Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo Zanzibar Ndg Hassan Abdallah Mitawi Akitowa Mada Kuhusu Umuhimu wa Vyombo Vya Habari na Maendeleo ya Taifa. Wakati wa Semina ya Waandishi na Watendaji wa SMZ

1.0     UTANGULIZI
Vyombo vya habari vinajulikana kama mfumo wa mawasiliano unaojumuisha kwa upande mmoja utangazaji wa redio, luninga, magazeti, na Majarida.  Kwa upande mwingine vyombo vya kijamii (Social media, kama Internet, You tube, Instagram, Twiter, Website nk.).
Vyombo hivi vina umuhimu mkubwa katika mawasiliano kati ya viongozi wakiwemo viongozi wa Serikali na wadau pamoja na jamii.
Mahusiano ya vyombo vya habari, viongozi na jamii ni ya lazima hasa katika nchi inayofuata demokrasia na utawala bora kama Zanzibar.
Baadhi ya wanataaluma wanalinganisha vyombo vya habari kuwa kama hewa safi kuhamasishwa katika utekelezaji wa majukumu ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Ni wazi kwamba ni vigumu kutekeleza sera kwa ufanisi bila kuwepo matumizi mazuri ya mawasiliano kwa kupitia vyombo vya habari. Ni vigumu pia kufanikisha utumiaji wenye ufanisi bila kuwepo mahusiano bora kati ya vyombo hivyo na viongozi (wanasiasa).

Kwa kuzingatia umuhimu huo, mfumo wa habari, mbali ya kudumisha vyombo vya habari kwa hali na mali umeweka pia maafisa wa mawasiliano (Public Relation Officers) ili kudumisha mahusiano bora kati ya viongozi na vyombo vya habari.
Mada hii imegawika katika sehemu tatu kubwa, ikiwemo Majukumu ya vyombo vya habari vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mahusiano bora ya viongozi na vyombo hivyo pamoja na kujitokeza mitandao ya jamii.

2.0     Majukumu ya Vyombo vya Habari vya SMZ
Zanzibar ni nchi iliyobahatika kuwa mwanzilishi wa utumiaji wa vyombo vya habari katika Bara la Afrika hasa kusini ya Sahari.
Mwaka 1951, Zanzibar ilianzisha Redio iliyojulikana kama Redio Unguja. Mwaka 1973/4 Televisheni ya rangi ya Zanzibar ilianza kuwahudumia wananchi kwa lengo ya kutoa elimu kwa umma.

Kuanzishwa kwa vyombo hivyo kulifanikishwa kutokana na uwezo wa fedha uliofanikisha ununuaji wa teknolojia iliyohitajika wakati huo.
Kama kawaida teknolojia ya mawasiliano hubadirika mara kwa mara kama ilivyokuwa kwa teknolojia ya Redio Unguja na Televisheni Zanzibar ambayo ilitumia teknolojia ya 
Analojia kwa wakati huo.

Kutokana na mabadiliko ya tenolojia TVZ ilikabiliwa na changamoto kubwa katika ushindani na vyombo vipya vilivyoanzishwa katika nchi jirani kama Tanzania Bara, Kenya na hata Rwanda na Burundi, kwani nchi hizo zilidiriki kuanzisha vyombo vya habari kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi kuliko ile iliyotumika Visiwani.

Malengo na matumizi ya vyombo vya habari kutokana na Sera, itikadi na Siasa ya nchi husika.
Kuna miongoni mwa nchi ziinazotumia vyombo vya habari kwa malengo ya Propaganda, Agitation, Mobilization n.k
Baadhi ya nchi hudai kwamba vyombo vya habari vina majukumu ya kuelimisha, kutoa habari na kuburudisha.
Hata hivyo utekelezaji wake unafanana katika nchi karibu zote duniani.

Kuna aina kuu tatu za vyombo vya habari duniani, zikiwemo vyombo vya habari vya Serikali (State owned media), Vyombo vya jamii (Public Media) na vyombo vinavyomilikiwa na watu binafsi (Private media).

Kwa upande wa Zanzibar vyombo vya habari vya Serikali wakati huo huo vinajulikana kama vyombo vya habari vya jamii kutokana na sheria na uendeshaji wa vyombo hivyo, vikiwemo Shirika la Utangazaji Zanzibar na gazeti la Zanzibar leo, kwani vinasifa zote zinazoendana na viwango hivyo.

Sekta ya Habari ni moja ya sekta za huduma za jamii hapa nchini. Sekta hii inatoa huduma ambayo ni haki ya msingi ya raia kama inavyotamkwa kwenye Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Ibara ya 18 ya Katiba inasema:

(1) Kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa njemawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari nadhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipakaya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwakati.

(2) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusumatukio mbali mbali nchini na duniani kote ambayo nimuhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia juu yamasuala muhimu kwa jamii. Aidha, kutoa na kupokea habari kunatambuliwa duniani kote kuwani moja ya haki za binadamu.

Umoja wa Mataifa, na Umoja wa Afrika zina matamko rasmi ambayo serikali imeridhia kuhusu haki ya kupokea na kutoa habari. Haki hii, kama zilivyo haki nyinginezote, hutolewa kwa kuzingatia wajibu wa kila raia kwa jamii nauhuru binafsi wa binadamu.

Mbali na Katiba ya Nchi, ambayo ndiyo Sheria mama, vilevile ziko Sheria nyingine mbili ambazo zinasimamia shughuli za habari, ambazo ni Sheria ya Magazeti (1988) na Sheria ya Utangazaji (2002).  Sheria ya Magazeti (The Newspaper Act  No 5 1988) inampa mamlaka Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuzuia chapisho lolote linalotengenezwa hapa nchini ama kuingizwa kutoka nje ya Zanzibar ambalo linaweza kuhatarisha matakwa ya nchi. 

Sheria hii vilevile inampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya habari kuzuia kuchapishwa kwa toleo lolote la gazeti, na kwamba itakuwa ni kosa kwa mtu yeyote atakayechapisha, kuuza ama kusambaza gazeti hilo baada ya amri ya Waziri kutolewa. 

Sheria ya  Tume ya Utangazaji (The  Zanzibar Broadcasting Commission  Act No 7, 1997) ina vipengele vingi vinavyohusu shughuli za utangazaji.  Chini ya Sheria hii imeundwa Tume ya Utangazaji Zanzibar  ambayo inashughulika na utoaji leseni za kuanzisha vituo vya utangazaji pamoja na kudhibiti utendaji kazi wa vituo hivyo.

Licha ya kuwa na Sera na Sheria zilizoanzisha vyombo vya habari, usimamizi wa shughuli za Serikali unaendeshwa kisheria na Idara ya Habari/Maelezo.

Idara ya Habari Maelezo Zanzibar imeanzishwa mwaka 1996 baada ya
kutenganishwa na Sauti ya Tanzania Zanzibar kutoka Idara ya Habari Utangazaji
iliyoundwa baada ya Mapinduzi.
.Idara inamajukunu yafuatayo:-

1.     Kuwa Msemaji mkuu wa mambo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
2.     Kuweka kumbu kumbu na kutoa vibali vya kutengeneza Sinema, Video, Majarida, Vitabu vya taaluma, tamthilia na burudani.
3.     Kusimamia utekelezaji wa sera ya Habari ya Zanzibar na Sheria No. 5 ya 1988 inayohusiana na mambo ya vitabu na magazeti na utengenezaji Video na Sinema.
4.     Kutetea msimamo wa Serikali katika kupambana na Habari na tuhuma zinazotolewa na vyombo vyengine vya ndani na nje ya nchi dhidi ya Serikali.
5.     kuwa msimamizi wa kuchapisha makala mbali mabali katika magazeti, vitabu, vijarida na kadhalika.
6.     Kuishauri Serikali katika nyendo za vyombo vya Habari na kupendekeza hatua za kuchukua.
7.     Kusimamia, kutoa au kuzuia vibali vya uanziswaji magazeri na vijarida mbali mbali vya Zanzibar.
8.     Kusimamia kutoa vitambulisho kwa waandishi wa Habari na wapiga picha wa ndani na nje ya nchi ya Zanzibar waofanya shughuli hizo.
9.     Kuwaelekeza waandishi wa Habari watakaofanyakazi hapa Zanzibar maadili, maeneo na mipaka yao ya utendaji wa kazi .
10.            Ni msimamizi Mkuu (coordinator) wa msaada wa mafunzo kwa vyombo vya Habari hapa Zanzibar.

