Habari za Punde

Kuelekea Timu 12 msimu wa 2017/18 ZFA ihakikishe inasimamia kanuni tu

Na Suleiman Shaaban

Mwezi uliopita 16, March Zanzibar ilikubaliwa kuwa mwanachama wa shirikisho la Mpira Afika(CAF) na kuwa mwanachama wa 55.

Safari hii haikuwa ndogo maana harakati hizi za kuitafutia uanachama Zanzibar zilianza zamani na kutiwa shemere na aliyekuwa Rais wa ZFA Bw Ali Tamim Ferej hata kupatiwa jina na alokuwa Rais wa CAF Bw Issa Hayatou na kuitwa “Mr Disturbance” katika viunga vya ofisi za CAF,Addis Ababa.

Pongezi za dhati kwa wote walioanzisha mchakato huu kwa nia njema kabisa na wale waliokhitimisha mchakato huu.Orodha ni ndefu ila itoshe kutajwa Ali Tamim Ferej kuwa kinara wa harakati hizi hadi kufikia kutoboa mfuko wake mwenyewe kufanikisha hili.Ni mzalendo wa kweli kwa hili anafaa kuenziwa walau uwanja mmoja upewe jina lake ama nishani yeyote kuenzi mchango wake huu adhimu kwa Zanzibar.
Uanachama umepatikana ila kuna chanagmoto kadhaa ambazo Zanzibar inabidi ipitie kwenye kuwezesha ustawi mzuri na kurejesha hadhi ya soka lake.

Soka ya Zanzibar ilifikia kelele mnamo miaka ya 1990 kwa timu kama Mlandege, Small Simba, Malindi, Jamhuri n.k kuvuma na kupelekea kutamba kwenye ilokuwa ligi ya Muungano.

Marehemu Riffat Said, Abdul Wakati Juma, Duwa Said na wengineo ni majina yaliyokuwa yakitamba wakati huo mitaa ya Zanzibar  na hata Tanzania kwa ujumla.
Wakati huo tulishuhudia msisimko wa soka kwenye ngazi zote Junior, Juvenile, Central na mpaka Ligi daraja la kwanza(Ligi Kuu kwa sasa).

Kwa leo tuangazie changamoto kubwa kuelekea uboreshaji wa Ligi kuu ni kubaki timu 12 kutoka timu 36 za msimu wa sasa 2016/17 katika msimu ujao wa ligi ya Zanzibar.

Kumezuka mambo kadhaa ya jinsi ya kufikia suala hilo na timu zipi kubakia kwenye Ligi kuu msimu ujao.

Ukipitia ibara ya 12(3) ya kanuni za Shirikisho la mpira CAF toleo la 2016 inaweka wazi kuwa “Kwa namna yeyote Chama cha soka (klabu) kina wajibu kuhakikisha haziingiliwi kwenye maamuzi na chombo chochote cha nje.

Pia kwa namna yeyote isiyokubalika chama cha soka kihakikishe kuwa hakuna taasisi, mtu ama kampuni kuingilia maamuzi ya klabu au chama soka pia kwa muktadha huo huo haitaruhusiwa kwa taasisi kwa kadri iwavyo ya mfumo wake wa uendeshaji/uongozi kuwa na zaidi ya timu moja kwenye mashindano ambao itapelekea upangaji wa matokeo”


Ibara hiyo inaweka bayana na hivyo kuziondoa timu za MAFUNZO, KMKM,  JKU, ZIMAMOTO na KVZ kwenye ligi ya msimu 2017/2018.

Mantiki hapa ikiwa Mfumo wa Utawala wa Klabu hizi ni mmoja.

Timu hizo zote ziko chini ya Wizara moja ila ni vitengo tofauti tu.

Waziri na Katibu Mkuu wote wanatoka wizara moja na hata upangiwaji wa mishahara na majukumu ya kazi yanatoka huko wizarani.

Kwa kutizama kipenegele cha 12(3) inasisitiza kuwa kwa mfumo wowote wa utawala Taasisi moja haipaswi kuwa na timu zaidi ya moja kwenye mashindano.

Hivyo timu zote hizo tano ziko chini ya Wizara moja kijedwali la utawala hivyo zinabanwa na sharti hili kuwemo kwenye Ligi mwakani.


Uwezekano mkubwa wa upangaji Matokeo.

Upo uwezekano mkubwa wa kupanga matokeo kwa timu hizi kuhodhi ligi kwa vile ziko chini ya utawala mmoja.

