Habari za Punde

Kueleka maadhimisho ya siku ya Wakunga Duniani, Mama wajawazito watakiwa kuwahishwa Hospitali

 Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar Bi. Amina Abdulkadir Ali akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja kuelekea  siku ya Wauguzi Duniani Mei tano.
 Mwandishi wa habari Sebetuu Amour wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) akiuliza swali wakati wa mkutano wa Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi Zanzibar kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wakunga duniani.
 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar Valeria Rashid Haroub akitoa ufafanuzi wa masuala ya waandishi wa habari kwenye mkutano wa kuelekea maadhimisho ya siku ya wauguzi Duniani. Mkutano uliofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja.
Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar Bi. Amina Abdulkadir Ali akiwaonyesha waandishi wa habari kitabu cha mwongozo wa maadili kwa wauguzi na wakunga Zanzibar.

Picha na Makame Mshenga -Maelezo Zanzibar.

Na Ramadhani Ali/Maelezo 

Mama wajawazito wanapoonyesha dalili za kuwa tayari kujifungua wanatakiwa kuwahishwa Hospitali ama vituo vya afya mara moja bila ya kupewa dawa za aina yoyote majumbani kwani ni hatari kwa afya zao.

Mwenyekiti wa Baraza la Wakunga na Wauguzi Zanzibar Bi. Amina Abdulkadir Ali ameeleza hayo katika mkutano na  waandishi wa  Habari ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Wakunga Dunia katika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Zanzibar.

Amesema kumuwahisha mzazi katika kituo cha afya mapema kunarahisisha kupata huduma kwa haraka na iwapo anatatizo linalomkabili kujulikana mapema na kupatiwa ufumbuzi katika hatua za awali.

Bi. Amina amesema hivi sasa huduma za mama wajawazito na watoto wachanga zimeimarishwa katika vituo vingi vya afya vijijini na hakuna haja kwa mama wajawazito kulazimisha kujifungulia Hospitali kuu ya Mnazimmoja.

Amewashauri kuvitumia vituo vya afya vilivyokaribu nao na iwapo kutatokea tatizo kubwa ambalo haliwezi kushughulikiwa katika kituo kidogo litapelekwa Hospitali kuu ya Mnazimmoja.

Amesema Baraza la Wauguzi na Wakunga limeandaa mwongozo wa maadili kwa wauguzi na wakunga ambao unatakiwa kufuatwa na wafanyakazi wa kada hizo kwa lengo la kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi.

Amesisitiza umuhimu wa wanaume  kutoa upendo wa karibu kwa wake zao wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua na hivi sasa zimewekwa wodi maalum katika Hospitali ya Mnazimmoja zinazoruhusu wanaume kuwepo wodini wakati wake zao wanapojifungua.

Muuguzi Mkuu Kiongozi wa Wizara ya Afya Mussa Rashid Musaa amesema vifo vya mama wajawazito wakati wa kujifungua na watoto wachanga wakati wa kuzaliwa vimepungua kutokana na kuimarishwa kwa huduma muhimu katika wodi za wazazi.

Amesema takwimu zinaonyesha kuwa katika mwaka 2007 kila akinamama laki moja waliofika vituo vya afya kwa ajili ya kujifungua  473 walifariki ambapo mwaka jana akinamama waliofariki wakati wa kujifungua walikuwa 117.

Kwa upande wa watoto wachanga amebainisha kuwa mwaka 2008 watoto waliofariki wakati wa kuzaliwa na mara baada ya kuzaliwa walikuwa 31 kati ya watoto 1000 na mwaka jana walikuwa watoto 15 kati ya watoto 1000

Hata hivyo amekiri kuwa idadi ya vifo hivyo bado ni kubwa na Serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga vinapungua kwa kuimarisha huduma katika wodi hizo

Kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya Wakunga Duniani mwaka huu ni wakunga, akinamama na familia ni washirika wa kudumu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.