Kutokana na umuhimu wa mawasiliano kati ya viongozi na jamii, serikali imetoa muongozo na kuwataka viongozi kuwasiliana na wananchi kupitia vyombo vya habari vya Serikali kwa usimamizi wa Idara ya Habari/Maelezo.
Kwa kiasi fulani inaonekana kuwepo changamoto kubwa kwa baadhi ya viongozi kutotimiza wajibu wao kwa ushiriki katika shughuli hizo kikawaida kufuatana na ratiba iliyotolewa.

 2.0    Umuhimu wa vyombo vya habari
Vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa katika kuhamasisha ustawi wa jamii, kushajihisha uchumi, utamaduni na siasa.

Pamoja na mambo mengine, vyombo vya habari vina uwezo wa kushawishi ajenda ya maendeleo ya taifa kufuatana na kutoa kipaumbele katika maandiko na matangazo  matangazo husika. Vinaweza pia kubadili fikra na mawazo ya watu na kuwalenga kwenye uwajibikaji.

Kumejitokeza mjadala wa muda mrefu unaodai kwamba vyombo vya habari kuwa Muhimili wa  nne wa Dola, Serikali, Mahakama na chombo cha kutunga sheria.
Madai ambayo yanapingwa na wanataaluma akiwemo Prof. Shivji. Anayedai kwamba vyombo vya habari havitakiwi kuwa sehemu ya dola.  

Akielezea umuhimu wa vyombo vya habari, Rais wa awamu ya tatu Marekani, Thomas Jefferson (1787) aliwahi kusema kwamba:

“Msingi mkuu wa serikali yetu ukiwa ni maoni ya watu, ni juu yetu kuhakikisha tunasimamia jambo hili kwa uthabiti; na endapo ningeliachiwa kuamua kipi bora, kuwa na serikali bila magazeti au kuwa na magazeti bila serikali, nisingelisita hata kwa sekunde kuchagua hili la mwisho…”

Ni kwa kutambua tu umuhimu wa vyombo vya habari ndiyo maana Rais Jefferson akatamka matamshi hayo. Si yeye tu aliyewahi kuzungumzia umuhimu wa vyombo vya habari, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitambua pia umuhimu wa vyombo vya habari na ndiyo maana mbali na sera ya mwaka 1970 iliyoeleza mwelekeo wa sekta ya habari bado serikali yake iliendesha semina za mara kwa mara kwa waandishi wa habari kuhusu mchango wanaoweza kuutoa katika ujenzi wa taifa.

Kwa kifupi tu Vyombo vya habari ni mikondo inayotumika katika mawasiliano miongoni mwa jamii, na hivyo kuendelea kuwa na umuhimu wa kipekee katika jamii.
Katika miaka ya karibuni wanazuoni wengi wanaelekea kukubaliana kuhusu umuhimu wa vyombo vya habari kwa demokrasia ya vyama vingi. Gurevitch na Blumer 1993, 1995) kwa mfano, wanaeleza kwa kifupi majumuisho ya mawazo na fikra mbalimbali kuhusu majukumu na dhima ya vyombo vya habari katika jamii – hasa zile za kidemokrasia – kama ifuatavyo:

Kutoa habari na taarifa kuhusu matukio na maana yake kwa jamii;
Kutoa maoni na miongozo au ushauri kuhusiana na matukio katika jamii;
Kuwezesha kusikika kwa mawazo na maoni ya watu kutoka makundi mbalimbali ya utetezi wa kisiasa;

Kuwezesha mawasiliano kati ya watawala na watawaliwa;
Kuwa mlinzi wa kuangalia maslahi ya taifa kwa kukuhoji na kuiwajibisha serikali.
Lakini kazi ya hivi karibuni zaidi Nordenstreng na wenziwe (2009), baada ya kupitia mawazo ya wanazuoni mbalimbali na hoja mbalimbali, wameamua kuweka majukumu muhimu ya vyombo vya habari katika demokrasia kwenye mafungu makuu manne:

Uangalizi (kuangaza na kubaini matukio mbalimbali yenye umuhimu kwa jamii, ikiwamo kubainisha hatari mapema);

Ushirikiano (kutoa ushirikiano kwa taasisi, ikiwamo serikali, na makundi mengine katika kuanzisha, kuendeleza, kutetea au kudumisha jambo muhimu na lenye manufaa kwa ustawi wa taifa na jamii kwa ujumla)

Uwezeshaji (kuwezesha makundi mbambali, yakiwamo makampuni ya biashara na asasi za kiraia, kusikika kwa wateja au walengwa wao kwa haraka);

Ulinzi (kusimamia ulinzi wa maslahi ya nchi na wananchi kwa ujumla dhidi ya njama zozote za ndani au nje, za serikali au sekta binafsi)

2.1 VYOMBO VYA HABARI KATIKA MAENDELEO
Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuripoti taarifa zinazohusiana na malengo ya Serikali hususan masuala ya maendeleo  ambayo yanatekelezwa na Serikali na wadau wengine.

Ni muhimu sana kwa vyombo vya habari kujikitza zaidi katika kuripoti habari za maendeleo katika nchi na hii ni kwa sababu wajibu mkuu ni kuelimisha hivyo itakuwa ni vigumu kwa jamii kupata uelewa mpana wa ushiriki wao katika kuharakisha maendeleo ikiwa hawana uelewa.

Kwa sababu mwisho wa siku ni kwa ajili ya watu kufahamu nini kinatakiwa. Ikiwa watu hawana ufahamu nini kinatarajiwa kutoka kwao, kama hakuna ufahamu, hakuna uelewa wa masuala yaliyomo na yapi yanaweza kuwa madhara basi tutashindwa kuyafikia malengo. Na kiungo muhimu cha kuyafikisha haya kwa wananchi, watunga sera ni kupitia vyombo vya habari na vyombo vya habari vina nguvu.

Wananchi  wanahitaji taarifa sahihi na zenye kuaminika, katika wakati sahihi. Vivyo hivyo kwa wafanyabiashara, masoko na hata Serikali. Watumiaji wa leo wa taarifa duniani kote wanataka kupata tarifa wanazozihitaji katika sekunde kadhaa na wala si saa au siku kadhaa.

Kupanuka kwa njia mbalimbali za kijamii za kusambaza habari hasa kwa kupitia teknolojia ya kisasa miongoni mwa watu na hata vyombo vya habari vyenyewe, kunaashiria hamu kubwa ya umma kupata taarifa wakati wote. Jambo hili limekuwa kama sehemu muhimu ya maisha ya kila siku.

Hivyo basi, kuna umuhimu mkubwa kwa vyombo vya habari kujielekeza katika kuripoti habari za maendeleo katika nchi na hii itaharakisha ukuaji wa uchumi na kufikia katika maendeleo endelevu.

Vyombo vya habari vina nguvu kubwa kuchambua na kutengeneza mustakabali wa taifa na hasa vijana iwapo itatumika vizuri katika kuripoti habari za maendeleo badala ya kuwa chanzo cha matatizo na uchochezi mambo ambayo yanaweza kulisambaratisha taifa.

Vyombo vya habari vina wajibu wa kutafiti, kutathmini na kupeleka taarifa zenye tija na kuhamasisha wananchi  kujituma kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza malengo ya Serikali,wakitekeleza wajibu huu, tunaweza kujenga nchi yenye uelewa mpana zaidi katika masuala ya maendeleo.

Ni muhimu pia kwa vyombo vya habari pamoja na utengenezaji wa vipindi vyenye kuelimisha jamii lazima viwajibike katika ngazi mbalimbali kwa kuwapa wananchi taarifa zilizosheheni fursa zilizopo na namna ya kuzifanyia kazi, ili waondokane na umaskini.

MITANDAO YA KIJAMII
Karne ya 21 imeleta mapinduzi makubwa ya mawasiliano na upashanaji habari. Mataifa na watu ambao hapo awali walikuwa wametenganishwa na mipaka ya nchi zao, wanaunganishwa moja kwa moja kwa kupitia mtandao wa mawasiliano wa Internet. 

Aidha, ni wao ndio wanaoandika na kuueleza ulimwengu mzima kuhusu hali zao.

Kwa sasa watu wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii katika kupashana habari na kwa sababu hiyo matukio yamekuwa yakiwafikia watu kwa haraka zaidi na kwamba jamii haiwezi tena kusubirik kwa muda mrefu kabla ya raia hawajaweza kusambaza taarifa zao na kujenga mitandao mikubwa ya upashanaji habari kwa kutumia njia za kisasa na thabiti za upashanaji habari kwa kupitia mtandao (social media tools).

