Habari za Punde

Mrajis wa Michezo Uso Kwa Uso na ZAHA, Sasa Wapanga Mikakati Mipya Baada ya Kukaa Miaka 3 Pasipo Kuchezwa Ligi Kuu.

Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Mrajisi wa vyama vya michezo vya Zanzibar Suleiman Pandu Kweleza amekutana na kamati tendaji ya muda ya chama cha Handball kwa kujadili masuala mbali mbali ya chama hicho ikiwemo kufanya uchaguzi, kikao ambacho kimefanyika Afisi ya Mrajis iliopo Mwanakwerekwe.

Kweleza amesema lengo la kukutana na kamati tendaji ya chama hicho cha mpira wa mikono ni kujadili vipi watafanya uchaguzi kwa kufata katiba na maelekezo ya Baraza la Michezo Zanzibar ambapo viongozi wa mchezo huo wamemuahidi Mrajis huyo kufanya haraka kuendesha uchaguzi huo.

“Tumekutana na kamati tendaji ya chama cha Hand Ball Zanzibar kwa kujadili mambo mbali mbali ukiwemo uchaguzi, na viongozi hawa wameniahidi kuharakisha kufanya uchaguzi kwa kufata katiba na maelekezo yetu kutoka baraza la Michezo”. Alisema Kweleza.

Nae Salum Hassan ambae ni mjumbe wa kamati ya muda ya chama cha Hand ball Zanzibar amesema chama chao ni kweli walichelewa kufanya uchaguzi kutokana na ukata wa fedha lakini wanawashukuru Baraza kwa kuwaahidi watawasaidia fedha za kuendesha uchaguzi huku akiahidi uchaguzi huo kufanywa kwa haraka kutoka sasa.

“Ni kweli tulikaa muda mrefu hatujafanya uchaguzi lakini nadhani sababu inajulikana kutokana na ukata wa fedha, lakini tunawashukuru baraza kwa kukaa na sisi na kuona kuna umuhimu wa kutusaidia ili tufanye uchaguzi kwa haraka, naamini uchaguzi utafanywa hivi karibuni”. Alisema Salum.

Chama cha Hand Ball Zanzibar (ZAHA) kimekumbwa na migogoro mingi ndani ya miaka mitatu ambapo kimeshindwa hata kuendesha ligi kuu ya Zanzibar ya Hand ball kwa muda wote huo wa miaka mitatu jambo ambalo limepelekea kuwanyima fursa wachezaji na walimu wa mchezo huo ambao wanafanya mazoezi lakini ligi hakuna.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.