STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 2.2.2017
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kauli
yake ya kuwataka viongozi na watendaji katika sekta ya umma kuacha kufanya kazi
kwa mazoea huku akieleza azma ya Serikali ya kuwaongeza mshahara wafanyakazi wa
kima cha chini ifikapo Aprili mwaka huu kuwa iko pale pale.
Dk. Shein aliyasema
hayo huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani, MnaziMmoja Mjini
Zanzibar wakati akifunga Semina ya siku moja kwa Viongozi na Watendaji wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Umuhimu wa Takwimu na Matumizi yake.
Katika maelezo yake,
Dk. Shein alisisitiza haja kwa kila kiongozi kuhakikisha anasimamia vyema kazi
zake pamoja na kuwasimamia anaowaongoza katika sehemu yake ya kazi pamoja na
kufanya kazi kwa bidii na kuachana na kufanya kazi kwa mazoea.
Alisema kuwa ni jukumu
la kila kiongozi kubadilika katika utendaji wake wa kazi na kuwataka wajitahidi
kufanya hivyo licha ya kuwa itachukua muda lakini aliwasisitiza kuwa si busara
kuendelea kufanya kazi kwa mazoea.
Dk. Shein alisema kuwa
moja kati ya tamko la Ilani ya Chama cha ASP katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1963
ilikuwa ni kuwapa nafasi Waafrika wa Zanzibar kuongoza nchi yao na baada ya
Mapinduzi ya Januari 12, 1964 chini ya uongozi wa Mzee Abeid Amani Karume hilo
lilifanikiwa kwa kuanzia Wizara ya Afya na kuendelea kwa Wizara nyengine ambapo
wananchi wa Zanzibar walipata fursa ya kufanya kazi.
Kutokana na mafanikio
hayo, Dk. Shein alieleza kuwa ndani ya miaka 53 wananchi wa Zanzibar wamekuwa
wakijiongoza wenyewe, hivyo ni vyema kwa kila mmoja ajisimamie mwenyewe
sambamba na kuwasimamia walio chini yake ambapo katika suala la usimamizi
limekuwa halifanywi vizuri hivyo, kuna kila sababu ya kulitilia mkazo jambo
hilo.
“Tufanye kazi kwani
hakuna wa kutusaidia wahisani watatusaidia pale tu tutakapohitaji msaada wao
lakini suala la kufanya kazi ni letu wenyewe, hivyo tufanye kazi wala tusifanye
kazi kwa mazoea’,alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alisisitiza kuwa suala la umuhimu wa takwimu na matumizi yake ni jambo kubwa na
kuanzia sasa Serikali itaweka mkazo mkubwa zaidi kwenye takwimu kutokana na
muhimu wake katika maendeleo ya nchi.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa katika ukusanyaji wa mapato
yake kwani tokea mwaka 2010 wakati alipoingia madarakani mapato yameongezeka
kwa kiasi kikubwa takriban mara nne hivyo, hakuna kisingizio kwani Serikali iko
vizuri na cha muhimu ni kufanya kazi.
Alisisitiza kuwa
Serikali iko vizuri na tofauti na baadhi ya watu wanavyoizungumzia ambao hawana
hoja za msingi na kueleza kuwa ahadi zote za Serikali zitatekelezwa kwa
asilimia mia ikiwemo ya kuwaongezea mshahara wafanyakazi wa kima cha chini
ifikapo Aprili mwaka huu sambamba na vikosi vya SMZ navyo kulingana na vikosi
vyengine kimaslahi.
Nae Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alisisitiza haja ya kuwepo kwa
mashirikiano katika utoaji wa takwimu na kuzitaka taasisi za umma na zile
binafsi kushirikiana vyema na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali.
Balozi Seif alisema
kuwa takwimu zina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi pamoja na wananchi
wake na zimekuwa zikisaidia kwa kiasi kikubwa katika kufanya maamuzi,
kuwahudumia wananchi pamoja na kuzisaidia Wizara katika kutekeleza mipango
yake.
Waziri wa Fedha na
Mipango Dk. Khalid Salum Mohammed nae alitumia fursa hiyo kueleza kuwa Wizara
yake kupitia Ofisi ya Mtakwimu Mkuu itahakikisha kuwa Sheria ya Mtakwimu Mkuu
wa Serikali inatekelezwa vizuri na kupanga mpango madhubuti wa utekelezaji huku
akiwataka viongozi kuwa wasimamizi wa utoaji wa takwimu sahihi.
Nae Katibu Mkuu
Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Abdulhamid Yahya Mzee aliitaka Ofisi
ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kuitumia vyema Sheria yake Namba 9 ya mwaka 2007
ambayo inaipa Ofisi hiyo mamlaka ya kuratibu na kusimamia masuala yote ya
kitakwimu ambayo itatatua vyema changamoto zilizopo.
Nao Washiriki wa
Semina hiyo wakitoa michango yao mbali mbali walisisitiza haja ya kuwepo kwa
mashirikiano baina ya taasisi zao na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ili
kufikia lengo lililokusudiwa pamoja na kueleza umuhimu mkubwa wa kuwepo takwimu
sahihi kwa maendeleo ya nchi.
Sambamba na hayo,
Washiriki hao walieleza haja na umuhimu wa kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii
sambamba na kufuata na kuyafanyia kazi maagizo yote yanayotolewa na Rais wa
Zanzibar katika kutekeleza wajibu wao wa kazi.
Pia, washiriki hao walieleza
kuwa juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa na taasisi zao katika ukusanyaji
wa takwimu na kufanyika kwa Semina hiyo itazidi kuwa chachu katika utekelezaji
wa majukumu yao.
Hatimae Semina hiyo
ilikuja na maazimio ambayo yalisomwa mbele ya washiriki wote kufuatia mada tano
silizowasilishwa na wasilishaji mbali mbali kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa
Serikali zenye maudhui tofauti ikiwemo mada ya Muhtasari wa majukumu ya Ofisi
ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali katika upatikanaji wa takwimu na matumizi yake.
Mada nyengine ilikuwa
ni Umuhimu wa takwimu, hatua za uzalishaji na matumizi yake, Takwimu za sekta
ya kilimo, Takwimu za sekta ya viwanda na Takwimu za sekta ya huduma.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment