Habari za Punde

Maandalizi ya Bonanza la kimichezo kisiwani Pemba yazidi kufana


Mbarouk Songoro, Bingwa Mtetezi wa Mbio za Baiskeli akiwa akielekea Kojani kuungana na Team Rafiki iliyopiga kambi Kisiwa cha Kojani kwa madhumuni ya kutafuta vipaji vya waogeleaji.

Ali Othman Ali, Pemba

Maandalizi ya Tamasha la kimichezo kisiwani Pemba linalojulikana kama Pemba weekend Bonanza yanazidi kufana ambapo timu ya Rafiki network inaendelea kusaka vipaji  vya washiriki katika michezo mbali mbali.

Tarehe 23 Julai 2017 Timu ya Rafiki network iliwasili katika kisiwa cha Kojani kwa ajili ya kusajili vijana wenye uwezo wakushiriki mashindano ya  kuogelea.

Jumla ya waogeleaji tisa kutoka kisiwa cha kojani wamethibitisha kushiriki  katika mashindano hayo ambayo yamepangwa kufanyika katika fukwe za vumawimbi siku ya tarehe 30 Julai 2017.

Akizungumza na washiriki hao mara baada ya kuwasili katika kisiwa cha kojani Mratibu wa Matukio na Matamasha wa Kampuni ya  Rafiki Network Nd. Salim Jabu Dawa amesema  ingekua si busara kufanya mashindano ya kuogelea kisiwani Pemba bila kushirikisha waogeleaji kutoka kisiwa cha Kojani.

“Tumeamua kuja hapa kojani kusaka vipaji vya waogeleaji kwani ingekua sibusara kufanya mashindano haya bila kuishirikisha  waogeleaji kutoka kisiwa cha kojani” amesema Mratibu wa Matukio na Matamasha wa Kampuni ya  Rafiki Network Nd. Salim Jabu Dawa.

Tamasha hilo la Kimichezo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku ya Ijumaa tarehe 28 Julai 2017 kwa mchezo wa Ng’ombe utakaofanyika chwale mbapo siku ya Jumamosi ya tarehe 29 Julai resi za baiskeli hatua ya mchujo zitafanyika zikijumuisha washiriki 67 na siku ya Jumapili Julai Tamasha litafikia kilele kwa kushuhudia resi za baiskeli mzunguko wa pili utakao wakutanisha washiriki 30.

Siku hiyo ya kilele cha tamasha jumla ya waogeleaji 70 wataonesha umahiri wao kabla ya Mchuano mkali wa Ngalawa  ambapo jumla ya Ngalawa 23 kutoka maeneo mbali mbali kisiwani Pemba zitachuana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.