Habari za Punde

MISA TANZANIA YATANGAZA MATOKEO YA UTAFITI WAKE KWENYE OFISI ZA SERIKALI

Mwenyekiti wa Misa Tanzania, Salome Kitomari

Na.George Binagi @BMGHabari
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika MISA tawi la Tanzania (MISA Tanzania),  umeonesha kwamba bado kuna changamoto kwenye upatikanaji wa taarifa za umma katika ofisi mbalimbali za serikali nchini.

Matokeo ya utafiti huo yanaashiria kwamba bado hakuna uwajibikaji wa moja kwa moja kwenye sheria ya Haki ya kupata taarifa ya mwaka 2016 na pia sera ya serikali kuhimiza matumizi ya teknolojia katika kutoa taarifa za umma.

Ripoti hiyo ya MISA Tanzania ya mwaka 2017 ililenga kubaini ni ofisi gani ya serikali kati ya Serikali Kuu (Ofisi ya Mkuu wa Mkoa) na Serikali za Mitaa (Ofisi za Halmashauri za Majiji na Manispaa) inatoa taarifa za umma kwa urahisi na ipi ni kikwazo kwa utoaji wa taarifa hizo.

Utafiti huo uliodumu kwa muda wa siku 21 ulihusisha mikoa saba ambayo ni Dodoma, Mbeya, Kigoma, Arusha, Mwanza, Mtwara pamoja na Dar es salaam ambapo watafiti walitumia njia za simu, barua pepe na ana kwa ana kuomba na kufuatilia taarifa katika ofisi husika.

Maksi za chini kwenye utafiti huo zilikuwa ni 0 na maksi za juu zilikuwa ni 20 ambapo kuliwa na dodoso mbili za utafiti na hivyo kufanya jumla ya maksi za juu kuwa 40. Ufafanuzi wa maksi hizo ni kwamba ofisi iliyopata maksi 0-6 inaashiria ina usiri katika utoaji ya taarifa za umma, maksi 07-13 ni ofisi iliyoonesha kiwango cha kawaida katika utoaji wa taarifa za umma na maksi 13-20 ni ofisi iliyoonesha uwazi wa kutia matumaini katika utoaji wa taarifa za umma.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ilipata maksi 16/40 huku Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ikipata maksi 25/40 na hivyo ofisi ya Manispaa ya Dodoma kuongoza kwa utoaji wa taarifa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ilipata maksi 21/40 huku ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya ikipata maksi 36/40 hivyo ofisi inayotoa taarifa za umma kwa uwazi mkoani Mbeya kuwa halmashauri ya Jiji la Mbeya.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ilipata maksi 31/40 na Ofisi ya Manispaa ya Kigoma ikipata maksi 13/40 na hivyo kufanya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuwa ofisi inayotoa taarifa za umma kwa uwazi.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ilipata maksi 31/40 na Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Arusha ikipata maksi 30/40 na hivyo kufanya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuwa ofisi inayotoa taarifa za umma kwa uwazi.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ilipata maksi 09/40 na Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikipata maksi 09/40 na hivyo kuashiria kwamba ofisi zote zina usiri kwenye utoaji wa taarifa za umma.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ilipata maksi 12/40 na Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara kupata maksi 08/40 na kuashiria kwamba ofisi zote zina usiri kwenye utoaji wa taarifa za umma.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ilipata maksi 03/40 na Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaa ikapata maksi 22/40 na hivyo kufanya ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kuwa ofisi inayongoza kutoa taarifa za umma.

Utafiti huu unaashiria kwamba asilimia kubwa ya wananchi hawanufaiki moja kwa moja na sheria ya Haki ya Kupata Taarifa ya mwaka 2016 katika ofisi za umma huenda kutokana na kutoijua vyema sheria hiyo jambo linalosababisha taarifa zenye maslahi kwa umma kuendelea kuwa siri na wakati mwingine kuibua mkanganyiko katika jamii.

Baadhi ya viongozi wa serikali nao bado wanaonekana kuwa wagumu katika utoaji wa taarifa za umma huenda kutokana na kutoitambua vyema sheria hiyo hivyo kuna kila sababu pande zote mbili kwa maana ya viongozi na wananchi kuendelea kujengewa uwezo ili kuitambua vyema kwa ajili ya manufaa ya jamii, kwani utoaji wa taarifa kwa uwazi ni kichocheo cha maendeleo.

Taasisi ya MISA Tanzania inahimiza ripoti ya utafiti huo uliotokana na mkoa mmoja mmoja kila kanda nchini, kutumiwa na ofisi nyingine katika kujitathmini namna zinavyotoa taarifa zake kwa umma huku ikitaka teknolojia kupewa kipaumbele ikiwemo matumizi ya barua pepe badala ya wananchi kujazana kwenye ofisi za serikali kufuatilia majibu kutoka kwa watumishi wa serikali na hivyo kupoteza raslimali pesa na muda.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.