Habari za Punde

Rais wa Tanzania Dk. Magufuli Amewahakikishia Watanzania Atalinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                                                                  26.04.2017
---
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dk. John Pombe Mgafuli amewahakikishia wananchi wa Tanzania kuwa yeye na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein wataendelea kuulinda Muungano kwa nguvu zao zote.

Rais Magufuli aliyasema hayo leo huko katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma katika sherehe za kuadhimisha miaka 53 ya Mungano wa Tanganiyika na Zanzibar, sherehe zilizohudhuriwa na maelfu ya wananchi pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali na vyama vya siasa akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Katika hotuba yake Rais Magufuli alitoa pongezi kwa Watanzania wote kwa kutimiza miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kusisitiza kuwa leo ni siku ya kihistoria na ni ‘Birthday’ ya Tanzania nzima.

Alisema kuwa siku kama ya leo miaka 53 iliyopita waasisi wa Taifa hili Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayari Mzee Abeid Amani Karume walifanya kitendo hicho cha kihistoria ambacho kimeweza kuendelezwa na viongozi wote waliofuatia katika uongozi wao nchi hii na kusema kuwa kwa upande wao na wao watahakikisha Muungano unadumu.

Alieleza kuwa kabla ya ukoloni mashirikiano makubwa yalikuwepo baina ya watu wa Zanzibar na Tanganyika sambamba na mashirikiano na uhusiano mwema wa vyama vya siasa vilivyopigania ukombozi ambavyo ni TANU na ASP na baada ya uhuru haikuwa vigumu kuunganisha nchi mbili hizo.

Aliongeza kuwa katika miaka 53 ya Muungano mafanikio makubwa yamepatikana ya kiuchumi, kisiasa na kijamii sambamba na kuendeleza amani, uhuru na umoja hali ambayo imepelekea kulindwa vyema kwa mipaka ya Tanzania.


Alisema kuwa Serikali zote mbili ya Jamhur ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefanya juhudi kubwa kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo pamoja na kukuza demokrasia na kueleza kuwa Tanzania ya leo ni tofauti na ile ya mwaka 1964.

Rais Magufuli alieleza kuwa kutokana na mafanikio hayo, Tanzania imeweza kushiriki katika ukombozi wa nchi mbali mbali ndani ya Bara la Afrika na nje ya Bara la Afrika na kuongeza kuwa zipo nchi nyingi zinazojaribu kuungana lakini zimeshindwa.

“Kuulinda Muungano si jambo rahisi kwani hata ndoa zetu kuzilinda ni tabu kubwa… na atakaejaribu kuuvunja Muungano huu atavunjwa yeye”,alisema Rais Magufuli.

Aidha, aliwataka Watanzania kufikiria walipotoka, walipo na wanapoelekea na kuleza kuwa katika kizazi kilipo hivi sasa wengi wao wamezaliwa baada ya Muungano huo hivyo ni vyema ukaendezwa, ukatunzwa na kulindwa kwa nguvu zote.

Sambamba na hayo, alisema kuwa licha ya kuwepo mafanikio bado kuna baadhi ya changamoto ndani ya Muungano huo ambapo kwa kupitia Kamati maalum iliyoundwa kwa alengo la kutatua changamoto hizo chini ya Mweneykiti wake Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan zinafanyiwa kazi.

Katika sherehe hizo mapema Amiri Jeshi Mkuu alikagua Gwaride na baadae lilipita mblele yake pole pole na kwa mwendo wa haraka na kusonga mbele hatua 15 kwa ajili ya kutoa salamu ya Utii kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu.

Kikundi cha Makomandoo kilionyesha ukomandoo wao na kuonesha jinsi walivyokomaa kijeshi na kikamandoo na kutoa budurani kwa viongozi na wananchi jinsi ya kujilinda katika mapambano sambamba najinsi ya kupambana na adui kwa kutumia miili yao.

Onesho la Mbwa na Farasi nalo lilitia fora pamoja na Halaiki ya vijana wa Skuli za Sekondari mjini Dodoma na kufuatiwa na vikundi maalum vya ngoma za asili nazo zilitumbuiza, Kwaya ya Makongoro kutoka Mwanza na Bendi ya Muziki wa Kizazi Kipya kutoka Yamoto Bend nacho kilitumbuiza uwanjani hapo.

Ndege za kivita zilionesha umahiri wake mbele ya Amiri Jeshi Mkuu na kuwa ndio kitendo cha mwisho kilichofunga sherehe hizo zilizofana kwa kiasi kikubwa huku umma wa wananchi wakishangiria kwa nderemo na vigeregere.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.