Habari za Punde

Wizara ya Elimu yatakiwa kuyafanyia matengenezo madarasa na madawati yanapoharibka ili kuepusha hasara

 Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud akikagua madarasa ya skuli ya msingi Jang’ombe ‘B’ yaliyofanyiwa ukarabati na kampuni ya Bima Jubilee ikiwa ni sherehe ya kutimiza miaka 80 tokea kuanzishwa. Kulia, ni Mwalim Mkuu wa skuli hiyo Bi. Salila Adam Sadik.
 Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud akikata utepe kuashiria uzinduzi wa madarasa sita yaliyofanyiwa ukarabati na kampuni ya Jubilee katika skuli ya Jang’ombe ‘B’. Wa kwanza kushoto ni Kamishna wa mamlaka ya  usimamizi wa Bima Zanzibar Mohammed Ameir, akifuatiwa na Meneja wa Bima Jubilee Zanzibar Abdulrauf Suleiman pamoja na Mwenyekiti wa kamati ya skuli ya Jang’ombe ‘B’ Taifani Vuai Makame.

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud akimtunuku cheti Meneja wa kampuni ya Bima Jubilee Zanzibar Abdulrauf Suleiman kwa kuthamini mchango wake wa kampeni ya mimi na wewe katika hafla iliyofanyika skuli ya msingi Jang’ombe mjini Zanzibar.

Meneja wa Kampuni ya Bima Jubilee Zanzibar Abdulrauf Suleiman (katikati) katika picha maalum na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud pamoja na Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Jang’ombe ‘B’ Bi. Salila Adam Sadik.

Picha na Makame Mshenga

Na Miza Kona-MAELEZO ZANZIBAR   
   
Mkuu wa Mkoa Mjini magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud, ameitaka  Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuweka mpango maalum wa kuyafanyia matengenezo madarasa na madawati pale yanapoharika ili kuepusha hasara. 

Ameyasema hayo huko Skuli ya Msingi Jang’ombe katika hafla ya Uzinduzi wa Madarasa sita yaliyofanyiwa matengenezo na Kampuni ya Bima ya Jubilee katika kusheherekea miaka 80 tangu kuanzishwa kwake.

Alisema mpango huo mbadala utasaidia kupunguza gharama za matengenezo na kuweka majengo katika mazingira mazuri yatayomwezesha mwanafunzi kusoma katika hali ya kuridhisha.

Alisema kuwepo utaratibu wa kuwatoza fidia kwa mwanafunzi au raia yeyote atakaharibu kitu ili kuweza kudhibiti majengo na vifaa vya skuli na kuiepushia serikali hasara ya kuyafanyia matengenezo kwa gharama kubwa.

Alieleza kuwa serikali inachukua jitihada ili kuhakikisha skuli zote zake zote zinapatiwa madawati ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

“Tatizo la madawati katika skuli litafikia ukomo wake mwishoni mwa mwaka huu,” alifahamisha Mhe. Ayoub.
Mkuu huyo wa Mkoa amewaomba wazazi na walezi kujiunga na bima ya elimu  kwa ajili ya watoto wao ili kuwekeza  katika elimu na kuwajengea mazingira mazuri ya maisha yao ya baadae.

Aidha alieleza kuwa kuna changamoto nyingi katika jamii hasa kwenye sekta ya elimu na afya, hivyo jamii inatakiwa kushirikiana ili kuzipatia ufumbuzi wa pamoja kasoro zinazojitokeza.

Ayoub pia ameipongeza kampuni ya Bima ya Jubilee kwa mchango wake huo wa kiunga mkono serikali katika sekta ya elimu na kuwataka wadau wengine kutoa michango yao katika huduma za kijamii ili kuleta maendeleo nchini.

Alikabidhi cheti kampuni hiyo kwa kuwa mdau mkuu wa kutoa mchango katika huduma za jamii na kuunga mkono kampeni ya Mimi na Wewe.

Akisoma risala, Meneja wa kampuni ya Bima Jubilee Zanzibar Abdulrauf Suleiman alisema kampuni yake imejitolea kukarabati madarasa sita katika sehemu zilizobomoka, sakafu pamoja na kuta, kuweka madirisha, milango na kupaka rangi ndani na nje ili  kuwaondoshea watoto kero zinazowakabili na kujali afya zao wakati wa masomo.

Aidha ameitaka jamii kuzitunza mali za serikali kwa kuzingatia kwamba skuli ni  mali ya jamii hivyo ni wajibu kuzienzi na kuzilinda ili ziweze kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Mapema akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Kamati ya skuli ya Jang’ombe Taifani Vuai Makame, alisema tatizo kubwa la skuli hiyo ni kuvuja kwa paa lake wakati wa mvua, hali inayofanya wanafunzi wasiweze kuendelea na masomo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.