Habari za Punde

Hutuba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Akiahirisha Mkutano wa Sita wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufunga Mkutano wa Sitai wa Baraza la Tisa laWawakilishi Zanzibar uliokuwa ukijadili Bajeti ya Serikali ya mwaka 2017/2018 katika Ukumbi wa Baraza hilo uliopo Chukwani nje kidogo ya Kusini mwa Mji wa Zanzibar.
Na.Othman Khamis .OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  ameonya kwamba kuanzia sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitowavumilia Madaktari wanaofanya uzembe wakati wa kutoa huduma za Afya kwa Wananchi wanafika Hospitalini kupata huduma za matibabu.

Alisema Serikali haitosita kumfukuza kazi mara moja Daktari ye yote atakayebainika kufanya uzembe  wa makusudi bila ya kujali jina au sifa alizonazo Daktari husika.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo wakati akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa Sita wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar lililojadili Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 2017/2018 kwenye ukumbi wa Baraza hilo Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema dhamira ya Serikali kupitiA Wizara husika ya Afya ni kutoa huduma bora  yaliyobainishwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wakichangia Hotuba ya Wizara ya Afya.

Balozi alisema yapo malalamikombali mbali ya kiutendaji hasa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja yaliyojitokeza  ambayo huleta kero na maudhi kwa Wananchi wanaofika kupata huduma za matibabu.

Alitanabahisha wazi kwamba  baadhi ya Madaktari wamekuwa na tabia sugu ya kutotekeleza wajibu na majukumu yao wakati wengine wakipenda kutumia lugha chafu zinazowavunja moyo wagonjwa.

Alisema hatua hiyo inakera na kuchukiza Wananchi kutokana na kufikia huduma zinazotolewa kamwe hazilingani na fedha nyingi zinazotolewa na kugharamiwa na Serikali kwa kila Mwezi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba vipo vifaa kufanyia uchunguzi kwa wagonjwa ambavyo kufanyiwa hujuma kwa makusudi ili wahusika wawaelekeze wagonjwa  kwenda kwenye Hospitali zao au zile wanazopewa baghshishi.

Alisema kitendo hicho kisichokubalika si cha haki kufanyiwa wagonjwa ambao wengi wao ni maskini na baadhi yao hutoka masafa ya mbali kama Vijijini kufuata huduma za matibabu Hospitali za rufaa.

Akizungumzia migogoro ya ardhi  Zanzibar licha ya Serikali kuanzisha Kamisheni ya  ardhi kwa lengo la kuodnosha migogoro hiyo kupitia Mamlaka ya Ardhi Balozi Seif alisema bado tatizo hilo halijapatiwa ufumbuzi kutokana na baadhi ya Watu hawajali kufuata sheria.

Alisema hivi sasa Kamisheni ya Ardhi ipo katika hatua za kutayarisha Sera mpya ya Ardhi, kuweka usimamizi imara wa Ardhi pamoja na upangaji wa matumizi bora ya Ardhi.

Balozi Seif alieleza kwamba Serikali kufuta maeneo yote ya Ardhi ili yarudi Serikalini na kupangwa upya.

Alifahamisha kwamba kuanzia sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitomvumilia mtu ye yote ambae atasababisha migogoro ya Ardhi hata kama ni Kiongozi au Mwananchi wa kawaida.

Kuhusu suala la mchanga Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema baadhi ya Wananchi na Wafanyabiashara  ya mchanga hawakuielewa vyema azma ya Serikali katika kudhibiti uchimbaji holela wa rasilmali hiyo.

Balozi Seif alieleza hatua iliyochukuliwa ilikuwa na dhamira ya kuweka utaratibu mzuri wa matumizi bora ya rasilmali hiyo ambapo Jamii inapaswa kuelewa kuwa kadri inavyotumika kwa kasi rasilmali hiyo ndivyo inavyoendelea kumalizika.

Alisema Serikali haina nia ya kuwadhulumu Wananchi wake licha ya kuwepo malalamiko mengi ya Baadhi waliokuwa wakimiliki maeneo ya vitalu vya mchanga wakidai kuchukuliwa maeneo yao.

Hata hivyo Balozi Seif amewataka Wananchi wenye madai ya kuchukuliwa maeneo yao ya vitalu vya Mchanga wawasilishe vielelezao vyao katika Taasisi husika na aliwaahidi kero zao kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wananchi wakiwemo wafanya biashara, Mashirika ya Serikali, Taasisi Binafsi, Asasi za Kidini na watu binafsi kwa kujitokeza kwa moyo wao wa dhati wa kuwasaidia ndugu zao waliopatwa na Majanga kufuatia mafuriko ya mvua za Masika.

Alisema mvua kubwa za masika zimesababisha maafa yaliyoikumba Mikoa yote ya Zanzibar pamoja na upepo mkali uliotokea katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar ikiwemo Fukuchani Wilaya ya Kaskazini A, Mwanakwerekwe, Kinuni, na Nyarugusu kwa Wilaya ya Magharibi B na Changaweni Wilaya ya Mkoani, Pemba.

Balozi Seif alisema kufuatia maafa hayo, miundombinu kadhaa ikiwemo nyumba zipatazo 150, barabara na madaraja yaliharibika pamoja uharibifu mkubwa wa mazao hali iliyopelekea Idadi kubwa ya wananchi kukosa makaazi na kupatiwa hifadhi kwa ndugu, jamaa na majirani.

Mkutano huo wa Sita wa Baraza la Tisa la Wawakilishi pamoja na kupitisha Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2017/2018 pia ulijadili na kupitisha miswaada Mitano ya Sheria.

Miswaada hiyo ni Mswaada wa sheria ya marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma nambari 4 ywa Mwaka 2015, Mswaada wa sheria ya matumizi { Appropriation Bill} pamoja na mswaada wa sheria ya Fedha { Finance Bill }.

Mwengine ni Mswaada wa Sheria wa kuweka masharti bora ya usimamizi wa Ushuru wa Stempu na Mambo mengine yanayohusiana na hayo na kufuta Sheria ya Ushuru wa Stempu ya Mwaka 1996 pamoja na mswaada wa Sheria ya kuweka Vifungu vya uanzishaji wa Kodi itakayojuilikana kama Ushuru wa Bidhaa na huduma zinazoingizwa na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Baraza la Wawakilishi limeahirishwa hadi asubuhi ya Jumatano ya Tarehe 27 Septemba Mwaka huu wa 2017.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.