayo kabla ya Mapinduzi ilikuwa ikiitwa Seyyid Abdallah, na
kufikia Disemba mwaka jana skuli za Serikali zimefikia 184, ambapo skuli za
Sekondari zikiwa 61 na baada ya kufunguliwa skuli hiyo mpya zitakuwa 62.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wazazi kutekeleza vyema jukumu lao la
malezi, pia, aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zinazoikabili skuli hiyo mpya
huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuiimarisha elimu ikiwa ni pamoja na
kuiongezea Bajeti Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Nae Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma alieleza juhudi zinazochukuliwa na Serikali
katika kuimarisha sekta ya elimu na kupongeza uongozi wa Dk Shein katika
kuiimarisha sekta hiyo na hatimae kupata mafanikio yanoyoonekana.
Mapema katika risala
ya ufunguzi wa jengo hilo iliyosomwa na Maalim Salim Kuza Farhan alisema kuwa
Mapinduzi yaliopelekea kutangazwa elimu bure kwa wanyonge leo yameonesha
ushahidi kwa jengo hilo ambalo mtoto wa mnyonge na wa tajiri watapata elimu kwa
usawa wao.
Alisema kuwa usanifu
wa majengo hayo ulifanywa na Kampuni ya PSM iliyoko Dar-es-Salaam ambapo ujenzi
ulianza tarehe 28.8.2012 na kufanyiwa usimajizi na washauri waelekezi kwa awamu
tatu.
Aidha, alisema kuwa
Mkandarasi wa ujenzi huo ni Kampuni ya kizalendo ya Rans ambapo ujenzi huo
unajumuisha jengo la madarasa na utawala lenye vyumba 16 vya madarasa, vyumba 2
vya maabara, chumba cha kompyuta, maktaba jengo la dakhalia lenye vyumba 38,
jengo la jiko na ukumbi wa kulia, jengo la nyumba za walimu lenye nyumba 8,
ambapo ujenzi wake umegharimu TZS Bilioni 4.
Nao Wakandarasi wa
Kampuni ya Rans walimueleza Dk. Shein umhimu wa Serikali kuzitumia kamuni za
kizalendo ambazo zina manufaa makubwa sana huku akiomba baadhi ya vipengele
vinavyowakwaza katika taratibu za tenda kuregezwa ili iwe rahisi kwao kuapata
tenda za ufundi.
Viongozi mbali mbali
wa Serikali, dini vyama vya siasa na wananchi walihudhuria katika hafla hiyo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment