NA HAJI
NASSOR, PEMBA
WANANCHI
shehia ya kisiwa cha Makoongwe wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba, wametakiwa
wasisubiri wafadhili, juu ya suala la kukikoa, na mbadiliko makubwa ya tabia
nchi yaliokikumba kisiwa hicho, na sasa wachukue hatua za haraka wenyewe.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa
kitengo cha mabadiliko tabia nchi kisiwani Pemba, Ali Abdi Mohamed alipokuwa
akifungua mkutano wa wazi kwa wananchi, wenye lengo la kuwahamasisha upandaji
miti na uhifadhi wa mazingira, ili kupunguza kasi ya mabadiliko tabia nchi.
Alisema kisiwa cha Makoongwe, ni
miongoni mwa visiwa vidogo vidogo ambavyo navyo, zimeshaanza kukumbwa na athari
za mabadiliko tabia nchi, sasa lazima wananachi wenyewe wajipange haraka, badala
ya kusubiri wafadhili.
Abdi alieleza kuwa, kukatazana
kuchukua mchanga pembezoni mwa fukwe, kutokata miti ovyo, kuacha kuchimba
mashimo kwenye mikoko ni miongoni mwa hatua, ambazo wananchi hao wa kisiwa cha
Makoongwe wanaweza kuzichukua pasi na fedha za mfadhili.
“Kila anaekikumbuka kisiwa cha
Makoongwe miaka 25 iliopita, sasa akipata kukitembelea miaka hii, anaweza kuona
jinsi kisiwa hicho, kinavyomegwa na maji ya bahari, ndio maana tunahimizana
tuchukue hatua sasa’’,alishuari.
Kuhusu kisiwa Panza, ambao wananchi
wamepata mradi wa kupunguza kasi ya mabadiliko tabia nchi, ambao wanatarajia
kupanda miti ya aina mbali mbali 400,000 amewataka wananchi kuitunza, ili
isaidie na kisiwa chao.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya
Mazingira wilaya ya Mkoani, Rashid Abdalla Salum, alisema hali ya kisiwa cha
Makoongwe, imeanza kutisha kutokana na kila eneo kuingia maji ya bahari.
“Kila eneo sasa lina mto wa maji ya
bahari, lakini na sisi wananchi wa kisiwa hichi, tumekuwa hanasababisha kwa
kuchimba mchanga kwenye mashamba ya wakulima na hata pembezoni mwa
fukwe’’,alifafanua.
Mapema Katibu wa Jumuia ya Sanaa,
Ealimu ya Ukimwi na Mazingira JSEUMA, Juma Ali Mati, alisema kupitia mradi wa
Kupunguza kasi ya mabadiliko tabia nchi waliopata, wanakusudia kupanda miti
kwenye hekta 200.
Aidha Mati alisema wananchi 110
wameshapewa taaluma ya kupambana na kasi ya mabadiliko tabia nchi, wakiwemo wa Kisiwapanza,
Makoongwe, Michenzani, Chokochoko, Kangani, Mwambe na Mtambile.
Wananchi wa kisiwa hicho, wamepongeza
hatua ya wao kukumbushwa wajibu wao kama wananchi, katika kupambana na kasi ya
mabadiliko tabia nchi.
Ahmed Ali Siasa alisema awali
walikuwa hawajui wao kama wananchi nafasi yao katika kupambana na kasi ya
mabadiliko tabia nchi.
“Sasa baada ya elimu mliotupa na sisi
wananchi tumeshajua wajibu wetu, lazima tuhamasishane maana athari zake
humkumba kila mmoja”,alifafanua.
Jumuia ya sanaa, elimu ya ukimwi na
mazingira JSEUMA ya kisiwa panza, imeshapanda miti kwenye maeneo ya Kitunga
ndege, Maduuni ambapo wakulima 50 wamerejea tena kwenye bonde hilo, baada ya
kukihama kutokana na kuvamiwa maji ya bahari.
No comments:
Post a Comment