Habari za Punde

Umuhimu wa Maonesho ya Kibiashara Kwa Kampuni Yako.

Na Jumia Travel Tanzania
Wafanyabiashara wengi wamekuwa wazito kujihusisha kwenye maonyesho ya kibiashara kutokana na kuhofia gharama kubwa za ushiriki. Wapo sahihi kwa kiasi fulani kwani ili ushiriki lazima kuna gharama zitakazohitajika kama vile; ada ya kiingilio, kuwapatia mafunzo wafanyakazi wako kuhusu unachotarajia kukifanikisha, vifaa vya kimasoko na matangazo pamoja na kuwasafirisha wafanyakazi wako endapo itahitajika.  

Lakini katika soko hili ambalo ili uaminike na kujulikana ndipo ufanye vizuri, wamiliki wa biashara hawana budi kutafakari kwa makini kushiriki kwenye maonyesho mbalimbali. Jumia Travel ingependa kukuelimisha kuwa ukizingatia yafuatayo basi biashara yako itanufaika vya kutosha: 
Weka malengo yatakayoisaidia biashara yako. Usikurupuke kushiriki kwenye maonyesho yoyote kama hujajua malengo ya kufanya hivyo. Hakikisha unaweka malengo ya kimauzo kwa wafanyakazi wako kabla ya kushiriki; hakikisha unajenga ukaribu na washiriki wote kwenye maonyesho kwani wanawezakuja kuwa wateja wako siku za usoni na mwisho kabisa hifadhi kumbukumbu ya watu unaowasiliana nao ili uje kufuatilia maendeleo yao baadae.

Jifunze kipi kinafaa na kipi hakifai. Katika kushiriki kwenye maonyesho ya namna hii sio siku zote yatakuwa na mafanikio makubwa. Hivyo basi hakikisha unachunguza ni mabanda yapi yanawavutia watu wengi zaidi na ujifunze mbinu zao; hifadhi kumbukumbu za bei na ofa wanazotoa washindani wako kisha ulinganishe na zako; jifanye kuwa ni mteja, kisha tazama watoa huduma wengine wanawasiliana kwa namna gani na wewe, na wanakuwa na malengo yapi ya kibiashara. Lazima kuna vitu utajifunza tofauti na unavyofanya wewe. 

Kuza na imarisha jina la biashara yako. Zipo mbinu nyingi katika kulifanikisha hili hususani kama biashara yako ndiyo kwanza inachipukia. Baadhi yake ni kama vile; jaribu kuweka banda lako mahali ilipo kampuni kubwa (kama utapata fursa hiyo) ili kukuza muonekano wako kwani wateja watakapotembelea hapo watavutiwa na kufanya hivyo kwako pia; tengeneza mabango yenye kuvutia na kuonekana kwa urahisi ili kuwavutia wateja wako na wale wapya; ni vema kujumuisha taarifa zako za kwenye mitandao ya kijamii ili wahudhuriaji waweze kujiunga nawe huko.

Jaribu kufanya mauzo ukiwa maonyeshoni. Ingawa linaweza kuwa sio lengo lako kuu lakini ni lazima kufanya hivyo kwani pia inaweza kukusaidia kurejesha fedha ulizozitumia. Kama inawezekana, jaribu kufanya mauzo unapokuwa maonyeshoni wakati wahudhuriaji wakiwa na shauku ya kununua bidhaa; nenda na bidhaa zako ili kufanya mauzo papo hapo, pindi wahudhuriaji wanapoonyesha kuvutiwa na bidhaa na huduma zako; endapo utashindwa kufanya mauzo kwenye maonyesho, chukua mawasiliano ya wahudhuria na kisha panga kuwasiliana nao siku za usoni. 

Hakikisha unachagua maonyesho sahihi kwa biashara yako. Kabla ya kukata shauri la kushiriki kwenye onyesho lolote hakikisha kwamba ni sahihi kwa kampuni yako. Kushiriki kwenye onyesho ambalo hautotimiza malengo yako ni sawa na kupoteza muda na rasilimali zako ambazo ungeweza kuzielekeza sehemu nyingine. Je, malengo yako ni kuuza bidhaa au kutoa huduma? Au kujenga na kuimarisha mahusiano yako ya kibiashara na wadau wengine kwenye tasnia moja? Haya yote ni muhimu kuyatambua kabla ya kukata shauri na kushiriki. 

Lakini hayo yote yatategemeana na kuchagua maonyesho sahihi/yanayofaa kwa ajili ya kampuni/biashara yako. Jumia Travel inakushauri kuwa unaweza kufanya hivyo kwa kuwauliza wenzako au washindani wako. Kushiriki maonyesho yasiyo sahihi kunaweza kukugharimu vitu vingi zaidi ya gharama za ushiriki.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.