Habari za Punde

Dhamira ya Serikali ni kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi


Na Habiba Zarali -PEMBA

Dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, inayoongozwa na Dk, Ali Mohamed Shein, ni kuwawezesha Wananchi  kujikwamuwa Kiuchumi ,kujipatia  ajira , kuongeza kipato chao na kujiletea maendeleo kupitia sekta ya Ushirika.

Ili kufikia lengo na dhamira hiyo  ya Serikali ni lazima kufanywa tathmini ambayo  itawawezesha Wadau kujuwa na kupima kwa pamoja kiwango cha ufanisi wa utekelezaji,gharama zilizotumika dhidi ya matokeo  yakiwemo huduma au manufaa yaliopatikana kwenye jamii kupitia miradi inayosimamiwa na Serikali kupitia sekta hiyo.

Hayo yalielezwa na Katibu Tawala Wilaya ya Chake Chake, Rashid Abdalla Ali, kwa niaba ya mkuu wa Wilaya hiyo, Salama Mbarouk Khatib huko katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari Madungu Pemba,wakati alipokuwa
akifunguwa Warsha ya tathmini ya utekelezaji wa mpango wa kuimarisha huduma za Fedha Vijijini.

Alisema Wizara ya Kazi kupitia Idara ya Maendeleo ya Ushirika , inatekeleza mpango wa kuimarisha huduma za fedha Vijijini, kwa msaada wa kifedha na wa kiufundi kutoka mpango wa miundo mbinu ya masoko, uongezaji thamani ya mazao na huduma za fedha Vijijini (MIVARF).

“ Lengo la mpango huu wa kuimarisha huduma za fedha vijijini , kutainuwa mipango ya uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma za fedha kwa Wazalishaji  na Wajasiriamali wadogo wadogo walioko Vijijini,” alisema.

Salama ,alifahamisha mpango huo unalenga kuimarisha uwezo wa utendaji wa Saccos , pamoja na asasi nyengine ndogo ndogo za fedha zikiwemo upatu na visanduku, ili ziendeshwe katika mfumo rasmi , utawala bora na uendeshaji wa kitaalamu wenye kuimarisha usalama wa fedha za watu wanyonge na wenye kipato cha chini.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Chake Chake Pemba, Salama Mbarouk Khatib , alisema mpango wa Idara na  sera ya Vyama vya Ushirika , ni kuvifanyia mageuzi vyama vya Ushirika kuwa taasisi imara za kiuchumi ambazo zitatowa huduma zenye tija na mafanikio ili kufikia hatuwa ya kimaendeleo.

Alieleza kuwa ni matarajio ya Serikali kuona   Wanaushirika wataendeleza yale yote yalioelekezwa ili kufikia dhamira ya Serikali katika kuinuwa maisha ya Wananchi hususan wa Vijini ili kuinuwa Vipato vyao kupitia sekta hiyo.

Kwa upande wake Mrajis Idara ya Vyama vya Ushirika Zanzibar, Khamis Daudi Simba, aliwataka Wanaushirika kuwa tayari kubadilika ili kuvifanya vyama vyao kuwa mkombozi wa maisha ya Wanachama na kukuza pato la Taifa.

Alisema ni wajibu wa Wanachama kuondowa mashaka ya kujiunga pamoja katika Benk za Ushirika za Kiwilaya na kuwa tayari kumpeleka mtu Mahakamani iwapo watamuona Kiongozi wa taasisi hizo anatumia fedha za wanyonge walizo ekeza kwa maslahi yake binafsi.

Simba,aliwataka Wanasaccos kuweka kumbukumbu ili kuweza kuepukana na janga la wizi pale wanapoeka pesa zao kwenye Benk hizo, pale zitakapo kuwa tayari kuanzishwa kwani lengo la Serikali ni kuon fedha za Wananchi zinabaki kuwa salama .

“ Tunataka fedha za Wananchi wanaoekeza katika Saccos ziweko mahala maalumu yaani Benk na zile chache tu ndio zibaki kwenye chama wenyewe” alisema Simba.

Nao Washiriki wa Warsha hiyo, walisema ushirikiano kati ya Viongozi na Wanasaccos wenyewe  ndio kutakako peleka mbele mafanikio ya Saccos na Serikali kwa ujumla.

Hivyo walieleza  juhudi za pamoja kati ya  Viongozi wa Idara ya Vyama vya Ushirika na Wanachama zinahitajika  katika kushirikiana ili kuona malengo ya Serikali yanafikiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.