Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Shein Azungumza na Bodi ya Ardhi Ikulu Zanzibar

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                                04.08.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachukua juhudi za makusudi kuzihakiki  na kuzitambua eka tatu zilizotolewa kwa wananchi na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume baada ya baadhi yao waliopewa kwenda kinyume na lengo lililokusudiwa.

Dk. Shein aliyasema hayo, alipokutana na uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Wajumbe wa Bodi ya Kamisheni ya Ardhi na Uongozi wa Kamisheni ya Ardhi katika vikao vinavyoendelea Ikulu mjini Zanzibar.

Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa eka zimebadilishwa mwelekeo na baadhi ya wananchi waliopewa eka hizo kwa lengo la madhumuni mazuri wamebadilisha mwelekeo na wengine wamekuwa wakiziuza na wengine wamediriki hata kuzikata viwanja.

Alisisitiza kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha ufumbuzi unapatikana juu ya suala hilo.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja kwa Bodi ya Kamisheni ya Ardhi kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na ukweli kwani kwa muda mfupi imeonesha kupata mafanikio makubwa hivyo ni vyema ikaongeza spidi ili ipate mafanikio zaidi.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuendelea kuyahakiki mashamba yote ya karafuu ya Serikali Unguja na Pemba ili kuweza kuyatambua.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuimarishwa kwa mashirikiano kati ya uongozi wa Wizara, Bodi pamoja na wafanyakazi wa taasisi za Wizara hiyo ili waweze kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Dk. Shein pia, alisisitiza umuhimu wa usimamizi katika kazi kwa viongozi kwani bado kumekuwepo kuoneana muhali, woga na kujenga hofu kwa wafanyakazi ambao wamekuwa wakikeuka maadili, taratibu, sheria na kanuni za kazi.

Aliongeza haja ya kufanya kazi kwa kufuata Sheria na utaratibu bila ya kumpendelea mtu huku akitilia mkazo kufuatwa kwa Sheria ya ardhi pamoja na sheria nyengine zote zinazoendana na taratibu za ardhi pamoja na ile sheria ya Kamisheni ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011.

Kwa upande wa mafanikio, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Bodi ya Kamisheni ya Ardhi kwa mafanikio iliyoyapata sambambana huku akieleza kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi za mwanzo za Afrika ya Mashariki zilizoanza na Sheria za ardhi na si mwanagenzi wa masuala hayo hivyo, ni vyema zikafuata ili mafanikio zaidi yaendelee kupatikana.

Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, alisisitiza azma ya wananchi wa Zanzibar kupewa eka tatu tatu ikiwa ni pamoja na kulima ili waweze kuendesa maisha yao wao na familia zao na si vyenginevyo.

Aliongeza kuwa kisheria kwa wale wote waliopewa heka tatu tatu pale wanapofariki ni lazima warithi warudi serikalini kwa lengo la kurithishwa kwa wale walioorodheshwa lakini ni bahati mbaya kwa baadhi ya wananchi waliopewa heka hizo hawafanyi hivyo.

Balozi Seif alitumia fursa hiyo kuipongeza Bodi hiyo pamoja na kueleza imani iliyopo kwa Bodi hiyo kutokana na uongozi wake.

Mapema Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib  alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara yake kwa kushirikiana na Bodi hiyo katika kutatua changamoto mbali mbali zilizokuwepo na kueleza mashirikiano yaliokuwepo kati ya Wizara hiyo na taasisi nyengine ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee nae kwa upande wake alisisitiza haja ya Bodi hiyo kutembelea katika maeneo ya ardhi badala ya kufanya kazi ofisini pekee kwa lengo la kuonana na wananchi na kutatua changamoto ziliozpo.

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan nae kwa upande wake alisisitiza haja ya kuzijua na kuzifuata sheria zote zinazojikita na masuala ya ardhi hasa ikizingatiwa kuwa eneo la ardhi ndio linaloongoza kwa kuwa na sheria nyingi.

Akitoa maelezo yake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kamisheni ya Ardhi Abdi Khamis Faki alieleza mafanio, dira, mwelekeo, madhumuni na changamoto za Bodi hiyo  ikiwa ni pamoja na kuanza kwa matayarisho ya ramani mpya ya Zanzibar kwa kutumia picha kwa utaalamu wa kisasa (drones).

Nae Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi Rashid Abdulrahman Rashid alieleza mafanikio yaliopatikana katika Kamisheni hiyo ya Ardhi kwa kipindi kifupi pamoja na kueleza jinsi mashirikiano mazuri wanayoyapata kutoka kwa Washirika wa maendeleo ikiwemo nchi ya Finland katika kutekeleza miradi mbali mbali ukiwemo mradi wa kujenga uwezo wa taasisi zinazohusika na sekta ya ardhi.

  Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.