Timu tano unazungumzia mechi 8 kwa mizunguko miwili ikiwa ni pointi 24 ambazo ni sawa na 36% ya pointi zote za ligi nzima yenye jumla ya alama 66 ya michezo ya wao kwa wao.

Hiyo maana yake si rahisi kwa wao kukosa ubingwa ikiwa wana akiba ya alama 24 za kuamua ubingwa.

Na kwa mfumo wa uendeshaji ligi kwa sasa pointi 24 ni nyingi sana hivyo uwezekano wa upnagaji matokeo ni mkubwa mno.

Na hili ni kosa kubwa sana kwenye soka tunakumbuka Juventus ilishushwa daraja kwa kosa la namna hii seuze sie ambao tutakuwa na timu tano(5) zenye kukiuka kipengele hiki muhimu.

Kwa kuzingatia hayo basi kuna ushauri na faida kadha kwenye soka la Zanzibar kwa ujumla

Kurejesha msisimko wa Ligi.

Soka ni mchezo wa watu hivyo lazima uhusishwe na jamii moja kwa moja.

Timu za vikosi zimehodhi ligi si vibaya kwa wakati uliopita kwa ajili kunusuru soka letu ila kwa sasa wakati umefika kurejesha hamasa ile ilokuwa zamani timu za wanajamii wenyewe zenye wapenzi na kujaza uwanja.

Tumeshuhudia timu za Jang`ombe Boys,Taifa Jang`ombe, Shaba, Jamhuri, Malindi n.k kujaza uwanja na hamasa ya kutosha kuliko timu za vikosi.

Nani asiyejua kuwa Polisi ikicheza na Mafunzo hata pasiwe na kiingilio uwanja haupati watazamaji?

Udhamini wa Ligi na Biashara.

Soka la sasa ni biashara hivyo moja ya sababu ya msingi ili kampuni iweze kuwekeza kwenye Ligi ni mvuto wa ligi yenyewe.

Kwa sasa mechi zenye mvuto ni zinapocheza timu za mitaani kama Malindi, Jang`ombe n.k na ndizo zina mvuto kibiashara kujaza uwanja.

Ligi haiuziki kwa mriundikano wa mechi nyingi za vikosi zisizo na mvuto.Ingawa zipo sababu nyengine kwa miaka hii hili ni moja ya sababu kuu pia kukosesha udhamini.Ligi isyovutia mtu anaekaa Amaan Fresh, Magomeni, Daraja Bovu au Welezo itavutiaje kampuni kubwa kuwekeza?
Kuunda na kuwa na Timu moja bora yenye tija
Uzuri wa ligi ni mkusanyiko wa wachezaji bora kwa pamoja katika ligi.

Na ndio maana CAF wakaonelea kuwa kwa Zanzibar Ligi haipaswi kuwa na timu zaidi ya 12 kwenye Ligi kuu ili kupatikana ubora “Quality” ya ligi.

Vipaji vingi vimetawanyika kwa timu kuwa nyingi hivyo kuondoa ladha ya mpira.

Vivyo hivyo kwa timu za MAFUNZO,KMKM,JKU,ZIMAMOTO na KVZ waunde timu moja ambayo kwa hakika kabisa itakuwa bora na kikosi kirefu ambacho inayoweza kufika hatua kubwa pia hata kwenye michuano ya Klabu Bingwa na Shirikisho kuliko hivi sasa kuwa wao wameingia mara kadhaa kwenye mashindano hayo na kusihia raundi za mwanzo tu.

Hapa pia kutawatengenezea biashara kubwa kutoka nje ya nchi kwa wachezaji wao.

Mfano tokea miaka 2000 timu hizi zimekuwa zinapokezana ubingwa ila hakuna iliyovuka hata raundi ya kwanza kwenye michuano hiyo.

Ushiriki wa timu na kuvuka vizingiti vya hadi robo fainali kunaongeza msisimko na umakini wa wadau wa soka duniani kuja kuwekeza na kusaaka vipaji Zanzibar.

ZFA kazi yao ni rahisi tu ya kusimamia kanuni na hata timu na wadau wenye kupendelea ustawi wa soka ushauri wa kuondoa timu hizo ni muhimu ili kuweza kuleta tija na kuondoa uwezekano wa kuweka doa wa kuanza uvunjaji kanuni za soka mapema.

ZFA ni kuacha “unazi” wa kila namna na kuwa wakali kwenye kusimamia taratibu za soka ili kurudisha heshima ya mpira wetu Zanzibar.
Suleiman S.
17,April 2017~Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.