Habari za Punde

Sera ya utoaji msaada wa sheria ipo njiani

Na Haji Nassor, Pemba

WIZARA ya Nchi, Afisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imesema iko mbioni kuandaa sera ya utoaji wa msaada wa kisheria, kufutia haki hiyo kutolewa kwa njia ya biashara, kama wanavyofanya baadhi ya wanasheria.

Wizara hiyo imesema haki hiyo ambayo ni ya kikatiba, lipo kundi kubwa la wananchi ambapo kwa unyonge wao wa kukosa fedha au uwelewa wa mambo ya kisheria, hukosa haki zao mbele ya vyombo vya sheria, ingawa sera hiyo ikikamilika hilo litaondoka.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo  Pemba Massoud Ali Mohamed, nje ya ukumbi wa kiwanda cha  makonyo Wawi Chakechake, wakati akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kufungua mafunzo kwa watoa huduma za kisheria.

Alisema wizara imeamua kuja na sera hiyo, kwa vile wananchi wanapaswa kupata haki zao na kujua sheria kupitia serikali yao kupitia wizara husika bila ya kujali unyonge wao.

Hivyo alisema lile kundi kubwa la wananchi wenye unyonge wa kifedha ua kutoweza kujitetea mbele ya vyombo vya sheria,  sasa sera hiyo itawawezesha kuzitambua haki na wajibu wao.

“Wizara imeona sasa kuwa, msaada wa kisheria kwa baadhi ya wanasheria wamekuwa wakiufanya kwa njia ya kibiashara, wakati ni haki yao kikatiba, hivyo sera hiyo ikija itatoa huduma sawa’’,alifafanua.

Akifungua mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo watoa huduma ya msaada wa sheria kwa wanasheria, waendesha mashitaka, mawakili, maofisa wa sheria na wasaidizi wa sheria, Afisa Mdhamini huyo alisema mafunzo hayo, ni muhimu kwani yataibua mbinu mpya ya kazi zao.

Mapema wakili wa kujitegema Pemba Zaharan Mohamed Yussuf alisema changamoto kubwa inayokabili, ni wananchi kukosa uwelewa wa kisheria na kutohifadhi kumbu kumbu zao vyema.

Nae msaidizi wa sheria kutoka wilaya Wete, Khamis Hamad Nassor, ameiomba jamii kuwaamini wakati wanawapowapa masaada wa kisheria, kwani wanalengo la kuwaelimisha haki na wajibu wao.

Mafunzo hayo ya siku tatu ambayo yamewashirikisha washiriki 50 wakiwemo mawakili, wanasheria, waendesha mashitaka, wasaidizi wa sheria na wadau wa sheria yamefadhiliwa na UNDP na kutayarisha na wizara inayohusiana na katiba na sheria.


Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC, ndio taasisi ya kwanza ya kiraia kwa Zanzibar, kuanzisha mpango wa utoaji wa huduma za kisheria bila ya malipo, ambapo pia mwaka 2007 ilianzisha mpango wa wasiaidizi wa sheria katika majimbo yote ya uchaguzi Zanzibar na kwenye Idara maalum za vikosi vya SMZ kwa lengo hilohilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.