Habari za Punde

Serikali Kununua Meli Mpya

Na.Frank Mvungi-Maelezo                                                                                                  
Serikali kununua meli mpya  ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma za usafirishaji ndani ya Ziwa  Victoria.
Akizungumza wakati wa kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi ) Dkt. Leonard Chamuriho alisema kuwa ujenzi wa meli hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa.
“Bajeti yetu ni takribani trilioni 2.5 hivyo, inatuwezesha kutekeleza mikakati yetu ya kuhakikisha kuwa sekta ya uchukuzi inachochea ujenzi wa uchumi wa Viwanda nchini”Alisisitiza  Dkt. Chamuriho.
Akizungumzia mikakati yakuendeleza sekta hiyo Dkt. Chamuriho alisema kuwa Bajeti waliyotengewa inawawezesha kuanza ujenzi wa reli kwa viwango vya Kimataifa (Standard gauge) ambayo itajengwa kwa awamu tano ambapo  awamu ya kwanza itahusisha eneo la Dar es salaam na  Morogoro.
Pia alifafanua kuwa ,upanuzi wa bandari ya Dar es salaam, Mtwara na Mwanza utachochea ukuaji wa uchumi hasa katika eneo la Bandari  ya Mtwara itochochea ukuaji wa Sekta ya gesi na Viwanda.
“Jambo Jingine ni kukarabati meli zote katika ziwa Victoria na Tanganyika ili kusaidia kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo katika maeneo mbalimbali” alisisitiza Dkt. Chamuriho.
Aidha Dkt.Chamuriho alibainisha kuwa Serikali imepanga kujenga Bandari ya Bagamoyo kwa kuwatumia wawekezaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Viwanda katika eneo la Bagamoyo na maeneo mengine kwa kuwa itatumika kusafirisha bidhaa zinazozalishwa na malighafi kutoka nje ya nchi kwa ajili ya viwanda.
Katika hatua hiyo Dkt Chamuriho alisema kuwa Mikakati mingine iliyopo ni kuimarisha shirika la ndege Tanzania (ATCL) kwa kufunga mfumo madhubuti wa kielektroniki utakaosaidia kuondoa tatizo la upotevu wa mapato hali itakayochangia kukuza shirika hilo kwa manufaa ya Taifa.
Sekta ya uchukuzi ni mhimili wa ujenzi wa Uchumi wa Viwanda hapa nchini kwa kuwaungainisha wazalishaji wa bidhaa, malighafi na wananchi katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.