STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 03.03.2017

SINGAROPE imeahidi kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kuendeleza sekta za maendeleo hasa katika sekta ya utalii, pamoja
na vipaumbele vyengine vilivyowekwa na Serikali ili Zanzibar izidi kuimarika
kiuchumi.
Balozi wa Singapore
nchini Tanzania Tan Puay Hiang aliyasema
hayo leo wakati alipofanya mazungunmzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake, Balozi
Hiang alimueleza Dk. Shein kuwa Singapore
inathamini sana juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo hivyo kuna kila sababu ya
kuendelea kuziunga mkono hasa ikizingatiwa kuwa Zanzibar inalingana na
Singapore kimazingira.
Balozi Hiang,
alimuahidi Dk. Shein kuwa atakuwa Balozi mzuri wa kuitangaza Zanzibar katika
sekta ya utalii nchini mwake hasa kwa vile Singapore imepiga hatua kubwa katika
sekta hiyo huku akiendelea kuahidi kuwa atahakikisha mashirikiano ya karibu
katika kuimarisha sekta hiyo kwa pande mbili hizo yanaimarika.
Aidha, Balozi Hiang
alisema kuwa nchi yake pia, itazidisha uhusiano na ushirikiano katika sekta ya
usafirishaji, uwekezaji, afya na biashara pamoja na kubadilishana utaalamu hasa
katika sekta ya afya na kuahidi kusaidia vipaumbele vilivyowekwa na Zanzibar.
Aliongeza kuwa nchi
yake inaona haja na umuhimu wa kuwepo kwa mashirikiano katika kubadilishana
uzoefu na utaalamu kwa viongozi na wataalamu katika sekta ya afya na kuahidi
kuwa Singapore italisiamaia hilo ili kukuza uhusiano mwema uliopo.
Sambamba na hayo,
Balozi huyo alipongeza azma ya ujenzi wa Bandari mpya ya Mapigaduri unaofanywa
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza kuwa hatua hiyo itazidisha
ukuaji uchumi na maendeleo na kuahidi kutoa ushirikiano wake katika kufanikisha
juhudi hizo hasa katika sekta hiyo ya miundombinu.
Nae Dk. Shein kwa
upande wake alipongeza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Singapore na
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa kipindi kirefu na
kusisitiza kuwa Zanzibar itazidisha uhusiano na ushirikiano huo uliopo.
Dk. Shein alisema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itautumia uzoefu wa Singapore katika
kuimarisha sekta zake za maendeleo kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa
katika uchumi wake ambao unatajika duniani.
Aidha, Dk. Shein
alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua
juhudi za makusudi katika kuimarisha sekta zake za maendeleo hasa katika
vipaumbele vilivyowekwa kwenye Dira ya 2020 na kuwepo kwa azma ya Singapore
kuunga mkono vipaumbele hivyo kutazidisha kufikia malengo yaliowekwa.
Dk. Shein alieleza
hatua zinazochukuliwa na serikali katika ujenzi wa Bandari mpya ya Mpigaduri
pamoja na juhudi katika kuimarisha sekta ya utalii huku akisisitiza kuwa
mafunzo na ubadilishanaji wa utaalamu na uzoefu kwa wataalamu na viongozi wa
sekta ya afya ni jambo muhimu katika kuimarisha sekta hiyo.
Wakati huo huo, Dk. Shein amefanya
mazungumzo na Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioteuliwa na kuapishwa
hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe
Magufuli, mazungumzo yaliofanyika Ikulu mjini Zanzibar.
Miongoni mwa Mabalozi
hao ni Balozi Pindi Chana anaekwenda nchini Kenya, Balozi Abdalla Kilima, anayekwenda
nchini Oman, Balozi Joseph Sokoine anaekwenda Ubelgiji, Balozi Silima Kombo
Haji anaekwenda Sudan, Balozi Fatma Rajab anaekwenda Qatar, Balozi Batilda
Masuka anekwenda Jamhuri ya Korea na Balozi Grace Mgovano anekwenda nchini
Uganda.
Akizungumzo na
Mabalozi hao, Dk. Shein aliwapongeza kwa kupata uteuzi wao huo walioupata
kutokana na sifa maalum walizonazo katika utendaji wao wa kazi na kujidhatiti
kwenda kuutumikia huku akiwataka kutekeleza Diplomasia ya uchumi ambayo ndio
mbinu kubwa kwa Tanzania ambayo itaongeza ari katika kufikia azma ya kuimarisha
sekta ya viwanda.
Dk. Shein
aliwasisitiza Mabalozi hao kutilia mkazo zaidi sekta za maendeleo kwa
kuitangaza vyema Tanzania ikiwemo Zanzibar kutokana na sifa zake njema hasa
katika sekta ya uwekezaji, utalii, uvuvi, viwanda, usafiri na usafirishaji,
kilimo pamoja na mashirikiano ya vyuo vikuu
na hospitali kati ya nchi wanazokwenda kufanyakazi na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nao Mabalozi hao
walimuhakikishia Dk. Shein kuwa watakuwa mabalozi wema wa Tanzania katika nchi
wanazokwenda na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyopewa na Rais Dk.
Shein.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment