Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) imepitisha ombi la Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) la
Zanzibar kuwa mwanachama kamili wa CAF. Katika kikao chake cha Kamati ya
Utendaji kilichoketi Januari 12, mwaka huu kiliamua kupitisha ombi hilo kuwa
moja ya ajenda za Mkutano Mkuu wa CAF utakaofanyika Machi 16, 2017 huko Addis
Ababa, Ethiopia.
Hivyo sasa Mkutano Mkuu huo utapiga kura na kama
Zanzibar itapata idadi ya kura theluthi mbili yaani 2/3 ya wanachama wote,
itatangazwa kuwa mwanachama mpya kamili wa CAF ambako atakuwa na haki
mbalimbali za kama mwanachama.
Haki hizo ni pamoja na kushiriki michuano yote
inayoandaliwa na kusimamiwa na CAF na hii ni pamoja na Kombe la Mataifa ya
Afrika (AFCON), fainali za Afrika Wanawake (AWCON), fainali za vijana (AFCON
U17 na AFCON 20)na pia kuhudhuria mikutano mbalimbali ya CAF kama mwanachama
kamili, kupokea na kusimamia kozi mbalimbali za CAF nakadhalika.
Pia itakuwa na fursa ya kupiga kura katika masuala
muhimu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) tofauti na sasa ambako
inapata fursa ya klabu zake zinazoshika nafasi ya juu katika Ligi Kuu ya
Zanzibar kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa
shukrani kwa Mheshimiwa Nape Nnauye – Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo wa Jamhuri ya Muungano Tanzania pamoja na Mheshimiwa Rashid Ali Juma -
Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi
Zanizbar (SMZ) kwa kufanikisha hatua hiyo.
Pia, TFF inatoa shukrani kwa Rais wa Chama cha
Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Ravia Idarus Faina pamoja na Rais wa Heshima wa
TFF Leodegar Chilla Tenga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa CAF na
Marais wa Heshima wa TFF Said Hamad El Maamry ambaye ni Mjumbe wa kudumu wa CAF
na Mzee Muhiddin Ndolanga na wadau wote wa familia ya mpira wa miguu kwa
mafanikio ya hatua hii.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa
sasa linajikita kwenye kampeni nzito ya kuomba kura za kutosha kuhakikisha
kwamba Zanzibar inapata nafasi hiyo ya uanachama kamili.
Kadhalika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) kupitia viongozi wake wako kwenye mchakato wa kumfanyia kampeni Rais wa
Heshima wa TFF, Bw. Leodegar Chilla Tenga kuhakikisha anashinda nafasi ya
Ujumbe wa Kamati ya Utendaji (Council) ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa
Miguu (FIFA).
Leodegar Tenga anawania nafasi hiyo kutoka nchi za
Afrika zinazozungumza lugha ya Kiingereza akishindana na Rais wa zamani wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Zambia, Kalusha Bwalya na Kwesi Nyantakyi wa
Ghana.
TFF inaomba Watanzania wote na wadau wote wa mpira
wa miguu nchini kutuunga mkono katika juhudi na jitihada zetu za kuona Zanzibar
inapata nafasi hiyo kadhalika Tenga anakuwa mjumbe kwenye baraza la ushauri
huko FIFA.
No comments:
Post a Comment