Mtandao wa Internet umepanua majadiliano na ubadilishanaji mawazo baina ya watu wa mataifa yote duniani. Kwa kiwango kikubwa mtandao huu wa mawasiliano ulichangia kuangushwa kwa tawala Kaskazini mwa Afrika mwaka 2011 katika kile kilichoitwa “Arabian Spring”

Mitandoo ya kijamii inanafasi kubwa sana katika jamii. Picha chini inaonyesha baadhi ya umuhimu wake.

https://3.bp.blogspot.com/-DT-xcN9WHAk/V_Ng2UV9_JI/AAAAAAAAAFY/I5lY_s8J-ooUPVrKk1MWNpY0Z3Txko4-gCLcB/s320/sociamedia-mkuumedia.png

Kama nilivyosema awali kwamba wananchi katika Ulimwengu wa Facebook, Twitter, Youtube, whasAPP, Istergram na aina nyengine ya Social Media wanataka kupata tarifa wanazozihitaji katika sekunde kadhaa na wala sio saa au siku kadhaa. Kupanuka kwa njia mbalimbali za kijamii za kusambaza habari hasa kwa kupitia teknolojia ya kisasa miongoni mwa watu na hata vyombo vya habari vyenyewe, kunaashiria hamu kubwa ya umma kupata taarifa wakati wote. Jambo hili limekuwa kama sehemu muhimu ya maisha ya kila siku.

Hapa Zanzibar wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ma ule wa marejeo wa mwaka 2016 vyama vya siasa vilitumia mitanmdao ya kijamii kwa kiwango kikubwa sana. Chama cha Mapinduzi kwa upande wake kilijidhatiti katika mitandao ya kijamii ambapo kampeni  kwa sehemu kubwa zilifanyika kupitia mitandao hiyo ambayo wapigakura wamekuwa wakitumia katika kujadili na kupashana habari kila baada ya muda. Watu wa Zanzibar, walitumia sana mitandao ya kijamii pengine kuliko wakati mwingine wowote kama sehemu ya ushiriki wao kwenye mambo yanayohusu Uchaguzi.

Mitandao ya kijamii imefanya kazi kubwa sana ambayo hakuna yeyote ambaye alitegemea. Bila kutarajiwa, kumekuwa na hamasa kubwa kutoka kwa wanasiasa na wafuatiliaji wa siasa. Ni kama vile wamegundua kuhusu ukweli kwamba mitandao ya kijamii ni kitu ambacho hakiwezi kuchukuliwa kirahisi.

Na kwa hiyo, kumekuwa na uwekezaji mkubwa, kwa mfano nchini Tanzania katika Uchaguzi wa mwaka 2015  idadi kubwa ya watu waliajiriwa ili kusimamia kampeni kupitia mitandao ya kijamii pamoja na kurasa za wagombea. Kwa hiyo, umuhimu wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania umeongezeka kwa kiasi kikubwa kabisa.

Hata hivyo, kumekuwepo na kile ninachoweza kukiita kufanya kazi bila weledi kwa kuwa watu waliopewa jukumu la kuendesha kampeni za mtandaoni hawakuwa na mikakati madhubuti katika hatua za mwanzo za kampeni. Matokeo yake, baadhi yao walianza wakiwa imara sana, na mara wakapotea, wengine walizidi kushika kasi kadiri kampeni zilivyokuwa zikiendelea, , lakini kama wangekuwa wamejipanga vizuri mapema, wafuasi wao wangalinufaika zaidi kupitia mitandao ya kijamii.

Watumiaji wa mitandao ya kijamii hapa nchini wamechipukia na idadi yao imeongezeka. Kwa mfano, idadi ya watumiaji wa Twittter waliojisajili wakati wa kipindi cha Uchaguzi Mkuu ni wengi mno. Mitandao ya Kijamii imejiweka mahali ambapo hapo awali haikuwepo-imekuwa yenye umuhimu mkubwa na inayohitajika. Watu wanatuma mitandaoni picha halisi ambazo zinapelekea baadhi ya makundi “kughushi picha” za mikusanyiko ya watu ili kuwaonesha wapiga kura kuwa wanaungwa mkono na wengi. idadi kubwa ya wakazi wa Afrika leo ni vijana.

Kwa mujibu wa takwimu za Kimataifa kuhusu idadi ya watu ,  Afrika ina idadi kubwa ya vijana ambao na asilimia 65% ya watu wake chini ya umri wa miaka 35, na zaidi ya 35% ni kati ya umri wa miaka 15 na miaka 35 ambapo hali hiyo inafanya vijana kuwa ndio kundi kubwa.Ikifika mwak 2020, inatarajiwa kwamba kati ya watu 4,  watatu watakuwa kwenye umri wa wastani wa miaka 20.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.