Habari za Punde

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA AZINDUA MWONGOZO KWA WAPELELEZI NA WAENDESHA MASHITAKA WA KESI ZA WANYAMAPORI NA MISITU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa Uzinduzi wa Mwongozo kwa Wapelelezi na Waendesha Mashitaka wa Kesi za Wanyamapori na Misitu kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Prof. Jumanne Maghembe akihutubia wakati wa uzinduzi wa mwongozo kwa wapelelezi na waendesha mashitaka wa kesi za wanyamapori na misitu.
 Naibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozo kwa wapelelezi na waendesha mashitaka wa kesi za wanyamapori na misitu uliofanyika jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.
 Muendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga akizungumzia namna Mwongozo kwa Wapelelezi na Waendesha Mashitaka wa Kesi za Wanyapori utakavyoleta matokeo chanya.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria Uzinduzi Kitabu cha Mwongozo kwa Wapelelezi na Waendesha Mashitaka wa Kesi za Wanyamapori na Misitu kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, wengine pichani ni Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Profesa Jumanne Maghembe (kulia),Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alvaro Rodrigues na kushoto ni Muendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga na Naibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni
 Sehemu ya waliohudhuria wa Uzinduzi Kitabu cha Mwongozo kwa Wapelelezi na Waendesha Mashitaka wa Kesi za Wanyamapori na Misitu kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alvaro Rodrigues akizungumza  wakati wa uzinduzi wa mwongozo kwa wapelelezi na waendesha mashtaka wa kesi za wanyamapori na misitu.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewaagiza wapelelezi na waendesha mashitaka nchini waepukane na vitendo vya rushwa bali wafanye kazi kwa bidii kwa kuweka maslahi ya taifa mbele kwa kuchukua hatua stahiki watu wanaoiba rasilimali za Taifa.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati anazindua mwongozo kwa wapelelezi na waendesha mashtaka wa kesi za wanyamapori na misitu katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Jijini Dar es Salaam.

 Makamu wa Rais amesema mwongozo aliouzindua utasaidia kwa kiwango kikubwa uboreshwaji wa upelelezi na uendeshaji wa kesi zinazohusu wanyapori na misitu nchini.

“Uwepo wa mwongozo huu ni dhahiri unategemewa kutoa matokeo chanya katika mapambano dhidi ya ujangili na uhalifu misitu yetu” Amesisitiza Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa anaimani mwongozo huo aliouzindua utasaidia kukomesha vitendo uhalifu ambavyo vimekuwa vikilisababishia Serikali hasara kubwa ikiwemo uharibifu wa rasilimali za taifa na kupoteza mapato ambayo yangesaidia kuimarisha huduma za kijamii nchini.

Kuhusu sekta ya utalii nchini, Makamu wa Rais amesema pamoja na sekta hiyo kuliingizia taifa mapato mazuri lakini inasikitisha kuona kuwa uwepo wa wanyamapori ambao ndio nguzo kuu ya sekta ya utalii unazidi kupungua kila kukicha hivyo kuwa tishio kubwa kwa uchumi na nchi.

Amesema vitendo vya ujangili vimeendelea kuangamiza wanyama hasa tembo hivyo ni muhimu kwa wapelelezi na waendesha mashtaka kutenda haki bila kuonea mtu kwa watu wanaokamatwa kufanya vitendo hivyo ili viweze kukomeshwa nchini.

“Wazee wetu walilinda na kutunza rasilimali zetu kwa faida yetu nasi tuzitunze kwa ajili ya vizazi vijavyo” Ameeleza Makamu wa Rais

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa kazi ya kupambana na ujangili na utoroshaji holela wa wanyama na viumbe wengine itakuwa endelevu na wale wote  watakaokamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha vitendo hivyo.

Waziri Profesa Maghembe amemwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini kuendesha oparesheni ya maalum ya kukusanya silaha zote ambazo zimekuwa zikitumika kwenye ujangili ili kuhakikisha wanyama hasa tembo wanakuwa salama kwenye maeneo ya Hifadhi za Taifa nchini.

Naye, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2014/2017 ofisi yake imewafikisha mahakamani washtakiwa wakubwa wa ujangili ambao walikuhumiwa vifungo virefu na faini.

Amesema kuwa washtakiwa 100 walihukumiwa kulipa faini ya zaidi ya shilingi bilioni 1.1 kwa kujihusisha na nyara za Serikali kinyume na sheria na faini hizo zimehalipwa Serikali.

Ameeleza kuwa kati ya idadi hiyo watuhumiwa zaidi ya 80 walihukumiwa kifungo cha miaka 20 hadi 30 gerezani na faini ya zaidi ya shilingi milioni 164 ambazo bado hazijalipwa Serikalini.


Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali Biswalo Mganga amesema mafanikio hayo yote yamechangiwa na usimamizi madhubuti wa kesi hizo kupitia dawati la wanyamapori katika Divisheni ya Mashtaka pamoja na Mawakili wa Serikali katika Ofisi zote za mikoani nchini.

Ameeleza kuwa changamoto kubwa wanayokutana nayo kwenye kazi kwa sasa ni dhamana kwa watuhumiwa wakubwa wa vitendo vya ujangili ambapo utafiti uliofanywa Mahakama za mkoa wa Dar es salaam tu katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015 unaonyesha kuwapo kwa jumla ya mashauri 13 yanayohusishwa na nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 800 zilizokamatwa ndani na nje ya nchi ambapo watuhumiwa wake walipewa dhamana na kutoweka.

Biswalo Mganga amesema katika mashauri hayo asilimia 69 walikuwa ni raia wa kigeni na asilimia 31 ni raia wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.