Habari za Punde

JAMII IMEHIMIZWA KUZINGATIA UZAZI WA MPANGO

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Otilia Gowele (wa kwanza kushoto) akimsikiliza Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Irenius Ruyobya (haupo pichani) alipotembelea banda la ofisi hiyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani iliyofanyika leo katika viwanja vya Mwembe yanga wilayani Temeke jijini Dar es Salaam. Katikati ni Kaimu Mwakilishi Mkazi wa UNFPA Dkt. Hashina Begum na kulia ni Mratibu wa Idadi ya Watu kutoka Tume ya Mipango Ibrahim Kalengo.
Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (wa pili kushoto) Irenius Ruyobya akimuelimisha mmoja wa wananchi waliotembelea banda la ofisi hiyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani iliyofanyika leo katika viwanja vya Mwembe yanga wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
Mkutubi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Issa Magabiro (wa
kwanza kulia) akitoa maelezo juu ya huduma zinazotolewa na ofisi hiyo kwa baadhi ya wananchi wa Dar es Salaam wakati wa  Maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani iliyofanyika leo katika viwanja vya Mwembe yanga wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

Kikundi cha ngoma cha Malezi Cultural Group kikitumbuiza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani iliyofanyika leo katika viwanja vya Mwembe yanga wilayani Temeke jijini Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA EMMANUEL GHULA)
Na: Veronica Kazimoto
JAMII imehimizwa kuzingatia uzazi wa mpango ili kupata familia bora ambazo watamudu kuzihudumia katika mahitaji muhimu ambayo ni elimu, chakula na malazi.
Hayo yamesemwa  na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Otilia Gowele wakati wa maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Mwembe Yanga.
Dkt. Gowele amesema ni muhimu kwa jamii kutumia njia za uzazi wa mpango ili kupanga familia waitakayo na yenye tija katika kuihudumia kwenye mahitaji muhimu.
“Leo tunaadhimisha Siku ya Idadi ya Watu Duniani yenye kauli mbiu isemayo ‘Uzazi wa Mpango; Huwezesha watu; Huendeleza Mataifa’. Hii inatukumbusha kwamba, kila mmoja wetu anatakiwa kutumia njia za uzazi wa mpango ili kupata familia iliyo bora ambayo anaweza kuimudu.


Tukiwa na familia ambazo zinazingatia uzazi wa mpango, tutapunguza vifo vya akina mama wajawazito, tutasaidia watoto kukua wakiwa na afya njema kwa kupata mahitaji yao muhimu pamoja na kuiwezesha Serikali kuwahudumia wananchi wake,” amesema Dkt. Gowele
Amesema Wizara ya Afya itaendelea kuhimiza wananchi kutumia uzazi wa mpango ili kufanikisha azma ya Serikali katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na wananchi wenye afya bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shughuli za Kitwakimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Irenius Ruyobya amesema kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania wa Mwaka 2015/16, amesema takribani wanawake 4 kati ya 10 walioolewa ambao ni sawa na asilimia 38 wanatumia njia yeyote ya uzazi wa mpango.
Amesema asilimia 32 ya wanawake hao wanatumia njia za kisasa na asilimia 6 wanatumia njia za asili. Njia ya kisasa inayotumika zaidi ni sindano kwa asilimia 13 ikifuatiwa na vipandikizi kwa asilimia 7 na vidonge kwa asilimia 6.
Irenius Ruyobya amesema kuwa NBS itaendelea  kutoa takwimu rasmi zinazohusiana na masuala ya afya kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na wadau wengine ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango mbalimbali ya kuwahudumia wananchi wake.
Maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani huazimishwa kila mwaka tarehe 11 Julai ambapo mratibu mkuu ni Tume ya Mipango chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ikishirikiana na Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Idadi ya Watu Duniani (UNFPA)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.